Lazaro Mambosasa, Kamanda wa Polisi Dar es Salaam

Wabunge walioko Dar watakiwa kujisalimisha Polisi

Spread the love

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam nchini Tanzania, limewataka wabunge waliokaidi agizo la kurejea bungeni jijini Dodoma ndani ya masaa 24, kujisalimisha Ofisi ya Upelelezi ya kanda hiyo, kwa ajili ya mahojiano. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Jana Jumatano tarehe 6 Mei 2020, Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, aliwataka wabunge wasiokuwa na vibali vya udhuru kutoka kwa Spika Job Ndugai, kurejea bungeni kwa ajili ya kuhudhuria vikao vya bunge vinavyoendelea.

Leo tarehe 7 Mei 2020, SACP Lazaro Mambosasa, Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, amewataka wabunge hao kwa hiari yao kuripoti Ofisi ya Upelelezi ya kanda hiyo mara moja.

Taarifa ya agizo hilo la Kamanda Mambosasa, limetolewa kwa niaba yake na kamanda Ronarl K. Makona.

“Kufuatia agizo la Mkuu wa Mkoa na Mwenyekiti Wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda la tarehe 6 Mei 2020, kwa waheshimiwa wabunge ambao wapo mkoani hapa badala ya kuwa bungeni Dodoma, kurudi ndani ya saa 24,” inaeleza taarifa ya Kamanda Makona kwa niaba ya Mambosasa.

Taarifa hiyo imeongeza, “Kwa wale ambao bado wapo jijini Dar es Salaam wanatakiwa kuripoti kwa hiari yao Ofisi ya Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa mahojiano.”

Agizo la Makonda alilitoa kipindi ambacho baadhi ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wanaendelea kutekeleza maagizo ya chama hicho yaliyotolewa na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema tarehe 1 Mei 2020 la kuwataka kutohudhuria shughuli za bunge na wabaji majumbani mwao kwa siku 14 kujikinga na maambukizi ya corona.

Hatua hiyo ilitokana na vifo vya wabunge watatu vilivyotokea ndani ya wiki mbili akiwamo waziri wa katiba na sheria, Balozi Augustine Mahine. Wengine waliofariki ni Getrude Rwakatare, mbunge wa viti maalum pamoja na Richard Ndassa mbunge wa Sumve.

Mbowe aliwataka wabunge hao wakae karantini, hadi pale janga hilo litakapopatiwa ufumbuzi wa namna ya kudhibitiwa.

Pia, Mbowe alilitaka bunge lisitishe shughuli zake, kisha kuwapima wabunge wote na watumishi wa mhimili huo, ili kujua hali ya maambukizi ya ugonjwa huo, pamoja na kupata ufumbuzi wa kudhibiti ueneaji wake.

Lakini hatua hiyo ilipingwa na Makonda kwa madai kwamba, wabunge hao hawawatendei haki wawakilishi wao kwa kutohudhuria bungeni, huku akiwafananisha na wazurulaji.

Makonda alisema wabunge hao wasiporudi bungeni ndani ya saa 24, watakamatwa kwa kosa la uzururaji.

“Hakuna asiyefahamu kuwa sasa hivi tuko katika mapambano dhidi ya virusi vya Corona na sio uzururaji, ifahamike huu sio mji wa wazururaji hivyo natoa saa 24 kwa wabunge wote kurudi Dodoma tofauti na hapo tutawakamata kwa kosa la uzururaji kama tunavyowakamata machangudoa,” amesema Makonda.

Tangu kutolewa kwa agizo hilo la Makonda, baadhi ya wabunge akiwamo Zitto Kabwe wa Kigoma Mjini kupitia ACT-Wazalendo walilipingwa na kudai katiba ya Tanzania inawaruhusu kuwa eneo lolote lile bila kubughudhiwa.

About Regina Mkonde

Leave a Reply

Your email address will not be published.

error: Content is protected !!