Thursday , 13 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kiki ya Babu Seya haimwachi salama Rais Magufuli
Habari za SiasaTangulizi

Kiki ya Babu Seya haimwachi salama Rais Magufuli

Spread the love

Mheshimiwa Edward Lowassa aliposema kuwa angemtoa Babu Seya, CCM walimdhihaki wakisema, “atamtoaje mbakaji?” Anaandika Ansbert Ngurumo … (endelea).

Leo Rais Magufuli amemtoa Babu Seya na mwanaye. Nasubiri kusikia vigelegele vya wana CCM.

Hapa kuna mambo ya kutafakari. Hili ni tukio jema kwa Babu Seya na familia. Hatimaye sala zao, za mshabiki wao, na raia wema wengine zimesikilizwa, wamekuwa huru.

Kwa vyovyote vile hili ni tukio la kisiasa kwa upande wa Magufuli. Kwa wafuatiliaji wa siasa za watawala wetu, hiki ni kijembe cha kimya kimya dhidi ya Rais Kikwete na serikali ya awamu ya nne.

Ni mbinu ile ile ya awamu moja kutaka kuaibisha awamu iliyoitangulia ili kupata kiki ya kisiasa.
Lakini pia huu ni mwendelezo wa utekelezaji wa ajenda za wapinzani. Na hiki ni kielelezo cha umuhimu wa demokrasia, hasa uhuru wa kujieleza.

Kama Lowassa asingeyasema haya (CCM wakamzomea), yawezekana Magufuli asingejua umuhimu wa kumwachia huru Babu Seya katika mazingira haya.

Kumbe sauti za wapinzani ni muhimu kwa usitawi wa watawala na raia. Basi, wapinzani wasikilizwe wasizibwe midomo kwa vitisho vya dola, maana wana maoni, maono, mawazo, ujuzi, mang’amuzi, upeo, na hekima zinazohitajika kwa ajili ya watawala kufanya uamuzi. Kupuuza wapinzani ni kukwepa yote hayo. Ni kuua nchi.

Lipo la nyongeza. Wapika propaganda wa CCM na serikali wanadhani watu wanamshangilia Magufuli kwa kumwachia Babu Seya.

Kimsingi watu wanashangilia Babu Seya kuwa huru. Ni ushindi aliopigania kwa muda mrefu. Wanamshukuru kwa Babu Seya kapata haki yake kwa njia hii. Basi!

Wala hili halitampa kiki Magufuli kama alivyotarajia, kama alivyoshawishiwa na waliompa ushauri huo.

Watanzania wanajua kuwa kumwachia huru Babu Seya na wenzake hakutaleta chakula mezani kwao. Hakupandishi bei ya mazao yao, wala mishahara ya watumishi waishio kwa mshahara. Hakuongezi posho yao halali.

Hakutaongeza mzunguko wa shilingi mitaani. Hakutaboresha biashara na uwekezaji nchini.

Hakutaondoa ukatili katika mioyo ya watawala. Wakati huyu anaachiwa, wao wanawinda wengine ili wawatokomeze kwa vile tu wanakosoa serikali.

Hakufuti ukatili wa watu wale wale waliotaka kumuua Tundu Lissu, wala hakupeleki pesa ya matibabu Nairobi.

Hakusaidii Ben Saanane apatikane. Hakumrudishii uhai Alphonse Mawazo.

Hakufanyi Watanzania wawe huru katika nchi yao, na hakuwafanyi watawala waache mbinu chafu za kutusaka ili watuangamize kama walivyoangamia hao wanaookotwa ziwani, baharini, na mitoni kila mara wakiwa wamefungwa kwenye viroba.

Hakurejeshi uhai wa makumi ya wananchi waliouawa Kibiti. Hakurejeshi mwandishi wa Mwananchi, Azory, aliyepotezwa na watu wasiojulikana.

Hakufungulii magazeti makini yaliyofungiwa au yaliyofutwa na serikali. Inabaki kuwa kiki ya kisiasa isiyompeleka JPM popote isipokuwa ofisini mwake.

Yawezekana anaposikia wananchi wanashangilia anadhani wanamshangilia yeye. Amekosea. Wanajua wanachoshangilia!

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari MchanganyikoHabari za Siasa

Deni la Serikali lafikia trilioni 91

Spread the loveWaziri wa Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo amesema hadi...

Habari za SiasaTangulizi

Mbunge Dk. Shogo Mlozi afariki dunia

Spread the loveMbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) ambaye pia ni...

KimataifaTangulizi

Boti yazama DRC, 80 wafariki dunia

Spread the loveJUMLA ya watu 80 wameripotiwa kufariki dunia huko nchini Congo...

BiasharaHabari MchanganyikoHabari za Siasa

Marekani yasaka fursa uwekezaji sekta ya nishati Tanzania

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko amekutana...

error: Content is protected !!