July 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

ACT-Wazalendo yataka wanajeshi watenganishwe na siasa

Jenerali Venance Mabeyo, Mkuu wa Majeshi Tanzania anayemaliza muda wake

Spread the love

 

CHAMA cha ACT-Wazalendo nchini Tanzania, kimeishauri Serikali kutowateua wanajeshi katika nafasi za uongozi wa umma, ili kuwatenga na siasa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Ushauri huo ulitolewa na Msemaji wa Sekta ya Ulinzi wa ACT-Wazalendo, Masoud Abdallah, akizungumza na wanahabari jana Alhamisi, tarehe 19 Mei 2022, jijini Dar es Salaam.

Abdallah alidai kitendo cha wanajeshi kuteuliwa katika nafasi za uongozi kama ukuu wa mikoa na wilaya, unaleta taswira kwamba kuna uhusiano wa karibu kati ya jeshi na chama tawala katika kujiimarisha madarakani.

“Serikali imekuwa na utamaduni wa kuwateua maafisa wa vyombo vya dola waliopo kazini na wastaafu, kushika nafasi za kisiasa kama vile wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya. Uzoefu na uchambuzi wa majukumu na vitendo vya wakuu wa wilaya na mikoa, ni vigumu kutenganisha wajibu wao na viongozi wa chama tawala,” alisema Abdallah.

Msemaji huyo wa sekta ya ulinzi wa ACT-Wazalendo, alitaka wanajeshi waachwe watekeleze majukumu yao ya kijeshi, kwani kitendo cha baadhi yao kuteuliwa serikalini, kinawafanya walioko kazini kutozingatia maadili yao kazi kwa kuanza kujipendekeza kwa watala ili kupata teuzi.

Katika hatua nyingine, Abdallah aliishauri Serikali kuwaunganisha wanajeshi katika mfumo wa bima ya afya ya taifa (NHIF), ili waondokane na changamoto za upataji matibabu hasa kwa wanaostaafu ambao Serikali haigharamii matibabu yao wanapoondoka kazini.

“Licha ya malalamiko na ahadi ya Serikali ya kuanzisha bima ya afya kwa ajili ya wanajeshi lakini hadi sasa bado serikali haijawaunganisha wanajeshi katika mfumo wa bima ya afya ya taifa. Athari za utaratibu huu unakuwa na madhara makubwa zaidi kwa wastaafu ambao kwa mujibu wa sheria na kanuni, Serikali inagharamia matibabu kwa wanajeshi waliopo kazini pekee kupitia vituo na hospitali maalum za jeshi.”alisema Abdallah.

error: Content is protected !!