Sunday , 19 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Jeshi ladaiwa kutembeza kipigo uraiani
Habari Mchanganyiko

Jeshi ladaiwa kutembeza kipigo uraiani

Spread the love

WATU waliovalia mavazi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wamevamia kijiji cha Kisemvule, wilayani Mkuranga, mkoani Pwani na kuwashambulia wananchi waishio katika eneo hilo, kwa mijeredi, mikanda, ngumi na mateke.

Miongoni mwa walioshambuliwa na kupigwa na “maofisa hao wa jeshi,” ni vijana wanaoendesha biashara ya pikipiki, maarufu kama bodaboda, waliopo katika eneo hilo, anaandika Mwandisi Maalum kutoka Mkuranga.

Haikuweza kufahamika mara moja sababu za “askari” hao kuingia mtaani na kutembeza kichapo kwa wananchi, wala kambi wanayofanyia kazi.

MwanaHALISI Online limeshindwa kumpata Kamanda wa Polisi, mkoa wa Kipolisi wa Kibiti (RPC), Onesmo Lyanga ili kuweza kuzungumzia suala hilo. Mara zote simu yake ya mkononi ilikuwa inaita bila kupokelewa.

Aidha, gazeti limeshindwa kumpata msemaji wa jeshi kufafanua madai kuwa baadhi ya maofisa wake, wamevamia kijiji hicho na “kutembeza kichapo kwa wananchi.”

Hata hivyo, kwa mujibu wa mkanda wa video na kwa mujibu wa baadhi ya wananchi wanaoishi katika kijiji hicho na ambao wameshuhudia tukio hilo wanasema, ni kweli kuwa watu waliovalia nguo za kijeshi wamevamia eneo hilo na kutembeza kipigo kwa wananchi.

Mmoja wa watoa taarifa aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa gazetini anasema, “hapa kwetu Kisamvule, hali si shwari. Ni baada ya wanaodhaniwa kuwa maofisa wa jeshi kuvamia kijijini kwetu na kuanza kuwaporomoshea wananchi kipigo.”

Anasema, “watu wameumizwa sana. Hawa watu waliovalia mavazi ya jeshi, wameanza kupiga waendesha bodaboda, majira ya mchana, jambo ambalo limesababisha taharuki kwa watu kukimbia ovyo.”

Amesema, “baadhi ya waliotembeza kipigo hicho kwa wananchi walikuwa wamevaa nguo za jeshi na wengine walivalia kiraia.”

Anasema, hakuna hata mmoja miongoni mwa waliokuwa wanashambulia raia hao, aliyekuwa anaeleza sababu ya kufanya hivyo.

Mtoa taarifa huyo anasema, “…hakuna anayejua sababu ya maofisa hawa wa jeshi kuingia kijijini na tembeza kipigo hiki kwa wananchi. Wala hakuna anayejua nani aliyowatuma askari hawa wanaolipwa kwa kodi za wananchi, kufanya uharamia huu.”

Anasema, “tumeuliza kwenye ofisi ya mwenyekiti wa kijiji hadi mtendaji wa kata, kote huko tumeelezwa kuwa hakuna taarifa ya kilichosababisha wanajeshi kuingia mtaani na kuanza kupiga raia.”

Taarifa zinasema, miongoni mwa walioathirika na vurugu hizo, ni pamoja na wafanyabiashara wadogo wakiwemo mama lishe, ambao walikimbiwa na wateja waliowapa huduma kuhofia maisha yao.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Balile aukwaa uenyekiti wahariri Afrika Mashariki

Spread the loveJumuiya ya Wahariri wa Afrika Mashariki (EAES), imemchagua Mwenyekiti wa...

Habari Mchanganyiko

Jeshi la Uhifadhi kujengewa uwezo zaidi

Spread the love  WIZARA ya Maliasili na Utalii imejipanga vyema kuendelea kulijengea...

Habari Mchanganyiko

Wanavyuo Dodoma waonja utamu wa chimbo la nyuki

Spread the love  TAMASHA la Chimbo la Nyuki lililofanyika katika Ukumbi wa...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Wakili Mwabukusi anusurika kufungiwa, asema hatarudi nyuma

Spread the loveWAKILI Boniface Mwabukusi amesema kuwa hatorudi nyuma kuwatetea Watanzania na...

error: Content is protected !!