December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais mstaafu Benjamini Mkapa afariki dunia

Rais Mstaafu Benjamin Mkapa

Spread the love

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli ametangaza kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa kilichotokea usiku wa kuamkia leo Ijumaa tarehe 24 Julai, 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Rais Magufuli amesema, Benjamin William Mkapa amefariki dunia hospitalini Jijini Dar es Salaam alikokiwa akipatiwa matibabu.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa imesema, Rais Magufuli amewataka Watanzania wote kuwa watulivu na wastahimilivu baada ya kupokea taarifa za kuondokewa na mpendwa wao Benjamin William Mkapa.

“Kwa masikitiko makubwa tumepata msiba mkubwa, Mzee wetu Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu amefariki dunia katika hospitali Jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa.”

“Niwaombe Watanzania tulipokee hili, tumepata msiba mkubwa na tuendelee kumuombea Mzee wetu Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa ambaye ametangulia mbele za haki,” amesema Rais Magufuli

“Taarifa zingine zitaendelea kutolewa lakini Mzee Mkapa hatuanaye tena” amesema Rais Magufuli katika taarifa yake kwa Taifa.

Benjamini Mkapa, alikuwa Rais wa Tanzania kati ya mwaka 1995 hadi 2005 akipokea uongozi kutoka kwa Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi.

Baada ya miaka yake 10 Ikulu akiwa na kauli mbiu ya Ukweli na Uwazi, Mkapa alikabidhi uongozi wa Jakaya Mrisho Kikwete.

Mkapa ameandika kitabu kiitwacho “My Life, My Purpose” (Maisha Yangu, Kusudio Langu) akizungumzia safari yake ya maisha akiwa mdogo, hadi kuingia madarakani na kustaafu kwake.

Kitabu hicho, kilizinduliwa tarehe 12 Novemba 2019 na Rais Magufuli.

Endelea kufuatilia MwanaHalisi Online na MwanaHalisi TV kwa taarifa zaidi.

error: Content is protected !!