Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kubenea: Nitawasaka wanaonichafua
Habari za Siasa

Kubenea: Nitawasaka wanaonichafua

Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo
Spread the love

MBUNGE wa Ubungo (CHADEMA), Saed Kubenea, amekana madai kuwa anataka kukihama chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Faki Sosi… (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari, ofisi kuu ya Chadema Kanda ya Pwani, Magomeni jijini Dar es Salaam, Kubenea amesema, taarifa kwamba anataka kujiunga na CCM na kujiuzulu ubunge siyo za kweli.

“Siwezi kuondoka Chadema na kujiunga na CCM kwa kuwa siyoni jipya linalovutia ndani ya chama hicho ili nijiunge nalo,” ameeleza.

Kubenea amesema, hana bei na hakuna fedha itakayoweza kumnunua na wala hana mpango wa kuondoka Chadema na kujiunga na CCM.

Amesema siku zote yeye hujali utu zaidi kwa sababu heshima waliompa wananchi wa Ubungo ni kubwa kwake.

“Napenda niwahakikishie sijawahi kuzungumza na chombo chochote cha habari kwamba nina mpango wa kutoka Chadema kwenda kwingine. Wala sijawahi kuzungumza na mtu yeyote wa CCM au Chadema juu ya kuondoka kwenye chama changu cha sasa; na au kunishawishi kujiunga na CCM. Sijawahi,” amesisitiza.

Amesema, “nimekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya CCCM kuhusu masuala mbalimbali ikiwamo ubinafsishwaji wa mashirika ya umma na uwekezaji unaofanywa na kampuni za kigeni hapa kwetu.”

Alisema kwa miaka 15 amekuwa akiandika habari za uchunguzi na uchambuzi kwa kukosoa sera ya ubifsishwaji ambayo imewaacha watanzania maskini na kujenga nyufa baina walioo nacho na wasio nacho.

“Kwa uelewa wangu sioni jipya ambalo linaweza kunishawishi kwenda CCM na mimi sijawahi kununuliwa na huwa sinunuliki.

“Nikifanya jambo lolote ujue limetoka ndani ya moyo wangu, kama vishawishi vya fedha nimevipitia vingi lakini sijawahi kuyumba katika msimamo wangu,” ameeleza Kubenea.

Alisema amekuwa katika mageuzi hayo kwa miaka 15 sasa na kujiwekea historia ya kukosoa utawala wa CCM kuanzia wa awamu tatu uliokuwa ukiongozwa na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa.

“Kwa miaka mingi nimekuwa nikiwakosoa kwa dhamira chama hiki kijirekebishe, kifuate itikadi yake ya ujamaa na kujitegemea, kifuate misingi yake ya asili ya utu wa mtu na siyo kitu na kitimize ahadi zake 10 za TANU… wakati huo tulikuwa tukikisema sana kwenye magazeti na CCM ilikuwa inajirekesha,” alisema.

Alisema katika miaka 10 ya utawala wa awamu ya nne ulioongozwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, CCM ilikuwa inakwenda inazaliwa upya lakini hakujiunga kwa kuwa aliamini katika kazi za utetezi wa watu nje ya kuwa na chama.

Alisema ameweza kujenga jina lake kwa miaka 15 na kupata ubunge na sifa nzuri za Chadema na anaamini juhudi binafsi za kutetea wananchi pia zimemfikisha hapo alipo.

“Sasa nimepata fursa ya kutunga sheria, mimi mbunge sina bei, nikiondoka Chadema nitaondoka kwa dhamira yangu siyo kununuliwa.

Kubenea alisema, “siyo mtu aniambie nimefikia bei, mimi sina bei, utu wangu ndiyo bei yangu.”

Alisema hawezi kufanya uamuzi huo kwa kuwa atawasaliti wananchi wa Ubungo na Watanzania kwa kuwa walijitoa kwa kumchangia kwa hali na mali aweze kufanikisha safari yake ya kupata kiti hicho.

Alisema, “kuna watu nimeshiriki kuwaleta Chadema watanielewaje? Miongoni mwao yumo Sumaye (Waziri Mstaafu Frederick Sumaye) na Lowassa (Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa).

Alihoji: “Hawa viongozi wangu, watanionaje? Niwaambie tu kwamba nimesikitika sana, nimefedheeshwa mno na nimeumizwa kwelikweli na habari hizi za mimi kuondoka Chadema.

“Mimi bado mwanachama na mbunge wa jimbo la Ubungo mpaka 2020 labda nife au kitokee kitu kingine ambacho sikijui.

“Lakini kwa utashi wangu nitaendelea kuwa mwanachama wa ukweli ninayekipigania chama kupitia vikao, hivyo hayo maneno yapuuzwe,” alisema Kubenea.

Alisema hakuna mtu yeyeote aliyewahi kuzungumza naye na kama yupo aweke ushahidi mezani.

Alisema siku zote akipewa fedha huwa si za hongo wala ushawishi wa kitu fulani isipokuwa ni msaada tu lakini siyo za ushawishi… mtu anaamua tu kumpa.

Alisema lengo la kufanya propaganda hizo ni kuwatoa wanachama wa Chadema kwenye mstari wa kuwaza uchaguzi mdogo katika majimbo ya Longido na Singida Kaskazini na Songea Mjini.

“Wanataka wanachama wetu, wabunge watumiane wenyewe kwa wenyewe wao wanajiandaa ikifika baada ya wiki moja tunapigwa.

“Wanataka wanachama wahangaike kujibu mambo ya mitandaoni,” alisema Kubenea.

Mjadala juu ya Kubenea kujiunga na CCM ulipamba moto kwa kasi kati ya Jumatatu na Jumatano wiki hii, hasa baada ya mbunge mmoja wa Chadema aliyejipa kazi ya kupiga ramli, kudai kuwa ameoteshwa kutokea kwa jambo hilo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!