Sunday , 19 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kesi ya Mbowe; Mahakama yapokea kielelezo nusu, yakataa kingine
Habari za SiasaTangulizi

Kesi ya Mbowe; Mahakama yapokea kielelezo nusu, yakataa kingine

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mawasiliano mkoani Dar es Salaam, imekubali kupokea sehemu ya hati ya ukamataji mali ya mshtakiwa wa kwanza, Halfan Bwire Hassan, kwenye kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freemam Mbowe na wenzake, Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mbali na Mbowe na Hassan, washtakiwa wengine ni Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya, ambao walikuwa Makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Nyaraka hiyo imepokelewa leo Ijumaa, tarehe 17 Desemba 2021 na mahakama hiyo mbele ya Jaji Joachim Tiganga, akitoa maamuzi madogo dhidi mapingamizi ya upande wa utetezi, juu ya upokelewaji wa hati hiyo.

Akitoa uamuzo huo, Jaji Tiganga amesema amepokea ukurasa na kwanza ya nyaraka hiyo na kutopokea ukurasa wake wa pili, kwa kuwa una mashaka.

“Kuna hoja kwamba vitu vimeorodheshwa na kwamba kuna sahihi ya polisi haina tarehe kuonesha iliwekwa tarehe ngapi, katika hali hiyo mahakama inaona mapungufu yako wazi kwenye kielelezo hiki. Mapungufu hayo yanaleta mashaka na yanakuwa resoved kwenye favor ya mshtakiwa, ikumbukwe kielelezo kina page (kurasa) mbili kwa maana ya kwanza imesainiwa na mashahidi wote na ya pili haijasainiwa na haijawekwa tarehe, mahakama inapokea page ya kwa maana inaachana na page ya pili,” amesema Jaji Tiganga.

Jaji Tiganga alitoa uamuzi huo, baada ya mawakili wa utetezi jana kupinga upokelewaji wa nyaraka hiyo, pamoja na mambo mengine, walidai ukurasa wa pili umeingizwa kinyemela, kwa kuwa haikusainiwa na mashahidi walioshuhudia zoezi la ukamataji mali, pamoja na mshtakiwa mwenyewe, bali ina saini ya shahidi aliyeiomba kuitoa kama kilelezo bila ya kuwa na tarehe iliyowekwa.

Mapingamizi hayo yaliibuka baada ya shahidi wa nane wa Jamhuri, SP Jumanne Malangahe, kuiomba mahakama hiyo ipokee hati ya ukamataji mali zinazodaiwa kuwa za Hassan, kama kielelezo cha upande wa mashtaka, akidai alihusika katika uandaaji wake baada ya kufanya upekuzi na kukamata mali za mshtakiwa huyo, tarehe 10 Agosti 2020, nyumbani kwake maeneo ya Yombo Kilakala, Dar es Salaam.

Kuhusu mapingamizi mengine, Jaji Tiganga amesema, ameyatupa kwa kuwa hayana mashiko kisheria.

Kuhusu mapingamizi yaliyodai nyaraka hiyo haina uwezo wa kupokelewa kisheria, pamoja na kutokuwa na uhusiano ikidaiwa kifungu cha sheria iliyotumika katika kuiandaa hakijatamkwa, Jaji Tiganga amelitupa akisema suala hilo haliathiri upokelewaji wa hati hiyo ya ukamataji mali.

“Uzito wa kuto-cite (tamka) kifungu cha sheria inatibika, basi katika mazingira hayo ambayo ni serious kwenye mazingira ya nyaraka kama hii ni lazima na yenyewe inatibika, basi hoja hiyo ya kwanza imelenga bekenye long citation naiondoa kwa sababu nilizoeleza,” amesema Jaji Tiganga.

Akitoa uamuzi dhidi ya pingamizi lililodai hakuna ushahidi unaonesha shahidi aliyeomba kuitoa nyaraka hiyo, alifanya upekuzi nyumbani kwa mshtakiwa huyo, Jaji Tiganga amelitupa akisema, SP Malangahe alitoa ushahidi huo alipodai alihusika katika ukamataji wa mali, zilizopatikana nyumbani kwake Hassan, kisha akamsainisha katika hati ya ukamataji mali.

