Friday , 3 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Jecha: Maalim Seif alidanganya
Habari za SiasaTangulizi

Jecha: Maalim Seif alidanganya

Spread the love

MIEZI 15 tangu alipofuta uchaguzi mkuu wa Zanzibar na kushutumiwa kuwa amekibeba Chama Cha Mapinduzi (CCM), mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), amefanya mahojiano na kituo cha televisheni cha Azam Tv, anaandika Jabir Idrissa.

Jecha Salim Jecha amesema alilazimika kuchukua hatua hiyo baada ya uchaguzi kukumbwa na “uharibifu mkubwa” hasa kisiwani Pemba.

Akihojiwa na mwandishi wa habari nguli nchini, Tido Mhando, kupitia kipindi chaFunguka, kinachorushwa na kituo hicho kila Jumapili, Jecha alisema alichukua hatua “peke yake” kama kiongozi wa tume.

Hakutaja mamlaka aliyotumia kufuta uchaguzi tarehe 28 Oktoba 2015, na alikiri kuwa hakushauriana na makamishna wa tume hiyo.

“Mimi ni kiongozi mkuu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, sasa kiongozi unapoona mambo yameharibika, husubiri mashauriano, wewe nahodha, chombo ukishaona kinakwenda mrama, unachukua hatua kwanza ya kuepusha balaa. Ndicho nilichokifanya,” alisema.

Alipotakiwa kubainisha uharibifu ulitokea maeneo gani ya uchaguzi na kama kuna malalamiko yoyote ya vyama, alishindwa kueleza.

“Ndugu mtangazaji mimi nadhani haya tuyawache. Tusubiri ripoti ya uchaguzi wa Zanzibar tutaitoa hivi karibuni, itaeleza kila kitu,” amesema.

Katika hatua nyingine, Jecha amesema Maalim Seif Shariff Hamad, aliyegombea kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), alitoa matokeo ya uongo.

“Hakukuwa na matokeo yale. Alitoa matokeo ya uongo,” alisema, bila ya kueleza matokeo ya kweli ni yepi.

Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alitangaza ushindi wake tarehe 26 Oktoba 2015 kwa kuzingatia matokeo yaliyokusanywa na mawakala wake kwenye vituo vya uchaguzi, yakiwa yameidhinishwa na watendaji wa tume.

Jecha amesema uchaguzi wa urais wa muungano na wabunge haukuwa na tatizo kwa sababu hisia kali za kisiasa zinauhusu uchaguzi wa rais wa Zanzibar na uwakilishi pekee.

Amesema hadhani kama ataendelea kuiongoza tume baada ya muda wake wa utumishi wa mwenyekiti kumalizika ifikapo Aprili mwaka ujao wa 2018. Aliteuliwa Aprili 2013.

“Anayo mamlaka hayo lakini nikiulizwa basi ni vizuri atokee mtu mwingine aongoze,” alisema alipoulizwa kama atamkatalia rais atakapomteua tena.

Uamuzi wa kufuta uchaguzi katika siku ambayo tume ilitarajiwa kukamilisha kumtangaza mshindi wa urais, ulizusha shutuma kali kwa kuwa watazamaji waliupa sifa uchaguzi kuwa huru na wa haki.

Ni hatua iliyoibua upya mgogoro wa kisiasa Zanzibar hasa kwa kuwa vyama kadhaa vikiongozwa na CUF vilikataa kushiriki uchaguzi wa marudio ulioitishwa 20 Machi 2016.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Sabaya afutiwa kesi, ruksa kugombea uongozi

Spread the loveMwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali DPP leo Ijumaa amefuta rufaa...

Habari za Siasa

Serikali yasaka bilioni 3 kujenga daraja Mto Mpiji

Spread the loveSerikali imesema inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kiasi cha...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kwafukuta kisa chaguzi, Lissu aibua tuhuma nzito

Spread the loveCHAGUZI za kusaka viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo...

Habari MchanganyikoTangulizi

Kimbunga “HIDAYA” chaendelea kuimarika, wananchi wapewa tahadhari

Spread the loveMAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa...

error: Content is protected !!