Hakimu wa Nondo agoma kujitoa

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi mkoa wa Iringa imekataa ombi la Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo la kukataa kuendelea usikilizwaji wa kesi yake mbele ya  Hakimu John Mpitanjia. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Nondo anayeshtakiwa mahakamani hapo kwa tuhuma za kudaiwa   kujiteka na kusambaza taarifa za uongo katika mitandao ya kijamii, alimkataa Hakimu Mpitanjia kwa madai ya kutokuwa na imani naye.

Hakimu Mpitanjia amegoma kujitoa katika kesi hiyo kutokana na  sababu za kumkataa ni za kufikirika na hazina mashiko.

Nondo aliwasilisha maombi ya kumkataa Hakimu huyo juzi kwa njia ya barua kwa kile alichoeleza kuwa hana imani na hakimu huyo ikiwa pamoja na sababu ya ukaribu wa hakimu huyo na Mkuu wa upelelezi wa jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa.

Akitoa uamuzi huo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa,  Hakimu Mpitanjia amesema sababu alizotoa mshtakiwa hazina msingi wowote na ataendelea kusikiliza shauri hilo kwani akijitoa haki itachelewa.

“Sababu walizotoa upande wa utetezi ni za kufikirika ambazo hazina ushahidi wowote na kwa kuwa mahakama ni chombo cha mwisho katika kutenda haki na kuwahisha haki, nitaendelea kusikiliza shauri hili ili niwahishe haki ya mshtakiwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Hakimu Mpitanjia.

Jebra Kambole, wakili wa Nondo akizungumzia uamuzi huo amesema upande wa utetezi wamepokea uamuzi wa mahakama na hawawezi kuupinga ila kama kutakuwa kuna ulazima wa kufanya jambo lolote la kisheria watatumia njia nyingine za kupata haki yao.

“Kwa sasa tunaona shauri liendelee tu ili mshtakiwa aendelee na mambo mengine, kama anafungwa afungwe na kama anaachiwa aachiwe akaendelee na shule,” amesema Kambole.

Wakulima Morogoro watoa kilio chao kwa Serikali

WAKULIMA wadogo mkoani Morogoro wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuyashauri makampuni ya mbolea kupunguza kipimo cha mifuko ya mbolea ambacho watamudu kununua ili kuwawezesha kulima kilimo chenye ubora. Anaripoti Christina Haule … (endelea).

Wakulima hao wameomba Serikali kuzungumza na makampuni hayo ya mbolea ikiwezekana wafunge mifuko ya kila 10 ya mbolea badala ya ile ya kilo 50 kama iliyozoeleka na makampuni hayo.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mkulima kutoka kata ya Kibati wilayani Mvomero mkoani hapa, Anna Mushi amesema kilimo kwa wakulima wadogo kimekuwa kigumu kutokana na mbolea ya kupandia na ya kukuzia kuuzwa kwa bei ya juu.

Aidha amesema katika msimu wa mwaka jana walifanikiwa kuvuna mazao ya kutosha kutokana na kupata mbolea katika ujazo wa hadi kuanzia kg 5 za kupima ambapo mpango ulioletwa na Serikali kwa sasa umewafanya mahindi yao kutoonekana kukua vizuri baada ya mengi ya mahindi shambani kuwa ya rangi ya njano huku yakiwa hayajabeba vizuri.

Amesema, akiwa mkulima wa heka moja katika msimu wa kilimo wa mwaka jana alifanikiwa kuvuna magunia 15 yanayomsaidia hadi sasa kwa chakula na kujikimu na familia yake baada ya kuweka mbolea aliyoipata kwa bei rahisi lakini kwa mwaka huu ameshindwa kutokana na kupanda kwa bei ya mbolea.

Naye  mmoja wa wauzaji pembejeo za kilimo kwa bei ya jumla na rejareja mkoani hapa, Mkurugenzi wa Kampuni ya ETG Inputs Ltd, Pratik Patel amewashauri wakulima kufuata ushauri wa wataalamu wakati wa kununua madawa ya kuulia wadudu pindi mazao yao yanaposhambuliwa na wadudu shambani  ili waweze kuokoa mazao na kuzalisha kwa tija.

Patel amesema kuwa wakulima wamekuwa wakipata hasara pindi kunapotokea mlipuko wa magonjwa katika mazao kutokana na kushindwa kunununua madawa sahihi ya kuuwa wadudu kutoka kwenye maduka ama makampuni yaliyosajiliwa .

Amesema kwa sasa wanauza mbolea kwa kufuata bei elekezi iliyotolewa na Serikali ambayo kwa mfuko wa kg 50 wanauza kwa sh 51,300 kwa mbolea ya kukuzia wakati hapo nyuma waliuza kwa sh 38,000 hadi 40,000.

Patel amesema, ni vema serikali ikapunguza gharama hizo za uuzaji wa mbolea ili wakulima wa hali ya chini waweze kununua kwa rejareja na kuweza kupata .

