June 22, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wizara ya Ujenzi kinara utawala wa Rais Magufuli  

Barabara ya kiwango cha rami

Spread the love

WIZARA ya Ujenzi, Uchukuzi na Mwasiliano, imeongoza kwa kupatiwa fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2019/2020. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Wizara hiyo imekuwa kinara kwa kupatiwa fedha nyingi za miradi ya maendeleo, kwenye kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli aliyeingia madarakani tarehe 5 Novemba 2015.

Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kuanzia mwaka 2016/17 hadi 2019/2020, iliyotolewa leo Alhamisi tarehe 11 Juni 2020, bungeni na jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango imeonyesha wizara hiyo ilipewa zaidi ya  Sh.10 trilioni katika kipindi hicho.

Fedha hizo (zaidi ya Sh. 10 trilioni), ni kati ya Sh. 37.8 trilioni zilizotolewa kwa ajili ya kugharamia utekelezwaji wa miradi ya maendeleo katika mwaka 2016/2017 hadi 2019/20, kwenye wizara zote nchini.

Ambapo Idara ya Uchukuzi ilipewa Sh.6.1 trilioni, Ujenzi  Sh. 4.57 trilioni na mawasiliano  Sh. 80.47 biloni.

Kati ya fedha hizo, Serikali ya Tanzania ilitoa zaidi ya Sh. 7 trilioni kati ya hizo Sh. 5.62 trilioni za Uchukuzi,  Sh. 2.84 trilioni za Ujenzi na Sh. 6.26 bilioni zilikwenda Mawasiliano huku zaidi ya Sh. 2 trilioni ya fedha hizo zikitolewa na wafadhili.

Wizara ya Ofisi ya Rais, Ikulu, ilifuata kwa kupatiwa fedha nyingi, ambapo ilipewa Sh. 4.57 trilioni  kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kati ya fedha hizo, Serikali ya Tanzania ilitoa Sh. 4.7 bilioni huku fedha za nje zikiwa ni Sh. 4.5 trilioni.

Dk. Phillip Mpango, Waziri wa Fedha na Mpango

Wizara ya Nishati imekuwa ya tatu kwa kupatiwa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, katika kipindi hicho, ambapo ilipatiwa Sh. 4 trilioni huku fedha za ndani zikiwa ni Sh. 3.1 trilioni wakati za nje zikiwa ni Sh. 863.8  bilioni.

Katika kipindi cha mwaka 2016/2017 hadi 2019/2020, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto imekuwa wizara ya nne kwa kupewa fedha nyingi, Sh. 3.65 trilioni.

Katika fedha hizo zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye wizara hiyo, Sh. 1.47 ni fedha za ndani na, Sh. 2.17 trilioni  zikiwa ni fedha za nje.

Ofisi ya Rais –TAMISEMI ilifuata kwa kupewa Sh. 2.8 trilioni  ikifuatiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliyopewa Sh. 2.4 trilioni.

Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ilipewa Sh. 840.3 bilioni, Wizara ya Maji ilipewa Sh. 714.9 bilioni.

Wizara ya Kilimo ilipewa Sh.96 bilioni huku Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikipatiwa Sh. 8.1 bilioni (Idara ya Uvuvi ilipewa Sh.5.9 bilioni na Mifugo Sh. 2.26 bilioni).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Sh. 37.8 trilioni zimetumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo.  Sh. 24.6 trilioni sawa na asilimia 65.14 ni fedha za ndani na Sh. 13.1 trilioni sawa na asilimia 34.86 ni fedha za nje.

error: Content is protected !!