Saturday , 27 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Lugola awafyeka Ma-RPC watatu, wengine wanafuata
Habari Mchanganyiko

Lugola awafyeka Ma-RPC watatu, wengine wanafuata

Kangi Lugola Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
Spread the love

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola jana ametangaza kutengua uteuzi wa Wakuu wa Polisi wa Mikoa (Ma-RPC) watatu kwa sababu tofauti. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Katika Ma-RPC hao waliotenguliwa wawili ni kukaidi maagizo aliyoyatoa ya kuvyeka vichaka vya rushwa na mmoja kujihusisha na kuwalinda wauzaji wa madawa ya kulevya na kuwasindikiza wafanyabiashara wa magendo.

Kangi alitoa taarifa hiyo ya kutengua uteuzi wa Ma RPC hao kutokana na kushindwa kufanya kazi zao kwa misingi ya maadili huku akisema kuwa wapo baadhi ya Ma RPC ambao wamekuwa wakibeza maagizo ambayo anayatoa kwa madai kuwa ni maagizo ya kisiasa.

Alitaja waliotenguliwa nafasi zao kuwa ni RPC wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Salum Hamdun, RPC wa mkoa wa kipolisi Temeke, Emmanuel Lakula na mkuu wa polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhan Nganzi.

Alisema kuwa hao wakuu wa polisi katika mikoa ya kipolisi wameshindwa kutekeleza maagizo aliyoyatoa kwa wakuu wa polisi mikoa yote ambayo yalikuwa yakilenga kufyeka vichaka ambavyo vinatumika kuwaficha maaskari wanaopenda kula rushwa na kuwakingia kifua wahalifu.

Pia alisema kuwa amelazimika kutengua uteuzi wa Kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha kutokana na kitendo cha kumnyanyasa askari mdogo ambaye alitoa majina ya baadhi ya maaskari ambao wanatumika katika kuwalinda wafanyabiashara wa madawa ya kulevya na kuwasindikiza wafanyabiashara za magendo.

Katika hatua nyingine Kangi amesema kuwa amemwagiza mkuu wa kitengo cha usalama barabarani kujitafakari na kujitathimini kama anatosha kuendelea kuwa katika nafasi hiyo kutokana na kushindwa kusimamia na kuzuia vitendo vya rushwa ambavyo vinafanywa na baadhi ya askari wa usalama barabarani.

Waziri huyo alisema kuwa yeye aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, tarehe 2 Julai, 2018 na alimuahidi rais Dk. John Magufuli kuwa kamwe hatamwangusha katika kutekeleza maagizo yake ikiwa ni pamoja na kusimamia Ilani ya CCM.

“Kutokana na hali hiyo nilianza kufanya kazi kwa kuzunguka mikoa mbalimbali na kuzungumza na wakuu wa polisi wa Mikoa, OCD na Ma-RTO ili kuhakikisha wanafanyakazi kwa misingi ya kuhakikisha mtanzania masikini anaishi bila kusumbuliwa.

“Kazi kubwa ya Jeshi la Polisi ni kuhakikisha usalama wa raia na mali zake unalindwa, huku amani  na utulivu vikitawala, lakini niliweza kubaini kuwa yapo mambo mbalimbali ambayo yanawakwaza watanzania kutokana na kuwepo kwa baadhi ya askari ndani ya Jeshi la Polisi wanakuwa wanaenda kinyume na utendaji wa kazi.

“Baadhi ya maelekezo niliyotoa kwa wakuu hao ni pamoja na kuepukana na tabia ya baadhi ya askari kuwabambikia kesi watuhumiwa, ucheleweshaji na visingizio katika utoaji wa dhamana jambo ambalo limepelekea kuwepo kwa msamihati unaosemwa kuwa kuingia polisi bure kutoka hela.

“Katika utoaji wa dhamana kumekuwepo na mianya mingi ya kutafuta rushwa ikiwa ni pamoja na askari kudai kuwa dhamana haitolewi usiku, haitolewi siku za Jumamosi na Jumapili au siku za sikukuu jambo ambalo limekuwa likisababisha rushwa kutolewa hasa pale inapofikia mwishoni mwa wiki na hivyo ndivyo vichaka ambavyo nilitaka vifyekwe,” alisema Kangi.

Hata hivyo alisema kuwa kutokana na maagizo hayo wapo baadhi ya wakuu wa polisi wa mikoa ambao walibeza maagizo hayo na kusema kuwa maagizo hayo ni ya kisiasa hivyo anayoyatoa ni mwanasiasa na ataondoka madarakani na kuwaacha wakuu hao wa polisi.

Kangi alisema kutokana na baadhi ya wakuu hao kubeza sasa ameanza kuonesha kuwa maagizo hayo siyo ya kisiasa bali yanatakiwa kufanyiwa kazi kwa misingi ya kuendelea kujenga imani kwa wananchi juu ya utendaji wa Jeshi la Polisi.

Alisema kwa kutuma salamu kwa baadhi ya wakuu wa polisi wa mikoa ambao wanabeza maagizo hayo ameanza kutuma salamu kwa kuwaondoa Ma-RPC hao watatu na wengine watafuata.

Katika hatua nyingine Lugila alisema kuwa katika kikosi cha usalama barabarani kuna maonevu makubwa na ubambikwaji wa makosa lukuki ambayo hayapo kisheria.

Alisema kuwa wapo askari ambao wamekuwa wakifuata pikipiki majumbani kwa watu au minadani na kuanza kuwauliza maswali na kutaka walipe faini jambo ambali alisema haliwezi kuvumilika na kutaka kukomeshwa mara moja.

Alisema sheria namba 39 kifungu cha 168 inatambua ubovu wa gari na kwa kutumia sheria hiyo hata kama gari itakuwa na makosa 30 askari wa usalama wa barabarani anatakiwa kuandika kosa moja tu ambalo linahusu ubovu wa gari na siyo kuandika makosa lundo kama inavyofanyika sasa.

Aidha alisema kuwa amemwagiza Katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuunda kamati ambayo itafanya kazi kwa miezi mitatu na kumpatia taarifa na iwapo atabaini kuwa kuna sehemu ambayo haifanyi vizuri hatua stahiki zitachukuliwa.

Pamoja na mambo mengine Kangi alisema kuwa anayo mamlaka ya kutengua uteuzi wa Ma RPC na kumwachia IGP kufanya uteuzi mpya.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Wakili: Ukimpa zawadi mwenza marufuku kumpora hata mkiachana

Spread the love  WANANDOA na watu waliko kwenye mahusiano ya kimapenzi, wamekumbushwa...

Habari Mchanganyiko

Majaliwa: Mvua zimesababisha vifo vya watu 155, kuendelea hadi Mei

Spread the love  WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mvua kubwa za El-Nino...

Habari Mchanganyiko

Exim Bank yatoa  vitanda kwa shule ya Jeshi la Polisi Moshi

Spread the love  BENKI ya Exim imekabidhii  seti ya vitanda kwa Shule...

Habari Mchanganyiko

NBC yakabidhi vitanda Shule ya Polisi Moshi

Spread the loveBenki ya NBC imekabidhi msaada wa vitanda 28 kwa Shule...

error: Content is protected !!