May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mnyika: Rais Samia amepotoshwa

Rais Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

KATIBU Mkuu wa Chama Kikuu cha Upinzania Tanzania, John Mnyika, amedai kwamba, Rais Samia Suluhu Hassan, amepotoshwa kuhusu sheria inayoruhusu vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara na maandamano. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Mwanasiasa huyo ametoa kauli hiyo leo Jumanne, tarehe 10 Agosti 2021, siku moja baada ya Rais Samia kusema sheria za nchi zinaruhusu vyama hivyo kufanya mikutano ya ndani. Kiongozi huyo alitoa kauli hiyo katika mahojiano yake na Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC), yaliyorushwa jana Jumatatu.

Mnyika amesema kuwa, huenda Rais Samia ametoa kauli hiyo kwa kuwa alipotoshwa na wasaidizi wake, ambao hawakumuelewesha vyema juu ya Sheria ya Vyama vya Siasa, inayoruhusu vyama hivyo kufanya mikutano ya hadhara na maandamano.

Katibu Mkuu huyo wa Chadema amesema, kwa sasa chama hicho hakitachukua hatua yoyote dhidi ya kauli hiyo, kwani huenda Rais Samia atafuta kauli hiyo.

“Kama wasaidizi wake walikuwa hawajamuonesha kifungu cha 11 cha Sheria ya Vyama vya Siasa, juu ya haki ya vyama kufanya mikutano ya hadhara na maandamano. Kama walimpotosha hawakumuonyesha sheria inasemajie, wataenda kumueleza rais haya uliyozungumza hayako kwenye msingi wa kisheria, pengine watatoa muelekeo tofauti,” amesema Mnyika.

Mnyika amesema, vyama vya siasa vimeruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara, ili viweze kueneza sera na misimamo yake kwa wananchi.

“Rais ametoa madai kwamba, uchaguzi ukishamalizika katika kile alichokisema cha kujenga nchi na haki za vyama vya siasa zinabaki kuwa haki za chama, kufanya vikao vya kikatiba vya ndani, jambo hili halina msingi wowote wa kikatiba wala kisheria,” amesema Mnyika.

Mnyika ameongeza “ na kauli hii ya rais inakinzana na kifungu cha 11 cha Sheria ya Vyama vya Siasa, ambacho si tu kimetoa fursa na haki kwa vyama kufanya mikutano ya ndani ya kikatiba, bali sheria imekwenda mbele zaidi, imeruhusu vyama vya siasa kuweza kufanya mikutano ya hadhara.”

“Sheria ile imetamka bayana kwamba, vyama vina haki ya kuweza kufanya mikutano hiyo kwa lengo la kupata wanachama, kueneza sera zake na misimamo mbalimbali kwa lengo husika,” amesema Mnyika.

Mnyika amesema zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa, linadhoofisha utendaji wa vyama hivyo.

“Kuvifungia vyama kwenye vikao vya kikatiba vya ndani peke yake, bila haki ya kufanya mikutano na shughuli nyingine zianzoruhusiwa kisiasa, ni mbinu ya kudhibiti vyama vya upinzani dhidi ya kufanya wajibu huo wa kisiasa,” amesema Mnyika.

error: Content is protected !!