Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Serikali yanena kuhusu viwanda, uvamizi Zanzibar
Habari za SiasaTangulizi

Serikali yanena kuhusu viwanda, uvamizi Zanzibar

Bunge likiendelea na vikao vyake
Spread the love

SERIKALI ya awamu ya tano imetoa taarifa kuhusu mipango ya utekelezaji wa mambo mbalimbali yanayohusu utendaji wa serikali pamoja na utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2016/2017, anaandika mwandishi wetu.

Hii ndiyo taarifa kamili iliyotolewa na serikali;

 TAARIFA KWA UMMA

SERIKALI YAELEZA UTEKELEZAJI WA MASUALA MBALIMBALI BUNGENI

Dodoma, Jumanne, Januari 31, 2017:

Serikali leo imeainisha utekelezaji na kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi katika sekta mbalimbali katika kikao cha kwanza cha Mkutano wa Sita wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Majibu ya Serikali kwa baadhi ya hoja ni kama ifuatavyo:

Ujenzi Nyumba za Walimu 

Akijibu hoja kuhusu ujenzi wa nyumba za walimu, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo, ameliambia Bunge kuwa Serikali ilitenga kiasi cha Sh. Bilioni 13.9 katika Bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu wa Sekondari, na Shilingi bilioni 11.4 kwa nyumba za walimu wa Shule za Msingi.

Aidha, Waziri Jafo ameeleza kuwa tayari nyumba 146 za walimu zimeshajengwa nchini kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari.

Pia amezungumzia Serikali kuanza kulipa madeni ya walimu.

Ujenzi wa Viwanda Nchini

Akijibu swali kuhusu uwekezaji wa viwanda nchini hususani mkoani Tabora ambako kuna kilimo cha Tumbaku na maeneo mengine yenye malighafi, Mhandisi Edwin Ngonyani kwa niaba ya Waziri wa Viwanda ameliambia Bunge kuwa tayari Serikali imeshafanya mazungumzo na wawekezaji kutoka Vietnam na kuzitaka Halmashauri zote nchini kuendelea kuitikia wito wa kutenga maeneo ya uwekezaji.

“Kituo cha uwekezaji Nchini (TIC) kimepewa maelekezo maalum kunadi fursa hii kwa wawekezaji katika sekta ya tumbaku na sigara hapa nchini,” alisema Mhandisi Ngonyani ambaye pia ni Naibu Waziri, Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Tupende Bidhaa Zetu

Akijibu hoja kuhusu bidhaa nyingi za Kenya kuingia nchini, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Suzan Kolimba amesema moja ya changamoto inazozikumba bidhaa za Tanzania ni wananchi wake kupenda vya nje.

“Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali iliunda Kamati ya Kitaifa ya Kudhibiti na Kusimamia Uondoaji wa wa Vikwazo visivyo vya Kiforodha na kuhamasisha wafanyabiashara nchini kuzalisha bidhaa zenye ubora,” alisema.

Serikali yagharamia 100% umeme vijijini

Serikali imesisitiza kuwa inagharamia ujenzi wa umeme vijijini kupitia Wakala wa Kusambaza Umeme Vijijini (REA) kwa asilimia 100. Akijibu maswali ya wabunge, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, alisema wananchi wanalazimika kuchangia Sh. 27,000 tu ambazo ni gharama za kodi ili waunganishiwe huduma hiyo wakati mradi ukiwa unaendelea.

“Lengo ni kuhamasisha na kuwawezesha wananchi wa vijijini wenye vipato vidogo kuweza kupata huduma za umeme kwa gharama nafuu,” alisema akisisitiza kuwa wale ambao huomba huduma hiyo baada ya wataalam wa REA kumaliza kazi yao ndio hulazimika kulipia umeme huo kwa Sh. 177,000 tu badala ya Sh. 320,960/wanazotozwa wakazi wa mijini kwa umbali usiohitaji nguzo.

Bei ya maji kupungua

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge amesema Serikali itaendelea kupunguza gharama za maji nchini hasa vijijini kadiri gharama za umeme zitakavyoendelea kupungua hasa wakati huu nchi inapoingia katika uchumi wa gesi.

Aliongeza kuwa kwa upande wa vijijini miradi ya umeme wa jua na nishati nyingine za bei nafuu pia itasaidia kupunguza gharama za umeme na kusaidia wananchi kupata maji katika miradi mingi inayondelea sasa nchini.

Madai ya Unyanyasaji Zanzibar

Serikali imewataka wananchi wote wanaodai kufanyiwa unyanyasaji na vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kutoa taarifa za matukio hayo polisi ili hatua stahiki zichukuliwe.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema kwa kuwa hakuna tarifa za kuripotiwa kwa matukio hayo katika kituo chochote cha Polisi, atachukua pia hatua za kutuma maafisa wake kufanya uchunguzi zaidi.

 Imetolewa na:

Dkt. Hassan Abbasi,

Mkurugenzi Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!