RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali yake lazima imuenzi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kwa kutekeleza miradi ya maendeleo katika jimbo lake la Ruangwa, ili kuenzi mchango wake katika kulitumikia taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Lindi … (endelea).
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Ruangwa Mjini, mkoani Lindi, leo tarehe 18 Septemba 2023, Rais Samia amesema Majaliwa wadhifa wake ni mkubwa hivyo lazima atunzwe.
“Wana Ruangwa mmesema maendeleo ni mengi na mengi yako njiani yanakuja. Waswahili wanasema mcheza kwao hutunzwa, kwa nini tusimtunze waziri mkuu kwa maendeleo. Lazima Serikali tumtunze kwa maendeleo. Wadhifa wake ni mkubwa, kazi yake ni kubwa ya kushughulikia Tanzania nzima lazima tumuangalie nyumbani kunakaa sawasawa lazima tulete maendeleo Ruangwa,” amesema Rais Samia.
Mbali na kufikisha maendeleo Ruangwa ili kumuenzi Waziri Majaliwa, Rais Samia amesema Serikali itaendelea kupeleka fedha za maendeleo mkoani Lindi, ili kuifungua kiuchumi huku akiahidi kutumia rasilimali zilizopo katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Rais Samia amesema, kwa mwaka wa fedha uliopo Serikali yake imetenga fedha kiasi cha Sh. 77 bilioni, kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Aidha, Rais Samia amesema Serikali itafanya tathmini ili kujua kiwango cha madini yaliyoko Lindi, ili itafute wawekezaji pamoja na kuandaa namna bora itakayowezesha wachimbaji wadogo kuchimba hasa madini ya dhahabu.
Leave a comment