Katika pingamizi lililodai kuwa jina lililoandikwa katika hati hiyo ya ukamataji mali kuwa sio la mshtakiwa, ambapo liliandikwa Halifan Bwire Hassan, badala ya Halfan Bwire Hassan, Jaji Tiganga ameliweka kiporo akisema litajadiliwa baadae kwa kuwa lina ubishi na haliwezi kuathiri upokelewaji wa nyaraka hiyo.

“Kuhusu pingamizi lililosema jina lililoandikwa sio la mshtakiwa kwanza, hili linabaki linaubishi na lina ushahidi, ni jambo ambalo haliwezi kuathiri upokelewaji, litajadiliwa baadae wakati mahakama inashughulika na suala lenyewe, hivyo haliwezi kuathiri nyaraka hii kupokelewa,” amesema Jaji Tiganga.

Baada ya Jaji Tiganga kutoa maamuzi hayo madogo, SP Malangahe anaendelea kutoa ushahidi wake.

Katika ushahidi wake, amedai baada ya kufanya upekuzi nyumbani kwa Hassan, walikamata baadhi ya vifaa vya na JWTZ na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ikiwemo sare za jeshi, kisu cha kijeshi na vifaa vya kusafishia silaha.

Mapingamizi hayo yaliibuka mahakamani hapo, baada ya shahidi wa nane wa Jamhuri, Mkuu wa Upelelezi wilayani Arumeru, Arusha, SP Jumanne Malangahe, kuiomba ipokee kama sehemu ya ushahidi wake.

Baada ya kutoa ombi hilo, mawakili wa utetezi wakiongozwa na wakili wa mshtakiwa huyo, Nashon Nkungu, waliweka mapingamizi likiwemo lililodai kuwa nyaraka hiyo haina uhusiano, huku lingine likidai haina uwezo wa kupokelewa kwa kuwa imechukuliwa kwa sheria ambayo haipo.

Pingamizi lingine lilidai kuwa, shahidi aliyeomba kuitoa nyaraka hiyo, ameshindwa kuithibitisha kama ndiyo yenyewe aliyoiandika tarehe 10 Agosti 2020, baada ya kukagua nyumbani kwa Hassan, maeneo ya Yombo Kilakala, Temeke mkoani Dar es Salaam.

Pingamizi lingine lilidai kuwa shahidi huyo hajaonesha mlolongo wa utunzwaji kielelezo hicho hadi kilipomfikia mahakamani hapo (Chain of Custody), wakati anatoa ushahidi.

Lingine lilidai shahidi huyo aliingiza kinyemela taarifa ambazo hazijasainiwa na mshtakiwa pamoja na mashahidi walioshuhudia zoezi la upekuzi huo.

Hata hivyo, Mawakili wa Jamhuri wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, waliiomba mahakama hiyo iyatupilie mbali mapingamizi hayo, wakidai kuwa hayana mashiko kisheria.

1 Comment

  • Asante kwa taarifa kuhusu tukio hilo.

    Karibu ujifunze uwekezaji katika ARDHI NA MAJENGO.

    Tembelea mtandao wa UWEKEZAJI MAJENGO BLOG.

    Rafiki yako,

    Aliko Musa.

    Wa UWEKEZAJI MAJENGO BLOG

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Wakili Mwabukusi anusurika kufungiwa, asema hatarudi nyuma

Spread the loveWAKILI Boniface Mwabukusi amesema kuwa hatorudi nyuma kuwatetea Watanzania na...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

RC Chongolo atangaza ‘vita’ kwa wanaovusha wageni kinyemela

Spread the loveKATIKA kulinda usalama wa nchi kupitia mpaka wa Songwe, Mkuu...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

RUWASA yachongewa, yateketeza mamilioni kwa maji yenye magadi

Spread the loveSAKATA la ukosefu wa maji wilayani Momba mkoani Songwe limezidi...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Lissu akabidhiwa gari lake, aomba msaada wa matengenezo

Spread the loveMakamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu leo Ijumaa amekabidhiwa...

error: Content is protected !!