Friday , 29 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Takukuru yadaka watendaji 12 Mbeya
Habari Mchanganyiko

Takukuru yadaka watendaji 12 Mbeya

Jiji la Mbeya
Spread the love

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwakamata mara moja, kuwahoji na kuwafikisha mahakamani watendaji wakuu 12 wa Halshauri ya jiji la Mbeya, kwa kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. bilioni 63.4, anaandika Mwandishi Wetu.

Watendaji hao ni waliokuwa wakurugenzi watatu, Kaimu Mkurugenzi mmoja, aliyekuwa Meya wa Manispaa hiyo, Mhasibu na msaidizi wake.

Wengine ni waliokuwa wajumbe wa bodi ambao walioidhinisha fedha hizo bila kufuata taratibu ambazo zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa soko la Mwanjelwa katika halmashauri hiyo.

Majaliwa alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri za Mbeya mjini na vijijini, katika ziara yake ya siku nne mkoani humo na kumuagiza Mkurugenzi wa Takukuru Mkoa huo, Emanuel Kiabo, kuhakikisha anawasaka watu hao na kuwatia mbaroni.

Alisema taarifa ya ubadhilifu huo wa fedha ni kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ripoti ya mwaka 2015/16.

“Haiwezekani watu hawa waisababishie serikali hasara ya fedha nyingi kiasi hiki na wakaachwa, kama wapo humu ndani na waliostaafu wote au kuhamishwa, naagiza wasakwe popote walipo, wakamatwe mara moja, wahojiwe na wafikishwe mahakamani,” alisema Majaliwa.

Aliwataja watumishi hao kuwa ni waliokuwa wakurugenzi, Mussa Zungiza (Mstaafu) Elizabeth Munuo, Juma Idd (aliyehamishiwa halmashauri ya jiji la Arusha), Kaimu Mkurugenzi, Dk. Samwel Lazaro ambaye kwa sasa ni Mganga Mkuu wa mkoa wa Songwe, aliyekuwa Meya wa Jiji hilo Athanas Kapunga (Mstaafu) aliyekuwa Mhasibu James George (Mstaafu) na Msaidizi wake Tumaini Msigwa (amehamishwa).

Wengine ni aliyekuwa Msimamizi wa Miradi, Henry Maganga ambaye yupo kazini na waliokuwa wajumbe wa bodi ambao waliidhinisha fedha hizo, Mussa Mapunda, Davis Mbembela, Lidya Abas na Samuel Bubegwa.

Majaliwa alisema watumishi hao ambao waliidhinisha fedha hizo, walikopa sh. bilioni 13 kutoka Benki ya CRDB bila kupata dhamana kutoka Ofisi ya Hazina na kutolipa deni hilo kwa wakati na kusababisha riba kuwa kubwa hadi kufikia zaidi ya Sh. bilioni 63.4.

Alisema kutokana na kudaiwa kiasi hicho cha fedha, halmashauri iliamua kupandisha gharama za pango la soko hilo kwa ajili ya kupata fedha za kulipa hali ambayo imewalazimu wafanyabishara kulikimbia jengo hilo.

Alisema pia Mkandarasi alifanyakazi hadi asilimia 80 ya kukamilisha jengo hilo na kulipwa Sh. bilioni 8.7 na alipomalizia asilimia 20 ya kazi iliyobaki alilipwa tena Sh. bilioni 7.1.

Alisema pia watendaji hao, waliongeza gharama za mradi zilizoidhinishwa kutoka bilioni 13 hadi kufikia bilioni 19 bila maelezo.

Majaliwa alisema taarifa ya CAG imebaini kuwa Benki ya CRDB haijalipwa deni lake kwa kipindi kirefu na kusababisha kuidai halmashauri Sh. bilioni 63.4.

“Kwa sababu ya uzembe na matumizi mabaya ya fedha za umma, halmashauri inadaiwa kiasi hiki cha fedha ambacho haijulikani kitalipwaje. CRDB wakiamua kudai fedha zao hapa, mali zote za halmashauri zitapigwa mnada kuanzia majengo ya ofisi, magari yote hadi ya taka, hakuna kitakachosalia, hawa watu lazima wakamatwe,” alisema.

Mara baada ya Waziri Mkuu, kumkabidhi Mkurugenzi wa Takukuru majini hayo na kuondoka katika ukumbi huo wa mkutano, alianza kuwakamata watendaji waliotajwa ambao walihudhuria mkutano huo.

“Wote mliotajwa hapa, kuja mbele, njoo kwa hiari yako hapa mbele… Kama upo hapa ndani na usipokuja hapa mbele kwa hiari yako tutakufuata popote ulipo na vyombo vya dola, hivyo njoo mwenyewe hapa mbele,” alisikika Mkurugenzi huyo.

Hadi msafara wa Waziri Mkuu ukiondoka katika ukumbi huo, watendaji watatu kati ya 12 waliotajwa katika tuhuma hizo, walikuwa wameshajitokeza mbele kwa ajili ya kuanza taratibu za kuhojiwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Puma Energy Tz: Watanzania tudumishe amani kuvutia uwekezaji

Spread the loveKAMPUNI ya Mafuta ya Puma Tanzania imewakutanisha wadau mbalimbali katika...

Habari Mchanganyiko

DAWASA waanza utekelezaji agizo la Samia

Spread the loveMamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam...

Habari MchanganyikoKimataifa

Zuma akataliwa kugombea urais

Spread the loveTUME Huru ya Uchaguzi Afrika Kusini (IEC) imemwondoa rais wa...

Habari Mchanganyiko

Mtandao watetezi wa haki za mazingira Tanzania waundwa

Spread the loveMTANDAO wa watetezi wa haki za mazingira nchini Tanzania, umeundwa...

error: Content is protected !!