March 5, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Sakata la Madiwani Arusha; Takukuru, Maadili kazi kwenu

Spread the love

MBUNGE wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari, sasa aweza kuwa “amefunga rasmi” mgodi wa ununuzi wa madiwani wa upinzani uliobuniwa na viongozi wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), anaandika Saed Kubenea.

Ni Jumapili iliyopita, katika ukumbi wa mikutano wa Safari Hoteli jijini Arusha, Nassari aliwaambia waandishi wa habari wa ndani na kimataifa, kuwa baadhi ya viongozi wa umma wanatumia rasimali za nchi kununua madiwani.

Alisema, “hatuna shida na mtu kuhama chama. Tuna shida na visingizio vinavyotolewa na wanaohama. Kwamba kuhama kwao kunalenga kumuunga mkono Rais John Magufuli, wakati ukweli ni kuwa wamenunuliwa kwa fedha za umma.”

Alisema, “tumekusanya ushahidi mwingi unaohusu jambo hili. Mwingine hatuwezi kuuonesha kwa vyombo vya habari kwa kuwa ni uchafu unaotia aibu serikali na hata mimi mbunge.

“Ushahidi huu tutaukabidhi kwa vyombo vinavyohusika (Takukuru). Tunataka pia watendaji wa serikali waliohusika katika matukio hayo waondolewe kwenye ofisi za umma kwa kuwa hawana sifa muhimu ya uadilifu.”

Akiongea kwa kujiamini, Nassari alitoa mkanda wa video unaowaonesha mkuu wa wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti; Katibu Tawala, wilaya ya Meru, Timotheo Mzava na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Christopher Kazeri, wakirubuni madiwani kwa njia ya rushwa na ajira.

Viongozi hao wanaonekana kwenye mkanda wa video, wakishawishi baadhi ya madiwani wa Chadema, kukihama chama chao kwa ahadi kuwa watapewa ajira, kulipwa mafao yao ya udiwani kabla ya kustaafu na kulipwa posho zao.

Ahadi nyingine ni kukamilishiwa miradi yao ya maendeleo waliyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliyopita, ili pale watakapopitishwa kugombea nafasi zao kupitia CCM waweze kushinda kirahisi.

Kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, kumeibuka wimbi la madiwani wa Chadema kukimbia chama chao na kuhamia CCM. Wote wanaohama wamekuwa wakieleza kuwa wanafanya hivyo ili “kumuunga mkono Rais Magufuli.” Tujadili:

Kwanza, madai kuwa madiwani wanaohama Chadema na kujiunga na CCM wamechukua hatua hiyo ili kumuunga mkono Rais Magufuli, yamekosa mashiko na yamesheheni ulaghai.

Hii ni kwa kuwa kiongozi anayeambiwa anapaswa kuungwa mkono – Rais John Magufuli – ni kiongozi wa umma na mkuu wa nchi. Ameapa kulinda na kutetea katiba.

Ndani ya katiba ambayo mkuu wa nchi ameapa kuilinda na kuitetea, kumetajwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, ataongoza bila ubaguzi.

Rais wa Jamhuri hatatekeleza kazi zake kwa kupendelea watu kutoka dini yake, kabila lake, rangi yake; na au sehemu anakotoka. Hatabagua yoyote kwa kuwa siyo mwanachama wa chama chake.

Rais anajua madhara ya ubaguzi na ubinafsi; ni adui wa haki, upendo, umoja, amani na maendeleo. Unaweza kusababisha wananchi ambao ndio wazalishaji wakuu wa uchumi, wakapoteza maisha kwa kuwa baadhi ya watu wachache wametumia madaraka yao kujinufaisha binafsi.

Kwa muktadha huo, rais wa nchi anapaswa kuungwa mkono na watu wote – wenye dini na wasio na dini. Wenye elimu na wasiokuwa nayo.

Kutaka kushawishi umma kuwa kumuunga mkono Magufuli, ni sharti ujiunge na chama chake, ni sawa na kutaka kila mtu kuwa mwanachama wa CCM.

Rais Magufuli ni muumini wa madhehebu ya Katoliki. Kusema huwezi kumuunga mkono mpaka ukajiunge na chama chake, ni sawa na kusema watu waache madhehebu yao, dini zao na makabla yao, ili kujiunga na dini yake, kabila lake na dhehebu lake.

Aidha, Rais Magufuli ni mwanasiasa. Kudai kuwa huwezi kumuunga mkono hadi ujiunge na chama chake, ni sawa na kutaka watu wote – wanajeshi, mapadri, masheikh na maimamu – wajiunge na vyama vya siasa.

Vinginevyo, hawawezi “kumsaidia Rais kuendesha nchi.” Hiki ni kisingizio kinachoweza kutolewa na watu walionunuliwa tu. Siyo vinginevyo. Watu huru na wenye uwezo wa kujisimamia, hawawezi kuzungumza kauli za aina hii. Hawawezi.

