Monday , 4 March 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Bwana Ali Juma ‘kafa ngangari’
Makala & Uchambuzi

Bwana Ali Juma ‘kafa ngangari’

Spread the love

“Masikini bwana Ali, kafa ilhali yuajua
Masikini bwana Ali, kafa yuaona
Masikini bwana Ali, kafa yuaasa
Masikini bwana Ali, kafa yungangari”

NAANDIKIA haya kwa heshima ya Ali Juma Suleiman, Mtanzania wa Zanzibar, aliyeuliwa na madhalimu wanaohifadhiwa na utawala wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Ameuliwa saa 48 baada ya kushambuliwa kwa silaha sizizo za moto na kutokwa damu nyingi, anaandika Jabir Idrissa.

Wauaji wake walimfuata nyumbani kwake Mtopepo, mjini Zanzibar, usiku wa manane kuamkia Septemba 28.

Walikuwa katika idadi isiyofahamika. Ni wengi kupita kumi, madume wakiwemo waliobeba bunduki za moto. Wengine walibeba marungu ya miti na mapande ya nondo. Baadhi walivaa sare za vikosi vya ulinzi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Uvaaji wa sare wenyewe ni nusu sare, nusu marapurapu – suruali, fulana, kofia za ovyoovyo. Baadhi walivaa mabuti ya kiaskari, wengine viatu vya raba. Waliizunguka nyumba yake. Wakaanza kumuita kwa sauti ya kuogofya. Hakuitika.

Katika simulizi aliyotoa kabla ya kukata mauti, huku akionesha miguu iliyofungwa mabendeji ikionesha kutapakaa damu nyingi, kiongozi huyu mwandamizi wa Chama cha Wananchi au the Civic United Front (CUF), katika Kurughenzi ya Habari, Uenezi na Mawasiliano na Umma, Wilaya ya Magharibi A, anasema mkewe ndiye alitangulia kuchungulia nje.

Akaona watu hao wengi. Haraka aliwatambua kuwa ni watu wa vikosi vya SMZ. Akajua ilikuwa zamu yao familia ya Ali Juma Suleiman. Akamjulisha mumewe. Wakajua wamekutwa. Wakakaza moyo. Wakaafikiana wasiitike hata kama tayari wakati huo waovu walishatishia kuvunja na kuingia ndani.

Baba wa nyumba akajificha. Wanaume wakavunja. Wakaingia ndani. Wakamsaka. Wakafanikiwa kumuona alikojificha. Wakamchomoa. Wakaanza kumpiga. Akapigwa huku mkewe anaona. Wakatamka mengi ya vitisho vya kishetani. Wakasakura ndani. Wakabeba walichokitaka. Ni pamoja na fedha.

Walipomtoa nje, Ali Juma Suleiman alikuwa hana nguvu zake za kawaida.

Unakuwa na nguvu gani mtu uliyedhibitiwa na kundi la watu wenye silaha za moto wakiwemo walioficha nyuso zao wasitambuliwe? Huna ujanja. Unawafuata watakavyo. Aliwafuata. Akasukumwa mpaka ndani ya gari. Gari nzuri ya sirikali – hardtop nyeupe.

Akafungwa kitambaa usoni. Ili iweje? Ebo, bwana Ali asiendelee kuona watekaji na watesi wake. Asione apelekwako. Asione, asione.

Kweli hakuona. Hela akisikia sauti na maneno yao madhalimu. Kipigo. Kila aliyependa alimpiga. Lakini kipigo zaidi alikipata kule alikoshushwa. Hakujua alikokuwa. Alipigwa. Aliteswa. Alidhalilishwa. Alihujumiwa. Alidhulumiwa khasa. Yote akitendewa huku akitupiwa maneno ya kipuuzi.

Bwana Ali, muuza vyakula vya matunda shambani kama ndizi, muhogo na nazi, achilia mbali matunda aina kwa aina, kwenye eneo la Mtoni Kidatu, alitupwa porini. Baada ya kusalimika kifo pale kabla, aligundua alikuwa msitu wa Masingini. Kuda ya Mwenyeezi Mungu ilimuibua huko hadi eneo ambako alipata msaada wa watu wawili waliokuwa na gari la ng’ombe.

