Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mbwembwe za Bombardier zayeyuka
Habari za Siasa

Mbwembwe za Bombardier zayeyuka

Spread the love

AHADI ya Rais John Magufuli ya kununua na kuleta ndege moja aina ya Bombardier ifikapo Julai mwaka huu, imeyeyuka. Ndege haijafika Tanzania. Na sasa rais hazungumzii suala hili tena, anaandika Faki Sosi.

Mwaka jana, akipokea ndege mbili mpya zilizotua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli aliahidi kuja kwa ndege nyingine nne katika dhamira yake ya kusaidia kukuza uchumi kupitia sekta ya utalii. Alisema Bombadier ingekuja Julai mwaka huu.

Lakini hajasikika tena akielezea ahadi yake hiyo huku ndege ikiwa haijaonekana. Kutofika kwa ndege Bombadier Q400 kunakuja wakati taarifa zikiwa zimesambaa nchini kuwa ndege iliyokusudiwa kuja imekamatwa nchini Canada.

Kwa mujibu wa taarifa hizo zilizoanzia kwa Zitto Kabwe, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), na kukolezwa na Tundu Lissu, mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), ndege hiyo inashikiliwa kwa sababu ya deni ambalo kampuni ya ujenzi ya Canada inaidai Tanzania.

Taarifa za Bombadier Q400 ya Tanzania, zikasema ndege hiyo inashikiliwa na kampuni ya Stirling Civil Engineering Ltd (SCEL) ambayo imeshinda kesi ya kuvunjwa mkataba wa ujenzi wa barabara ya Wazo Hill-Bagamoyo na hivyo kupewa amri ya kukamata mali za serikali ya Tanzania.

Zitto ambaye ni Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, alianza kuchokonoa suala la kutofika kwa ndege hiyo alipomuuliza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Teknolojia, Prof. Makame Mbarawa kwa njia ya mtandao, sababu ya kuchelewa kufika kwa ndege hiyo.

Prof. Mbarawa alijibu mtandaoni, “Ni kweli kabisa ahadi ilikuwa Julai, kuna taratibu za mwisho zinafanywa kabla ya kuwasili hivyo itawasili tu.”

Hoja ya Zitto katika mawasiliano yake hayo ya tarehe 17 Agosti, ilikuwa kwamba sio kwamba uchelewaji huo umesababishwa na ndege hiyo kukamatwa na watu wanaoidai Serikali? Hakupata zaidi ya hayo ya Prof. Mbarawa.

Lakini Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS), alitoa siri yote ya suala hilo siku iliyofuata.

Mbele ya waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, alisema wakamataji walielekezwa na kampuni ya Stirling ya jijini Montreal, Canada, ambayo inaidai serikali ya Tanzania kutokana na kesi ya kuvunjwa kwa mkataba wa ujenzi wa barabara.

Lissu alisema kampuni hiyo inaidai Tanzania Dola 38.7 milioni za Marekani, sawa na Sh. 87 bilioni za Tanzania. Ndege ilikamatwa kama sehemu ya mali zilizoorodheshwa katika amri ya Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara ya London (CSIS). Orodha ilihusu mali zilizoko Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ubelgiji, Uganda na Canada.

Serikali ilijibu taarifa hizo haraka kupitia ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali. Ilikiri ndege kuzuiwa na kwamba kuna kesi mahakamani. Lakini ikasema suala hilo linashughulikiwa kwa mazungumzo ya kidiplomasia ambayo yakimalizika, “ndege itakuja tu.”

Bali serikali pia ililaumu iliyoita “watu wanaoeneza taarifa” dhidi ya jitihada za serikali katika kuwaletea maendeleo Watanzania. Iliwaita wasaliti wa taifa waliosimama upande wa wanaohujumu taifa kiuchumi.

Mazungumzo yenyewe yalihusu deni la dola 38,711,479 inazodaiwa Serikali kutokana na hukumu mbili za Mahakama ya Usuluhishi zilizotolewa mwaka 2009 na 2010.

Jana, akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 33 wa Tawala za Mikoa Tanzania (ALAT), uliofanyika jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema kuwa serikali imenunua ndege mpya sita, mbili zikiwa zimeshawasili nchini; na zinafanya kazi.

“Tunaendelea kununua ndege nyingi mpaka shirika liimarike na Tanzania ipate maendeleo,” alisema.

https://twitter.com/TZ_MsemajiMkuu/status/915134351922343937

Rais Magufuli hakueleza ndege nne zitawasili lini. Wala katika hutuba yake hiyo, hakueleza mkasa wa ndege mojawapo inayoshikiliwa nchini Canada.

Kesi hiyo iliyofunguliwa tarehe 10 Desemba 2009, ilitokea baada ya serikali ya awamu ya tatu, wakati huo waziri wa ujenzi akiwa Magufuli, aliyekuwa pia mbunge wa Biharamulo, mkoani Kagera, kuvunja mkataba huo kinyume na taratibu za kimkataba.

Serikali ilimnyang’anya kazi mkandarasi huyo na kumtimua wakati akijitahidi kupata maelewano ili akamilishe kazi aliyopewa kwa mujibu wa sheria.

Ilikuwa tarehe 10 Juni 2010, mahakama ya usuluhishi ilipotoa hukumu. Ikaipa SCEL tuzo ya takriban Dola 25 milioni, na riba ya asilimia nane inayoishi mpaka deni litakapolipwa.

Tuzo hiyo imesajiliwa na kutambuliwa kama deni halali la Serikali ya Tanzania kwa kampuni hiyo; na utekelezwaji wa hukumu ukalazimu kwenda na orodha ya mali za Serikali ya Tanzania.

Kwa sababu ya serikali kutolipa kwa wakati na kwa mujibu wa makubaliano iloiyoyafikia, deni liliongezeka kufikia Dola 38,711,479 kwenye tarehe 30 Juni 2017.

Hapo ndipo SCEL ilipoomba amri ya Mahakama Kuu ya Montreal ya kukamata mali zote za Tanzania zilizopo kwa kampuni inayotengeneza ndege aina ya Bombardier, zikijumuisha ndege ya Bombardier Q400 iliyonunuliwa na Serikali ya Tanzania mwaka jana.

Wakati serikali ikishughulikia suala hilo, mazungumzo yakiwa yamesimamiwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga, kulikuwa na jitihada za makusudi za kuficha taarifa kujulikana na umma.

Kampuni ya Stirling imekubali kuiachia ndege hiyo kwa malipo ya mwanzo ya Dola 12.5 milioni na baadaye ilituma ujumbe wake nchini kwa ajili ya kufanya makubaliano ya mwisho ya kukamilishiwa malipo ya deni.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!