Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Fuatana na Maalim kutoka Ikulu ya Zanzibar
Habari za Siasa

Fuatana na Maalim kutoka Ikulu ya Zanzibar

Spread the love
MAALIM Seif Sharif Hamad, ameapishwa kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar. Kuapishwa kwake, kumetokana na matakwa ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, toleo la mwaka 2010, linarohusu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUKI), Visiwani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Akizungumza kwa hisia kali, Maalim Seif alisema, uamuzi wa kuingia kwenye serikali hiyo, haukuwa mwepesi kutokana na kile kilichotokea kwenye uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa 27 na 28, Oktoba mwaka huu.”

Amesema, “amekubali kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ili kuweza kufungua milango ya kutibu majeraha yaliyotokana na uchaguzi mkuu uliogubikwa na vitendo vya uvujinfu wa amani na hivyo kuacha majeraha makubwa kwa baadhi ya wananchi. Ameingia kwenye serikali kwa kuangalia maslahi mapana ya Zanzibar.”

Kwa umuhimu wa kile alichoeleza, tumeamua kuwaletea neno kwa neno ya kile alichokisema Maalim Seif, katika hafla hiyo – Mhariri MwanaHALISI.

HOTUBA YA MAALIM SEIF SHARIF HAMAD, MWENYEKITI WA ACT WAZALENDO KATIKA HAFLA YA KUAPISHWA KUWA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS, IKULU ZANZIBAR TAREHE 08/12/2020

Mhe Dkt Hussein Ali Hassan Mwinyi,

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,

Waheshimiwa Viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na Serikali na

Waheshimiwa Wananchi wa Zanzibar,

Mheshimiwa Rais,

Kwanza, nianze kwa kumshukuru Mwenyenzi Mungu muumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake kwa kutuwezesha kukutana hapa kwa salama na amani kufanikisha shughuli yetu hii adhimu.  Sala na salamu zimfikie Mtume wetu Muhammad S.A.W.

Pili, niwashukuru sana Wananchi wa Zanzibar kwa imani kubwa walioyonayo juu yangu, kwa hakika hujikuta nipo katika wakati mgumu kila ninapojiona ninaishiwa nguvu za kuwatumikia ndipo imani yao huongezeka na kunipa nguvu kubwa. Imani ya wananchi hawa kwangu umekuwa ni wito mtakatifu unaonilazimisha kusimama kuendelea kuwatumikia.

Tatu, nakishukuru sana chama changu kwa kuwa na imani nami na hivyo kupendekeza jina langu kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Mwisho, lakini si mwisho kwa umuhimu, nakushukuru wewe Mhe Rais kwa nia yako thabiti uliyoionyesha ya kujenga maridhiano na kukubali pendekezo la chama changu na kuniteua kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais.

Mheshimiwa Rais,

Kwa upande wetu, uamuzi wa kuingia katika Serikali, Baraza la Uwakilishi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haukuwa uamuzi rahisi na mwepesi. Ulikuwa ni uamuzi uliotufikirisha sana, tumejadili sana na tumepishana sana. Hatimaye tukafikia uamuzi. Moja ya sababu zilizotufanya kufikia uamuzi huo ni imani yetu kwako wewe binafsi, maneno yako, vitendo na ishara zako ambazo zimetushawishi kuwa unayo nia njema na dhamira safi ya kututoa tulipokwama na kuibadilisha Zanzibar yetu katika nyanja zote. Tumeona wewe ni mtu tunayeweza kufanya naye kazi, tunayeweza kusikilizana na tunayeweza kukupa nafasi uthibitishe nia yako njema. Nia yako ambayo ndiyo iliyotufanya na sisi tutangulize nchi kwanza  licha ya madhila yote yaliyojitokeza katika Uchaguzi uliopita.

Wenzangu walipokuja na wazo hili la sisi kuungana na wewe, na baada ya kushauriana na wanachama wetu, niliwashauri kuwa sasa ni wakati wangu mimi kupumzika na kupeleka jina la damu mpya. Hawakunikubalia. Waliniambia, wewe ndiye uliyeongoza maridhiano na Rais Amani Karume mwaka 2009 na wewe ndiyo uliyeshiriki Serikali ya Kwanza ya Umoja wa Kitaifa na Mheshimiwa Rais wa wakati huo Dkt. Mohamed Ali Shein. Wakaniambia maadam wewe ndio umelianza, basi ulimalizie. Wakasema wewe mtu mzima na utu uzima dawa. Wakanitaka nikubali ili nije kusaidia azma hii ya kutibu majeraha ya Zanzibar na kuyastawisha maridhiano. Sikuweza kuwakatalia. Niliwakubalia na ndio maana leo niko hapa.

Mheshimiwa Rais,

Serikali ya Umoja wa Kitaifa [SUK] iliyoasisiwa na Katiba ya Zanzibar kupitia Marekebisho ya Kumi ya Katiba ya mwaka 2010 ilikusudiwa kuwa chombo cha kusimamia, kuratibu na kuongoza juhudi za Wazanzibari kufikia Maridhiano na Umoja wa Kitaifa.  Haikuwa na bado sio lengo la Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuwa chombo cha kugawana vyeo kwa kambi za kisiasa.  Ni vyema jambo hili tukalikumbuka kila wakati.