Watu wa kawaida sana walimsaidia, baada ya watu makini wenye akili zao na uwezo wao wa kila kitu, kumtelekeza. Yumkini waliogopa kuja kushambuliwa na madhalimu walewale. Wanajua imepata kutokea.

Hatimaye alipata msaada wa matibabu. Ila alilazimika kupelekwa Hospitali Kuu ya Zanzibar – Mnazimmoja Referral Hospital – kwa kuwa madaktari waliogopa kumtibu zaidi kwa kuhofia usalama wao. Wale watu wawili waliomsaidia kwa kumpakiza ndani ya gari la ng’ombe, walimpeleka mpaka hospitali.

Bwana Ali alipofanikiwa kufika nyumbani kwake, alikaguliwa na uongozi wa CUF, miongoni mwa watu waliofika haraka. Akatoa simulizi. Hayo niloyatanguliza, ameyaeleza katika video iliyoenea mitandaoni.

Kauli aliyoirudia mara kadhaa mbele ya viongozi wenzake, ilikuwa “Tusikubali kuonewa hata iweje.”

Maneno haya ndiyo yanatumika sasa kumtaja Ali Juma Suleiman kuwa amekufa shahidi. Kifo cha haki kutokana na ushiriki wake katika kupigania wanayoamini ni haki yao. wazanzibari wanapigania haki ya utawala wanaoutaka. Wanadai utawala waliouchagua. Wanawajua viongozi waliowachagua katika uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015. Ni uchaguzi uliofutwa kibabe tarehe 28 Oktoba, siku tatu baadaye wakati yakitarajiwa matokeo ya kiti cha urais.

Maneno yake ya kimapambano yanathibitisha kuwa aliuliwa kwa sababu hiyohiyo ya kupigania haki ya wananchi – kuongozwa na wale waliowapatia ridhaa kupitia uchaguzi huo wa 25 Oktoba 2015, na si mwengineo.

Kwa hivyo, Ali Juma Suleiman, ameuliwa. Waliomuua ni watu wanaokwenda kwa hifadhi ya utawala ulioko chini ya Dk. Ali Mohamed Shein, mwanasiasa ambaye analalamikiwa haongozi kwa ridhaa ya umma kupitia ule uchaguzi halali uliofutwa kibabe.

Waliomuua mpigania haki Ali Juma Suleiman, aliyezaliwa 1950 kisiwani Pemba, akiwa ameacha watoto 16 na kizuka mmoja, ni watu ambao wamekuwa wakilalamikiwa kwa miaka yote ya mfumo wa vyama vingi tangu 1995 ulipomalizika uchaguzi wa kwanza.

Wamekuwa wakiendesha visa vya kidhalimu kwa njia tofauti tangu hapo. Baadhi ya njia ni kutia moto makazi ya wananchi wanaoamini wanapenda CUF. Wananchi wengine walichomewa mali zao – vitegauchumi vyao – kwa sababu waliaminika wanasaidia kifedha upinzani.

Hakuna hata wakati mmoja walidhibitiwa. Ndio maana kwa miaka mitano mfululizo akiwa ndani ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, alilieleza tatizo la askari wa vikosi vya serikali kushambulia wananchi mitaani na kuwaacha wakiwa majeruhi na baadhi ya wakati wakiwa wamewaibia mali zao zikiwemo fedha.

Maalim Seif alipata kusema wakati huo akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alikuwa akilieleza suala hilo mara kwa mara ndani ya vikao vya Baraza la Mapinduzi (Baraza la Mawaziri) na hata anapokuwa na vikao vya mashauriano na rais peke yao au pamoja na Makamu wa Pili, Balozi Seif Ali Iddi.

