Friday , 3 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kesi ya Mbowe: NCCR-Mageuzi wamshangaa Rais Samia
Habari za SiasaTangulizi

Kesi ya Mbowe: NCCR-Mageuzi wamshangaa Rais Samia

Anthony Komu, Naibu katibu Mkuu NCCR- Mageuzi
Spread the love

 

CHAMA cha siasa cha upinzani nchini Tanzania cha NCCR-Mageuzi kimeshangazwa na kauli ya Rais wa nchi hiyo, Samia Suluhu Hassan kuhusu mashtaka dhidi ya Freeman Mbowe. Anaripoti Kelvin Mwaipingu…(endelea).

Mbowe ambaye ni kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema pamoja na wenzake watatu, anakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi na kupanga njama za ugaidi. Kesi ipo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Jana Jumanne, Rais Samia akijibu swali la Salim Kikeke, mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) katika mahojiano maalum yaliyofanyikia Ikulu ya Dar es Salaam alisema, kesi dhidi ya Mbowe haina chembe ya kisiasa.

Akijibu swali hilo lililotaka kujua kama mashtaka ya Mbowe yamechochewa na harakati za kisiasa hususan mchakato wa Katiba mpya, Rais Samia alisema “Mimi sidhani kama yamechochewa kisiasa, kwa sababu ninavyojua Mbowe alifunguliwa kesi Septemba 2020, yeye pamoja na wengine na kama ulivyosema mashtaka ya ugaidi na kuhujumu uchumi.”

Rais Samia Suluhu Hassan

Leo Jumatano tarehe 10 Agosti 2021, Naibu Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Anthony Komu akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho, Ilala jijini Dar es Salaam amesema kumshikilia Mbowe, hakutarudisha nyuma harakati za kudai Katiba mpya.

“Rais alisema hii kesi haina chembembe za kisiasa, sisi tunasema ina mabonge ya kisiasa kwa kuwa ni njama chafu na kumshikilia Mbowe wanadhani watazima moto wa kudai katiba mpya, sisi kama NCCR tunasema tutauwendeleza,” amesema Komu

Pia, Komu amekosoa kauli ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro aliyoitoa hivi karibuni kuhusu Mbowe kuwa watu wasimwone Mbowe kuwa hawezi kutenda makossa bali kama wana hisia anaonea wakamuulize.

Komu amesema “Kamanda Sirro hana mamlaka ya kesema Freeman Mbowe ni gaidi na wala sio malaika, huko ni kuvuka mipaka, sisi tumeona kama ni maoni yake binafsi kwa kuwa vyombo vyenye mamlaka vipo.”

Mbunge huyo wa zamani wa Moshi Vijijini amesema, “tuendelee kuheshimu katiba ya sasa licha ya kuwa na pangufu, kwa kuwa kuna sehemu imetuvusha ila tukirekebisha itakuwa vizuri zaidi ya sasa ilivyo.”

Kuhusu tozo za miamala ya simu ambayo imeibua mjadala tangu kuanza kwake hadi Rais Samia kuagiza iangaliwe lakini si kuitoa, Komu amesema “kwenye swala la tozo huu ni ujambazi na unyang’anyi, leo ukitaka kumtumia mzazi wako pesa kijijini Serikali inaanza kukata hela yake, haya ni matokeo ya kuwa na Bunge la chama kimoja.”

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Sabaya afutiwa kesi, ruksa kugombea uongozi

Spread the loveMwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali DPP leo Ijumaa amefuta rufaa...

Habari za Siasa

Serikali yasaka bilioni 3 kujenga daraja Mto Mpiji

Spread the loveSerikali imesema inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kiasi cha...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kwafukuta kisa chaguzi, Lissu aibua tuhuma nzito

Spread the loveCHAGUZI za kusaka viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo...

Habari MchanganyikoTangulizi

Kimbunga “HIDAYA” chaendelea kuimarika, wananchi wapewa tahadhari

Spread the loveMAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa...

error: Content is protected !!