Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Serikali inaua uchumi – Mbowe
Habari za SiasaTangulizi

Serikali inaua uchumi – Mbowe

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema
Spread the love

SERIKALI imeshauriwa kuja na “mpango mkakati” wa namna itakavyorekebisha uchumi wa taifa ambao kwa maneno ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), “unaporomoka kwa kasi,” anaandika Hamisi Mguta.

“Ukichukua mapato ya kila mwezi ya serikali. Uchukue na vipaumbele vya matumizi ya serikali kibajeti, unaona wazi serikali imezidiwa na matumizi na haiwezi kutekeleza bajeti yake kwa ufanisi. Hii inaashiria hatari kiuchumi,” amesema Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema, akizungumza na waandishi wa habari aliokutana nao leo.

Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, alikutana na waandishi wa habari kwenye Hoteli ya Protea Courtyard, jijini Dar es Salaam, kueleza maazimio ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichofanyika tarehe 29-30.

Kusikia zaidi alichosema unaweza kutazama VIDEO hii hapa chini,…. 

Mbele ya baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, akiwemo Edward Lowassa, aliyegombea urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015, Mbowe, akitumia takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), alisema mapato ya mwezi katika kipindi cha serikali mpya kufikia Mei 2017, yalifikia Sh. 1.2 trilioni.

Hata hivyo, katika mapato hayo, serikali inatumia kwa wastani Sh. 570 bilioni kulipa mishahara na Sh. 650 bilioni kwa ajili ya kulipia deni la taifa la nje, kila mwezi.

Kwa mwenendo huo, Mbowe anasema serikali inashindwa kutoa fedha za kutekeleza shughuli za maendeleo. Hakuna fedha hizo na ndio maana, anasema, “utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2016/17, ulikuwa wa kati ya asilimia zero na asilimia 34.”

Maana ya takwimu hizo ni kwamba yapo maeneo ya kisekta hayakupatiwa fedha hata chembe kwa mwaka mzima wa kibajeti huku serikali ikiishia na kutoa asilimia isiyozidi 34 ya fedha za bajeti kwa baadhi ya maeneo mengine.

Mbowe amesema serikali inapaswa kujiendesha katika namna ambayo inatumia zaidi kwa maeneo yanayochagiza uzalishaji na sio mwenendo wa sasa wa kutumia fedha nyingi kwa maeneo yasiyotoa tija kwa uchumi.

Amesema uendeshaji wa uchumi usiozingatia sekta zinazogusa zaidi wananchi walio wengi, kama vile kilimo kinachoshikirisha zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania, hauwezi kuisaidia nchi kwa sasa. “Fedha nyingi zinatumika kwa maeneo yasiyoleta tija kwa sekta za kiuchumi. Kununua ndege za Bombadier ni jambo zuri, lakini ni watu wangapi wananufaika na ununuaji huo nchini petu,” alihoji.

Amesema katika bajeti mbadala ya kambi ya upinzani ambayo “kwa makusudi ilitengenezewa mazingira isisikike kwa wananchi kwa kuwa siku ambayo ilipangwa kusomwa bungeni kuliandaliwa uwasilishaji wa ripoti ya pili ya makinikia Ikulu, tulisema matumizi ya serikali ni lazima yaelekezwe zaidi katita elimu, kilimo na viwanda.”

“Watanzania hali tunayoiona sasa ni maumivu yanayotokana na kuwa na serikali yenye viongozi wasiokuwa na upeo wa kuendesha uchumi kitaalamu. Sisi tunaviona viashiria vinavyoelezea kuwa uchumi unaporomoka kwa kasi na lazima tupate ufumbuzi si hivyo subirini itakapofika Desemba muone matokeo zaidi ya kuuendesha uchumi kwa sera za ovyo,” amesema.

Shida kubwa inayowakabili wananchi kwa sasa ni ongezeko kubwa la bei za vyakula; kasoro ambayo Mbowe alisema inasababishwa na serikali kutozingatia utaratibu wa kununua chakula cha akina ambacho hutumika kupunguza mfumuko wa bei.

Tatizo jingine ni kutokuwepo kwa urari wa kibiashara nchini kati ya uagiziaji na uuzaji wa bidhaa. Biashara ya dhahabu imetetereka kutokana na maamuzi ya serikali yasiyotokana na utafiti wa kitaalamu.

Amesema uagiziaji bidhaa, akitaja kwa mfano pembejeo za kilimo na magari ya mizigo, umeshuka, hali inayochangiwa na kupungua kwa hamu ya wafanyabiashara kukopa kwenye mabenki ya biashara.

“Mikopo kwa ajili ya sekta ya kilimo tulizoea ikifikia asilimia 6 ya mikopo yote nchini. Leo tunaona imeshuka kufikia chini ya -9 huku biashara nayo ikishuka katika kukopewa. Hizi si taarifa nzuri kwa uchumi unaokua. Ni hatari,” alisema.

Mbowe amesema ni miujiza kuitoa nchi kwenye umaskini kwa kuwa inazidi kuzidiwa na deni la taifa. Mwaka wa pili wa utawala mpya wa Rais Dk. John Magufuli deni limefikia Dola 17.907 milioni Mei 2017 kutoka Dola 14,762.7 milioni mwaka 2015.

Deni la ndani ambalo Mbowe amesema serikali inadharau kulipa, limefikia Dola 11.353 bilioni kutoka Dola 7.707 bilioni mwaka 2015. Ni ongezeko la zaidi ya Dola 3,645.7 bilioni.

Pia alizungumzia hatua ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuiandikia kampuni ya uchimbaji madini ya ACACIA hati ya madai ya kodi yanayofikia Sh. 425 trilioni akisema kiasi hicho cha madai ya kodi hakifikiriki kitaalamu na kinatafsiriwa na vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa kuwa kinaonesha namna Tanzania isivyo na uongozi unaojua mambo.

Hatua hiyo imetekelezwa kama maelekezo ya serikali kwa TRA baada ya kuwasilishwa kwa taarifa za Tume mbili za rais zilizoangalia athari za kiuchumi za usafirishaji nje wa mchanga wenye madini kutoka migodi ya dhahabu inayoendeshwa na Acacia, yenye makao makuu nchini Canada.

Akijibu swali la sababu ya kambi ya upinzani kuikataa bajeti ya serikali iliyowasilishwa bungeni mwezi uliopita, Mbowe alisema “sisi sio watu wa kukubali kila kitu hata kama hatukiamini. Tulisema bajeti ni mbovu na isiyotekelezeka. IMF wamethibitisha katika ripoti yao kuwa bajeti ya Tanzania haitekelezeki.

Tulitoa bajeti mbadala lakini serikali haitaki kushauriwa, nasi hatukubali tusichokiamini.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!