Katika kuwasaidia wale wenye imani au ufahamu potofu juu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, napenda kutumia mfano rahisi.  Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni sawa na chombo cha usafiri.  Kwa msafiri yeyote awe wa baharini, angani au nchi kavu, lengo lake sio kuingia katika meli, ndege au gari.  Lengo lake ni kufika safari aliyopanga.  Safari ya Wazanzibari ni Maridhiano ya Kweli, Mshikamano na Umoja wa Kitaifa.  Chombo chetu cha kufika safari hiyo kwa wakati ni Serikali ya Umoja wa Kitaifa.  Hivyo, ni wajibu wa viongozi sote ambao tumepewa jukumu la kuongoza Serikali kuhakikisha kwamba tunaelekeza chombo hichi katika safari hiyo.

Mheshimiwa Rais,

Maridhiano yale yalilenga sio tu kuwa na mfumo shirikishi katika uendeshaji wa nchi bali yalikusudia kuondoa kabisa siasa za mivutano zilizotawaliwa na chuki, uhasama na visasi ambavyo kwa njia moja au nyengine vimekwamisha ustawi wa nchi yetu kwa muda mrefu sana. Tulitarajia pia kupitia maridhiano yale tungetoka katika diwmbi la historia ya kuwa na chaguzi za mivutano ambazo zimekuwa ni sababu ya maafa makubwa kwa wananchi wa Zanzibar.

Kwa masikitiko makubwa sana, Maridhiano yale yalikwama njiani.  Kwasababu hii basi uchaguzi wa mwaka 2020 umeturejesha tulikotoka. Uchaguzi umetuacha na uhasama mkubwa ZAIDI, umetuacha na maafa makubwa zaidi. Haya ni mambo ya aibu sana na fedheha kwa nchi yetu. Hili ni doa katika historia ya nchi yetu na hatuna budi kuchukua hatua thabiti za kulifuta doa hili kwa njia itakayowaridhisha waathirika na wananchi kwa ujumla. Kuja kwetu Serikalini na kuingia kule Barazani, ni ishara ya nia yetu njema ya kutaka kushirikiana na wewe kutafuta majawabu wa kudumu ya matatizo haya.

Mheshimiwa Rais,

Uchaguzi Mkuu uliopita na changamoto zilizojitokeza zimetufunua macho kuwa majawabu ya kisheria na kikatiba pekee hayatoshi kutufikisha katika matamanio yetu ya maridhiano. Tunao wajibu sawia wa kutafuta majawabu pia ya kutafuta muafaka wa kijamii. Zanzibar iliyogawika haiwezi katu kupiga hatua yoyote ya maendeleo.  Maridhiano, amani na utulivu ndio jawabu la kuivusha Zanzibar kutoka ilipo sasa kwenda kuwa Zanzibar iliyopiga hatua kubwa kimaendeleo.

Kwasababu ya mwelekeo huu ndio maana chama changu cha ACT Wazalendo na mimi mwenyewe binafsi tumekubali kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kusaidia na Kuijenga Zanzibar mpya. Ni imani yangu binafsi na Chama Changu kuwa wajibu wa mwanzo wa Serikali hii ya awamu ya 8 utakuwa ni kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar kuwa wa moja. Kwa muktdha huo basi tumekubali kuja kushirikana na wezetu katika kuhakikisha kuwa yaliyotokea kabla, wakati na baada ya Uchaguzi wa Oktoba 2020 hayajirudii tena.

Mheshimiwa Rais,

Leo si siku ya kusema sana. Bila shaka tutapata wasaa mwingi wa kukaa pamoja, kushauriana na kutafakari mustakhabali wa Zanzibar yetu na nini kwa pamoja tunaweza kufanya. Nikuhakikishie juu ya dhamira yetu safi mimi na wenzangu ya kufanya kazi na wewe kwa manufaa ya Wazanzibari wote.

Nimalizie kwa kukupongeza Mhe Rais kwa kuanza kazi vizuri. Nimpongeze pia Ndugu yangu Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais. Aidha niwapongeze Mawaziri wote waliobahatika kuteuliwa pamoja na Wakuu wa Mikoa. Niwapongeze pia wawakilishi Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazuri na Mheshimiwa Omar Said Shabaan kwa kuteuliwa na wewe kuwa Wawakilishi.

Mheshimiwa Rais,

Mwisho kabisa nitoe wito kwa Wazanzibari wote waliopo ndani na nje ya nchi wakubali kunyoosha na kupokea mkono wa Maridhiano. Tumeze machungu yanayotakana na Uchaguzi.. Historia yetu imejaa kila ina ya majeraha, ni wakati wa kuzika historia hiyo na kushikamana kuijenga Zanzibar yetu. Maridhiano ndiyo yatayofungua milango ya kuiwezesha Serikali kuchukua hatua za marekebisho na kujenga upya pale palipovunjwa, pale palipovurugwa, pale palipoharibika na pale palipokosewa.

Bila ya hatua hii, mageuzi tunayoyataka hayataweza kufanyika na kusimamiwa ipasavyo kwa kiwango cha kukidhi matarajio ya wananchi.  Na sisi viongozi tuonyeshe njia kwa wananchi wetu kwa kutibu majeraha haya kwa waathirika kwa kuwaonyesha kwa vitendo kwamba tunayo nia ya dhati ya maridhiano ili tujenge Zanzibar moja, Zanzibar yenye kuheshimu haki na kulinda misingi ya kidemokrasi tuliyojiwekea.

Mungu Ibariki Zanzibar!

Ahasanteni kwa kunisikiliza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!