Pili, kitendo cha mkuu wa wilaya, mkurugenzi wa halmashauri na katibu tawala, kujihusisha na “biashara haramu ya ununuzi wa madiwani,” kinathibitisha kuwa watumishi wengi wa umma tulionao, ni “waoga, wasiojiamini na wasiothubutu kumueleza rais ukweli.”

Badala yake, wanatenda kile ambacho wanaamini rais anakipenda. Kwa mfano, kwenye video ambayo Nassari ameonesha waandishi wa habari, kunaonekana mkuu wa wilaya – Alexander Mnyeti akimueleza diwani anayemchumbia, “rais atafurahi kusikia umejiunga na chama chake.”

Naye diwani anaonekana akiwa na mashaka ya kutolipwa fedha zake iwapo atatekeleza mradi wa mkuu wa wilaya na ambao anamhusisha na mkuu wa nchi. Huyu ni diwani wa kata ya Makiba, Emmanuel Mollel.

Kunaonekana hata majibu ya mkuu wa wilaya. Anasema, mara baada ya diwani kuandika barua ya kujiuzulu na kuhamia CCM, atatafutiwa ajira.

Anasisitiza, “mimi sifanyi uamuzi, lakini nina ushawishi mkubwa kwa viongozi wangu wakuu. Katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, tayari amechukua wasifu wako (CV).”

Anaongeza, “Rais Magufuli anatarajiwa kufanya ziara mkoani Arusha baada ya wiki tatu zijazo (kuanzia siku waliyokuwa wakizungumza) na kupata nafasi ya kukutana na rais na kuzungumza naye.”

Anamuahidi kuwa ni yeye Mnyeti atakayemchukua diwani huyo na kumpeleka moja kwa moja kwa rais ili wakutane usiku wa siku ambayo rais alifika Arusha.

Mnyeti anasema, “madiwani wengine wawili wameshatafutiwa ajira katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na katika ofisi za wizara ya maliasili na utalii.”

Anamtaka diwani huyo aandike barua ya kujiuzulu hata kama hana ajira, yeye yuko tayari kumlipa mshahara ili aweze kutunza familia yake.

Si hivyo tu: Video inamuonesha diwani huyo akilalamikia kiasi cha Sh. 2 milioni alizoahidiwa kupewa na mkuu wa wilaya.

Naye Kazeri – mkurugenzi wa halmashauri – anaonekana kwenye video akitetea malipo hayo kwa kusema, “hakuna diwani aliyepewa zaidi ya kiasi hicho cha fedha.”

Anasema, tayari amepiga hesabu ya vikao vilivyosalia vya baraza la madiwani kabla ya mwaka 2020.

Nassari anaeleza diwani Mollel ameshaelekeza mhazini wa halmshauri kulipa kiinua mgongo cha miaka mitano pamoja na posho za vikao vyote kwa madiwani wote waliojiuzulu, ingawa wamehudumu kwa mwaka mmoja na nusu.

Anafika mbali zaidi kwa kusema, katika uchaguzi wowote utakaoitishwa, hakuna mgombea wa Chadema atakayetangazwa hata kama atakuwa ameshinda.

Mkurugenzi wa halmashauri ndio ofisa uchaguzi wa wilaya. Ndiye anayetangaza matokeo ya mbunge na rais katika eneo lake.

Kauli yake hii inathibitisha madai ya upinzani kuwa uchaguzi mkuu ujao hautakuwa huru na haki. Kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ni tawi la chama kilichoko Ikulu.

Hivyo basi, ili matakwa ya wananchi yaliyopo kwenye sanduku la kura yaweze kuheshimiwa, NEC iundwe upya. Wakurugenzi wa halmashauri waondolewe kwenye jukumu la kusimamia uchaguzi.

Tatu, hatua ya mkurugenzi, katibu tawala na mkuu wa wilaya, kuamua kugawa rushwa kwa madiwani wa upinzani, ni kinyume na mzizi wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma ya mwaka 1995.

Sheria hii iliyotungwa mahsusi ili kudhibiti tabia na mienendo ya viongozi wa umma, inapiga marufuku matumizi mabaya ya madaraka kwa viongozi wa umma.

Kwa mujibu wa sheria hii, ni marufuku kwa kiongozi wa umma kutanguliza maslahi yake binafsi katika utendaji kazi wake.

Mnyeti, Kazeri na Mzava wametumia madaraka yao kughiribu baadhi ya madiwani kuhama. Wanalipwa mshahara unaotokana na kodi za wananchi. Wanapaswa kuhudumia wananchi bila kujiegemeza kwenye chama kimoja cha siasa.

Kutokana na hali hiyo, ni muda muafaka sasa kwa Tume ya Maadili; Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru), Jeshi la Polisi na hata Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, kuchunguza mwenendo wa Mnyeti na wenzake na kuchukua hatua.

Vinginevyo, vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, utapakanyaji wa rasimali za taifa, wizi, udanganyifu na “undumilakuwili,” havitaisha kwenye taifa hili.

error: Content is protected !!