January 15, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wabunge ACT-Wazalendo waapishwa, Spika Ndugai asema…

Spika Job Ndugai

Spread the love

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amewaapisha wabunge wanne wa chama cha ACT-Wazalendo huku akisema, akidi ya muhimili huo, imekamilika na unaweza kufanya uamuzi wowote. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Wabunge hao wameapishwa leo Jumanne tarehe 15 Desemba 2020 viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

Walioapishwa ni; Khatibu Said Haji (Konde), Salum Mhamed Shafi (Chonga), Omar Ali Omar (Wete) na Khalifa Mhamed Issa wa Mtambwe.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Haji amemshukuru Spika Ndugai kwa kuwaapisha akisema “tumechelewa kuja kula kiapo cha uaminifu kuanza kuwatumikia wananchi, hatukuwa tunakwepa wajibu wetu” bali walisubili uamuzi wa chama hicho juu ya ushiriki wao kwenye.

Haji amesema, uwepo wao una “baraka za Mungu, baraka ya chama chetu na wananchi na msiwe na shaka na ubunge wetu.”

Amesema, baada ya matokeo ya uchaguzi, Zanizbar “tuko kwenye Serikali na tuwapongeze Rais Hussein Mwinyi na Maalim Seif Sharif Hamad, kwa kutuongoza,”

Haji amesema “wakosoaji wetu wanasema mengi, uamuzi uliochukuliwa na viongozi wetu wale wanaokebehi na kudharau mapatano yale, muda utawajibu.”

Amesema, “tumezoea kila uchaguzi Zanzibar hutuacha na makovu kila uchaguzi sasa Rais Mwinyi na Makamu wake kila Ijumaa wanakwenda misikiti mbalimbali kuhubiri amani.”

Akimalizia kuzungumza, Haji ambaye anarejea bungeni kwa mara nyingine amesema, “sisi tutabaki hapa hapa Tanzania, hatutakwenda Ujerumani au Canada kulalamikia mambo ya Tanzania.”

Kwa upande wake, Spika Ndugai amesema hadi sasa bado wabunge kumi ambao hawajaapishwa.

“Rais John Magufuli wakati anaapishwa (5 Novemba 2020) alisema uchaguzi umeisha na sasa tunasonga mbele na kinachoendelea hapa ni kukamilisha Bunge. Katika wingi wake, idadi ya wabunge wote ni 393 mpaka sasa nadhani bado 10. Hivyo, tayari tunayo akidi ya kutosha kuendesha Bunge na kufanya maamuzi yoyote ya kibunge,” amesema Spika Ndugai.

“Niwapongeze sana waheshimiwa wabunge wanne ambao wamekula kipao kukamilisha adhma yao kuwawakilisha wananchi, hawa ni wabunge wa kuchaguliwa kutoka majimbo kule Pemba na majina yao tumeyapata kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, wamechelewa lakini hakuna kanuni walizovunja,” amesema Spika Ndugai.

Spika Ndugai ameahidi kuwalinda wabunge hao wa upinzani licha ya kuwa wachache huku akiwahakikishia kwamba atasikiliza na kuheshimu hoja zao licha ya uchache wao bungeni.

“Niwahakikishie kwamba, uongozi wa Bunge tutalinda haki zenu. Ni wajibu wa Spika kuhakikisha wabunge wachache wana haki ya kusikilizwa, lakini kama hoja ni nzito walio wengi wataamua na walio wachache wana haki ya kusikilizwa,” amesema Spika Ndigai.

Aidha, Spika Ndugai amewaomba wabunge wote walioapishwa katika nyakati tofauti, wafike bungeni pindi watakapopata taarifa za kuanza kwa vikao vya mhimili huo.

“Niwahakikishie bunge letu liko imara kuwatumikia. Kwa tarehe ya Katibu wa Bunge ataitangaza katikati ya Januari tutawahitaji waje kufanya kazi. Wabaunge wote walioapishwa ni wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wakati wa kufika wafike waendelee kutekeleza majukumu yao ya uwakilishi wa Watanzania, kusimamia Serikali na masuala mengine,” amesema Spika Ndugai.

Naye Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhahagama amesema, kukamilika kwa akidi ya Bunge hilo kunafanya mhimili huo kuwa imara katika ujenzi wa Taifa.

“Nikupongeze Spika kwa kuwa bunge ni chombo muhimu sana, tunayo mihili mitatu. Ikisimama vizuri ndio ukomavu wa Taifa. Spika umedhihiridhia nia na dhamira kuhakikisha Bunge linatekeleza wajibu wake ipasavyo,” amesema Mhagama.

Mhagama amewaomba wabunge walioapa leo kutimiza majukumu yao ipasavyo katika kuwawakilisha wapiga kura wao.

“Kwa wenzetu wabunge ambao wamekula kiapo leo, wamesema wamebeba maono na muelekeo wa uwakilishi halisi. Wanatazamiwa na wapiga kura wao na Watanzania wote kutekeleza majukumu yao sawasawa,” amesema Mhagama.

error: Content is protected !!