“Serikali ione ni namna gani ya kuwasaidia wakulima wa hali ya chini ili waweze kupata mbolea kwa rejareja kwa kuruhusu hata kuanzia kilo tano kwani ndio kundi kubwa la wakulima hasa wadogo walipo” amesema Patel.

Amesema wakulima wadogo kushindwa kumudu gharama za kununua mbolea ukilinganisha na wale wenye mashamba nakubwa imetokana na gharama kubwa ya mbolea iliyopo kwa sasa baada ya kupanda ukilinganisha na kipindi cha mwaka Jana.

Hata hivyo aliwashauri wakulima wadogo hasa wa majumbani kujenga utamaduni wa kununua madawa ya wadudu waharibifu wa mazao yakiwemo ya jamii ya mikunde kufuatia wakulima wengi kudai kutopata mazao hayo kwa mwaka huu.

Amesema madawa ya kuulia wadudu waharibifu yanapatikana kwenye maduka yaliyothibitishwa kwa bidhaa hizo kwa bei rahisi ambapo waone umuhimu wa kununua ili waweze kujikimu katika familia zao.

Bunge lamuweka rehani Waziri Tizeba

BAJETI ya Wizara ya Kilimo iliyowasilishwa bungeni mjini Dodoma jana Jumanne, ni mzigo kwa wananchi na imelenga kuwanyonya wakulima. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Akichangia mjadala wa bajeti ya wizara hiyo, mbunge wa Mbozi (Chadema), Pascal Haonga, ametuhumu serikali kunyonya wakulima na kupendelea wafanyabiashara.

“Hii serikali haina dira yeyote kwenye sekta ya kilimo. Haina mkakati wala mipango ya kusaidia wakulima. Kinachoonekana ni kwamba serikali imejipanga kupunja wakulima kupitia vyama vya ushirika,” ameeleza.

Amesema, “kuna watu wamefilisi vyama hivi vya ushirika, lakini hawajachukuliwa hatua. Leo serikali inafufua tena vyama hivi ambavyo vimekuwa mzigo kwa wananchi wetu bila kutuambia waliofilisi ushirika wamefanywa nini.”

Naye Nape Nnauye, mbunge wa Mtama (CCM), amedai kuwa bajeti hiyo haina jipya na hivyo inapaswa kuondolewa bungeni.

Amesema, “serikali isionea aibu kuiondoa bungeni bajeti ya wizara hii ili ikajipange upya. Hii bajeti itaiumiza wananchi wetu na hivyo kuiweka serikali ya chama changu kwenye wakati mgumu wa kujitetea.”

Nape amehoji mahali ambako mabilioni ya shilingi ambayo serikali imekuwa ikijigamba kuwa imekusanya yalikohifadhiwa.

Amesema, “umefika wakati wa kuelezana ukweli kuwa bajeti ya wizara hii ni ngumu na haiendani kabisa la Ilani ya uchaguzi ya CCM, ikipitishwa itakuwa mwiba kwa serikali. Namuonea huruma waziri wa kilimo, Dk. Charles Tizeba kwa kuwa kuna mambo yako nje ya uwezo wake, lakini kila jambo anabebeshwa yeye.”

Amesema, “bajeti inagusa asimilia 80 ya wananchi na inagusa maisha ya watu wetu. Serikali inajali maendeleo ya vitu au watu waliowaweka madarakani jambo ambalo majibu yake yatakuwa na maana tofauti kwa wananchi.”

Amesema serikali haiwajali wakulima kwa maelezo kuwa imekuwa ikipunguza bajeti hiyo kuanzia mwaka 2018/17.

“Wakati fulani tulisema Serikali ikwepe kuwekeza fedha nyingi kwenye miradi mikubwa inayoweza kujiendesha kibiashara, lakini tukashambuliwa kama si wazalendo katika nchi hii, na hili Tizeba tutakubebesha bure lakini si lako,” ameeleza Nape.

Amesema akikubali bajeti hiyo, wananchi wake wa Mtama na wakulima wa korosho, ufuta, pamba na mazao mengine nchini watamshangaa kwa kiasi kikubwa hivyo hakuna shida wala aibu kukaa pamoja na kuifumua kama ilivyowahi kufanyika kwa wizara nyingine.

Akizungumzia Ilani ya uchaguzi ya CCM, Nape ambaye aliwahi kuwa katibu mwenezi wa chama hicho amesema, “ilani ilitamka kuwa Serikali itakayoundwa itakuwa na jukumu la kuwasaidia wakulima kutafuta masoko ya nje lakini kwa sasa imekuwa kinyume kabisa na ilani hiyo, kwamba kukaa mezani ndio suluhu.

“Ukimwambia mtu akale magunia 20 ya mbaazi si unamtukana huyu, hivi tunawaambia nini wakulima katika jambo hili, ni kwa nini tusiwe wepesi wa kukubali ushauri na kuzungumza kwa pamoja. Naomba sana, bajeti hii iondolewe kwa kuwa haikidhi mahitaji ya sasa.”