Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Askofu Bagonza: Ni Mungu tu asiyekosea
Habari za Siasa

Askofu Bagonza: Ni Mungu tu asiyekosea

Askofu Benson Kagonza, KKKT Dayosisi ya Karagwe
Spread the love

UMMA na mataifa huongozwa na wanadamu. Sifa kuu ya mwanadamu ni kukosea au kuishi katika uwezekano wa kufanya makosa. Anaandika Mwandishi Maalum … (endelea)

Dawa ya kumsaidia mwanadamu mwenye uwezo wa kufanya makosa katika utendaji wake si kumpa kinga ya kutoshtakiwa kwa makosa aliyoyafanya. Ziko njia tatu kuu kati ya nyingi:

  1. Kumsamehe anapofanya makosa. Aweza kutubu mwenyewe au hata kusamehewa bila kudaiwa kutubu. Hii ni njia ya kidini zaidi.
  2. Kumnunulia bima ya kufidia makosa yake (Insurance for Malpractice). Hii inatumika katika sekta za kazi zote zinazogusa maisha ya watu binafsi. Bima hutumika kulipa fidia au faini endapo mtu au kundi limeathirika kwa makosa ya mtendaji.
  3. Kuwajibika kwa niaba ya chombo (Vicarious liability). Hii ni pale makosa ya mtendaji yanafunikwa au kuwajibisha chombo alichokiwakilisha wakati anatenda makosa hayo. Hii haihusishi makosa ya kijinai mathalani mtu hawezi kuiba, kubaka, kuua kwa niaba ya chombo.

Kwa yote matatu, mtendaji kama mtu binafsi bado anabaki peke yake anapofanya makosa ya kijinai.

Ili kupunguza matumizi mabaya ya kinga, idadi ya wenye kinga serikalini kila wakati hupungua kuliko kuongezeka.

Katika mifumo ya kidola, kinga ya kudumu kwa watendaji ni uwepo wa kanuni za Kukaguana (checks and balances), Kusimamiana (Oversight), na Demokrasia (Mamlaka itokayo kwa wananchi).

Haya yakifanyika, huwafanya watendaji kuwaogopa, kuwaheshimu na kuwatumikia wananchi. Yasipofanyika, wananchi huwaogopa, hulazimishwa kuwaheshimu na kulazimika kuwatumikia watendaji.

Katika karne ya 15 na 16, kulikuwa na mjadala mkali kuhusu uwezekano wa viongozi wa kanisa kutofanya makosa (infallibility). Mjadala uligonga ukuta, kanisa likagawanyika.

Kumbukumbu chungu ingalipo kwa sababu hata serikali kama taasisi, kanisa kama taasisi na bunge kama taasisi vinaweza kufanya makosa, sembuse mtu binafsi?

Muswada wa kuongeza idadi ya wenye kinga ni “karibu mno” na kumkosea Mungu.

Rais John Magufuli

Kinga inaondoa ubinadamu na kuwavika wenye kinga “Umungu bandia.” Wananchi walichagua wanadamu, wanapenda kutumikiwa na wanadamu. Mungu tunaye mmoja na ni yeye asiyefanya makosa

Njia iendayo Jehanamu imejaa nia njema. Yawezekana ipo nia njema katika muswada huu kama mimi ninavyojifikiria nina nia njema kuyasema haya.

Nani mwamuzi wa haki katika jambo hili? Mambo ya haki na dhamiri hayaamuliwi kwa wingi wa kura kwa sababu yana mizizi ya imani. Uhai wa taifa letu huru zaidi ya nusu karne, tumekuwa na kinga ya mtu mmoja na ilitosha.

Kwa uchache, kinga ya watajwa wote katika muswada inawafanya hao kuwa juu ya vyombo wanavyoviongoza. Watu hawawezi kuwa bora kuliko vyombo tukawa salama. Tusifunike shimo kwa kuchimba jingine

Chombezo

Nimejulishwa na mtu aliye ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali kuwa, muswada huu si juu ya kinga kwa watendaji wakuu bali unahusu njia za kufuata ili kuwashtaki. Bado nasimamia mawili:

  1. Njia za kuwashtaki zinatakiwa ziwe rahisi zaidi kuliko kufanywa ngumu. Ni watumishi, si mabwana wa wananchi.
  2. Iwe kinga au njia za kuwashtaki, bado ni muhimu kutambua kuwa ni wanadamu. Wanafanya makosa. Na njia za kuwakinga au kuwashtaki zitoke kwa wananchi, si wao wenyewe. Yaani makosa wafanye wao, kinga wajipangie, na njia ya kushtakiwa waamue wao?! Haifai.

Mwandishi ameandika uchambuzi huu, kipindi ambacho kuna Muswada umepelekwa bungeni pamoja na mambo mengine, unazuia Rais, Spika, Jaji Mkuu, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu kushtakiwa mahakamani.

Muswada huo unatarajiwa kupitishwa katika mkutano huu wa 19 wa Bunge unaoendelea jijini Dodoma huku ukipingwa na makundi mbalimbali ya wanasiasa, wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu. 

Mwandishi ni Benson Bagonza, Askofu wa Kanisa la Kiijini la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!