October 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jinsi Chadema ilivyopoteza Mameya Dar

Spread the love

UCHAGUZI Mkuu nchini Tanzania uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015, ulishuhudia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kikipewa ridhaa na wananchi wa Jiji la Dar es Salaam, kuongoza Manispaa tatu za Jiji hilo. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea)

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, upinzani kupata mafanikio makubwa kama hayo, tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi humo, Julai 1992.

Manispaa hizo, ni Ilala, Kinondoni na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam- jiji kubwa la kibiashara nchini Tanzania.

Hata hivyo, baadaye Manispaa ya Kinondoni iligawanywa na kutoa Manispaa mbili za Kinondoni na Ubungo.

Katika magawanyo huo, Chadema ilifanyiwa hila na kushindwa kuongoza halmashauri zote mbili – Ubungo na Kinondoni. Iliishia kuongoza Ubungo huko Kinondoni ikiongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Meya wa Manispaa ya Ubungo, alikuwa Boniface Jacob; Manispaa ya Ilala ikaongozwa na Charles Kuyeko na Isaya Mwita Charles akiongoza Jiji la Dar es Salaam.

Hata hivyo, mpaka leo Ijumaa ya tarehe 8 Mei 2020, Chadema ambacho ni chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, kimepoteza uongozi kwenye manispaa hizo kwa nyakati tofauti.

Jumamosi ya tarehe 23 Machi 2019, chama hiki kilianza kupoteza uongozi wa Umeya baada ya Kuyeko kutangaza kujiuzulu wadhifa wake na kujiunga na CCM.

Charles Kuyeko, aliyekuwa Meya wa Ilala

Kuyeko ambaye alikuwa Diwani wa Bonyokwa alisema, haoni sababu za yeye kuendelea kubaki upinzani wakati Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli inafanya vyema, na hiyo ilikuwa chachu ya kutimkia huko.

Uchaguzi ulipofanyika kujaza nafasi hiyo, CCM ilishinda uongozi kwa Omari Kumbilamoto kuibuka mshindi.

Tarehe 9 Januari 2020, Chadema kilijikuta kikipoteza tena uongozi wa Jiji la Dar es Salaam baada ya Meya wake, Isaya Mwita ‘kung’olewa’ katika mazingira yenye utata.

Utata huo, ulitokana na idadi wa wajumbe waliotumika kumng’oa kutoendana na matakwa ya kanuni na sheria za Halmashauri hali iliyomfanya Mwita kupinga.

Hata hivyo, Mwita ambaye ni Diwani wa Vijibweni licha ya kufungua kesi mahakamani kupinga uamuzi huo, hakufanikiwa na mpaka sasa Jiji hilo ninakaimiwa Abdallah Mtinika ambaye alikuwa Naibu Meya.

Mwita ‘aling’olewa’ baada ya kutuhumiwa kutoidhinisha matumizi ya Sh. 5.8 bilioni zilizotokana na mauzo ya hisa za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA). Lakini ukweli ni kwamba tuhuma karibu zote zilikuwa hazina mashiko.

Boniface Jacob, aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo

Kuondolewa kwa Mwita na kujuzulu kwa Kuyeko kuliifanya Chadema kubaki na meya mmona Jacob wa Ubungo ambaye naye zama zake zilihitishwa tarehe 2 Mei 2020, baada ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, Beatrice Dominic, kuridhia barua ya viongozi wa Kata ya Ubungo, waliyoeleza kuwa Jacob siyo mwanachama wa chama hicho.

Beatrice alifikia maamuzi hayo, baada ya kupokea barua kutoka Kata ya Ubungo, iliyoandikwa tarehe 28 Aprili na kufikishwa kwake.

Baada ya kuitambua barua hiyo na kwa kuzingatia sheria za Nchi, tarehe 6 Mei 2020, Beatrice alimuandikia barua Naibu Meya ambaye pia Diwani wa Manzese kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Ramadhan Kwangaya, kukaimu nafasi hiyo.

Taarifa zinasema, baadhi ya viongozi wa Chadema ngazi ya Kata na Taifa wamepinga uamuzi huo wakidai Jacob hajavuliwa uanachama na hakuna kikao chochote kilichokaa kumjadili.

Hatua hiyo imehitimisha uongozi wa Chadema katika manispaa tatu kwenye jiji maarufu nchini ambalo ni kitovu cha mapato ya Serikali.

error: Content is protected !!