Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Zitto Kabwe asema hatarudi nyuma, mapambano yanaendelea
Habari za Siasa

Zitto Kabwe asema hatarudi nyuma, mapambano yanaendelea

Dorothy Semu, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT wazalendo Bara
Spread the love

KIONGOZI wa chama cha siasa cha upinzani nchini Tanzania, Zitto Kabwe amesema, uamuzi wa kesi uliotolewa dhidi yake hautamrudisha nyuma katika harakati zake za kisiasa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Leo Ijumaa tarehe 29 Mei, 2020, Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Huruma Shaidi, ametoa hukumu katika kesi namba 327/2018 ya uchochezi iliyokuwa inamkabili Zitto.

Hakimu Shahidi katika maamuzi yake, amemkuta Zitto na hatia katika makosa yote matatu na kutoa hukumu ya kumtaka mwanasiasa huyo kutokutenda kosa lolote la uchochezi kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kwa mujibu wa waendesha mashitaka wa serikali, Zitto aliitisha mkutano na waandishi wa habari, tarehe 28 Oktoba 2018, makao makuu ya ACT Wazalendo,  akiwa na lengo la kuleta chuki kwa raia wa Jamhuri, kinyume na sheria.

Mara baada ya hukumu hiyo kutoka, makamu mwenyekiti wa ACT-Wazalendo-Bara, Dorothy Semu akatoa taarifa kwa umma akisema chama hicho kimepokea kwa mshtuko maamuzi ya kutiwa hatiani Zitto.

“Wananchi na wanachama wa ACT Wazalendo, kwa sasa itoshe tu kusema kuwa Chama cha ACT Wazalendo kinapokea na kuyaheshimu maamuzi ya Mahakama ya Hakimu Mkaazi Kisutu yaliyotolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi.”

“Kwa sasa, chama kinasubiri kupokea ushauri wa mawakili wa Zitto Kabwe kuhusu tafsiri ya hukumu hiyo na hatua sahihi za kuchukua,” amesema Dorothy

Makamu huyo mwenyekiti amesema, “muda mfupi uliopita, nimeongea na Kiongozi wetu na amenihakikishia kuwa yupo imara na kamwe hukumu hii haitamrudisha nyuma. Mapambano ya kuondoa mfumo kandamizi na uchumi goigoi lazima yaendelee. Aluta Continua!!”

Amesema, wakati wakiendelea kusubiri tafsiri na ushauri wa wanasheria, “nichukue fursa hii kwa niaba ya chama, kuwataka wanachama wote mtulie katika kipindi hiki huku mkisubiri taarifa mbalimbali zitakazotolewa na chama kupitia viongozi wenu.”

Dororhy ametumia fursa hiyo, kuwapongeza mawakili wote ambao wamefanya kazi kubwa tangu mwanzo hadi mwisho wa kesi hiyo.

Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo

Mawakili hao ni Stephen Mwakibolwa, Bonifasia Mapunda, Peter Kibatala, Jebra Kambole na Jeremia Mtobesya.

Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad na Wakili Fatma Karume wametumia mitandao yao ya kijamii ya Twetter kuizungumzia hasa wakimtaka mwanasiasa huyo kuwa mvumilivu kutokana na ‘kifungo cha kisiasa’ alichokutana nacho.

Katika hukumu hiyo, Hakimu Shahidi ameaimbia mahakama hiyo leo, kuwa “maneno aliyotamka Zitto hayana ukweli, makali na magumu mno.”

Amesema, “maneno yale yalikuwa strong (mazito), kwamba watu 100 kufa sio kitu kidogo. Maneno haya yameshindwa kuthibitishwa hata kwenye utetezi wake mahakamani.”

Zitto alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, tarehe 2 Novemba 2018, ambako alituhumiwa kwa makosa ya uchochezi dhidi ya jeshi la Polisi.

Katika kesi hiyo inadaiwa  tarehe 28 Oktoba 2018, Zitto  aliitisha mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika ofisi za Makao Makuu ya ACT Wazalendo, akiwa na lengo la kuleta chuki kwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinyume na sheria na kwamba alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi.

Zitto anadaiwa alitamka kuwa “watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya Nguruka, Polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua’’

Katika shitaka la pili ilidaiwa, alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi akisema ‘’lakini tumefuatilia kwa kina jambo hili, taarifa ambazo tumezipata kutoka kijijini Mpeta-Nguruka, Uvinza ni mbaya.

“Taarifa ambazo zinaonyesha wananchi wengi sana wameuawa na jeshi la Polisi pamoja na kwamba afande Sirro amekwenda kule, haijatoa taarifa yoyote kuhusu wananchi…kama hawa wanyantuzu walivamia eneo la Ranchi kuna taratibu za kiheria za kuchukua na sio kuwauwa, wananchi wengi sana wamekufa.’’

Ilidaiwa katika tarehe hiyo hiyo, Zitto alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi akisema “tumekuwa tukifuatilia kwa kia yanayojiri yote huko Uvinza tunasikitika kusema kuwa taarifa tunazozipata kutoka Uvinza zinaogofya mno, kwani tunaambiwa kuwa wananchi zaidi ya 100 wa kabila la Wanyantuzu wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi na polisi, wengine wakisema kuuawa hata wakiwa kwenye matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa kwenye purukushani na jeshi la polisi…’’

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!