Friday , 3 May 2024
Home Habari Mchanganyiko TUCTA yawasilisha mapendekezo ya viwango vya mishahara serikalini
Habari Mchanganyiko

TUCTA yawasilisha mapendekezo ya viwango vya mishahara serikalini

Spread the love

 

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) limepeleka mapendekezo yake Serikalini ya kutoridhika na nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma iliyoanza mwaka huu fedha huku wakionyesha kushangazwa kwa nyongeza hiyo kutolenga watumishi wote wa umma. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Aidha, Shirikisho hilo limependekeza kwa Serikali nyongeza ya asilimia 15 kwa kima cha juu kutoka asilimia 0.6 iliyoongezwa ambayo wamesema kuna tofauti kubwa sana baina ya nyongeza ya kima cha chini ya asilimia 23.3 hadi asilimia 0.6.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma, Rais wa Shirikisho hilo, Tumaini Nyamuhokya alisema tayari wamewasilisha mapendekezo hayo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishiwa Umma na Utawala Bora ili yafanyiwe kazi.

Alisema baadhi ya watumishi wa taasisi za Serikali wa hawajaguswa kabisa na ongezeko hilo la kima cha chini cha mishahara jambo ambalo limewashangaza wengi hasa ikizingatiwa ni watumishi wa umma vilevile.

Alitaja baadhi ya taasisi hizo ni pamoja na Shirika la Reli Nchini (TRC), Shirika la Ndege la Serikali (ATCL) na Shirika la simu Nchini (TTCL), kada za Afya na Serikali za Mitaa.

Aidha, alisema jambo walilozingatia katika mambo ya msingi kwenye mapendekezo yao ni pamoja na namna nyongeza ya mshahara ilivyofanyika.

Pia alisema kumekuwa na utaratibu ambao haukumridhisha mtumishi yeyote wa umma aliyepewa nyongeza hiyo ya mshahara.

“Hii ni kwa sababu tumeona kiwango cha kima cha chini ni asilimia 23.3 lakini ukitafuta kiwango cha juu tofauti yake ni kubwa mno.

“Kwa hiyo kima cha chini kimeongezwa asilimia 23.3 wakati huyu wa kima cha juu ana asilimia 0.6, hii ni tofauti kubwa mno ambayo haijawahi kutokea na utaratibu wa namna hii huwa haufanyiki,” alisema.

Alisema nia ya Rais Samia Suluhu Hassan ililenga kuongeza mishahara na hakuwa amelenga kuwatoa watu wa daraja fulani kuwapeleka mahala pengine huku akisema ni imani yao nyongeza ya mshahara inagusa kila ngazi ya mshahara wa mtumishi wa umma.

“Kwa hiyo hili nalo tumeliwasilisha lionekane lipo hivyo lakini pia katika nyongeza hiyo kuna baadhi ya kada (baadhi ya taasisi za umma hazipo katika nyongeza hiyo),” alisema.

Nyamuhokya alitolea mfano watumishi hao kuwa ni watumishi wenye mishahara binafsi wakiwemo wale wenye elimu ya darasa la saba inasemekana hao hawasomeki kwenye mfumo wa serikali na hakuna ‘setup’ ya kiwango chao cha mshahara.

Pia alisema wapo waliohama taasisi moja kwenda nyingine na kutokuta cheo chake chake katika muundo na kuhamishiwa kwenye mshahara binafsi nao hawakuguswa na nyongeza hiyo.

“Kwa hiyo tunaona hapo kuna ubaguzi mkubwa na sababu hatuioni nia nini inayofanya ngazi nyingine zisiguswe,” alisisitiza Nyamuhokya.

“Kwa hiyo kiujumla tumejaribu kutazama mambo haya lakini pia hata kiwango chenyewe cha 70,000 bado ukitazama pamoja na kwamba tunashukuru angalau kima cha chini kimetazamwa lakini bado siyo kiwango halisia kinachomtoa mtumishi kwenye adha za maisha ukilinganisha na maisha aghali yaliyopo sasa.

“Kwa hiyo hapo tumegusa kuonyesha kwamba kiendelee kutazamwa na siyo kwamba tumeridhika na nyongeza hiyo bado tunahitaji iongezeke zaidi,” alisema.

Kiongozi huyo alisema baada ya kupeleka mapendekezo hayo wanasubiri majibu ya Serikali ili nao wapeleke kwa wanachama wao.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

RPC Dodoma akabidhiwa bunduki mbili za wahalifu

Spread the love  Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa ya Kulevya...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC yazindua huduma maalum kwa wastaafu

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua huduma maalum kwa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB yazindua akaunti ya Kikundi

Spread the loveBenki ya NMB imezindua akaunti ya kikundi yenye  maboresho makubwa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wafanyakazi waidai STAMICO mishahara ya bilioni 1

Spread the loveWALIOKUWA wafanyakazi wa mgodi wa Shirika la Madini la Taifa...

error: Content is protected !!