Chini ya serikali ya umoja wa kitaifa iliyodumu kwa miaka mitano tu, kuanzia Novemba 2010 mpaka Oktoba 2015, mawaziri, hasahasa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili, Mohamed Aboud Mohamed, wakisema serikali itachukua hatua kuchunguza.

Basi huwa tu “Serikali itafanya uchunguzi na kuchukuwa hatua.” Ahadi za namna hiyo zilitolewa hata kabla ya kuingia kwa serikali ya mfumo wa umoja wa kitaifa. Mashambulizi ya wananchi yaliyofanywa na askari hao, ni ya kawaida Unguja na Pemba.

Juni mwaka huu, kupitia mtandao huu, niliandika makala ikionesha udhalimu wa askari hawa ambao baada ya kuishi kwa jina la Janjaweed mfano wa wale wanamgambo waliokuweko Sudan wakati ule, walopachikwa na sasa wanaitwa MAZOMBI.

Askari waliotambuliwa kutoka kikosi cha Valantia (KVZ), walimjeruhi mchuuzi wa bidhaa za mkononi mchana kweupe. Walimpiga, wakamchoma moto na kumtelekeza kambini kwao bila ya kumpatia matibabu.

Wakitumia lori aina ya Fuso, walimkuta mchuuzi huyo Abdulla Ahmed Juma, Mchangani, mtaa katikati ya mji wa Zanzibar, na kumshambulia kwa kumchangia hadi kumtia moto. Abdulla alikuwa na umri wa miaka 29.

Walimnyang’anya bidhaa zake za nguo na viatu, na wakamuibia Sh. 800,000 alizokuwa nazo.

Kaka yake, Nadir Ahmed Juma, alinieleza kwa simu: “Abdulla alipelekwa mpaka kwenye kambi ya Valantia pale Gymkhana. Akawekwa bila ya kupatiwa matibabu. Hawakumpa huduma yoyote ya tiba ilhali wamemshambulia watakavyo na kumchoma moto. Labda walikusudia kumfanyia vibaya zaidi ya walivyofanya.”

Miezi mitatu kabla, Machi, mazombi wakiwa katika operesheni za kidhalimu kwenye mitaa ya mji, walishambulia watu kadhaa akiwemo mzee Abdalla Pavu wa miaka 72, aliyekuwa ameketi kwenye barza ya CUF inayodhaminiwa na mwakilishi wa Pangawe, Suleiman Mchukucha.

Ndani ya Baraza la Wawakilishi na ndani ya Bunge, vilio vya wawakilishi wa CUF kutaka watu hao wadhibitiwe, vimepuuzwa kila vinaposikika.

Mara kadhaa mawaziri na manaibu wao wanasema serikali itachunguza. Lakini naibu waziri wa sasa wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni Yussuf amepata kusema “Jeshi la Polisi halina taarifa za matukio hayo.”

Alitaka walioathirika waripoti vituo vya polisi. Lakini alipopelekewa orodha ya karibu waathirika 400, aliishia kunyamaza.

Mazombi wanatumika kudhoofisha upinzani. Lengo ni kuimarisha utawala dhalimu. Manufaa makubwa zaidi wanayapata wakuu wa CCM. Mwenyezi Mungu tu anajua watakavyoishia; wao na wanaowatuma!

Muandishi ni Mhariri wa MwanaHALISI, gazeti lililofungiwa na Serikali tarehe 19 Septemba 2017.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Makala & Uchambuzi

Vijana wanavyoandaliwa kuziba pengo la ujuzi sekta ya madini

Spread the loveMOJAWAPO ya sekta ambazo katika miaka ya 2000 hazikuwa na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Lowassa: Mwanasiasa aliyetikisa CCM, Chadema

Spread the loveWAZIRI Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Edward Lowassa (70) amefariki Dunia...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Uongozi wa Samia kuendelea hadi 2030

Spread the loveKWETU sisi tuliowahi kusoma sekondari, iwe O levo au A...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Bado askari wastaafu wanaonewa

Spread the loveRAIS wangu Samia Suluhu Hassan tunaendelea kumshukuru Mungu kwamba wote...

error: Content is protected !!