October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zitto amtaka JPM urais 2020

Spread the love

ZITTO Kabwe ameeleza dhamira yake ya kutaka kupambana na Dk. John Magufuli, katika kugombea urais kwenye uchaguzi wa Oktoba mwaka huu. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Amesema, anatamani vyama vya upinzani vimuunge mkono kwenye uchaguzi huo ili akabiliano na Dk. Magufuli kama atateuliwa na chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – kugombea urais kwenye uchaguzi huo.

Zitto ambaye ni Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, ametoa kauli hiyo leo tarehe 18 Februari 2020, wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.

Amesema, katika mazingira ya sasa, ndoto yake hiyo itafanikiwa endapo vyama vya upinzani vitakubali kumuunga mkono katika harakati hiyo.

“Mimi kama Zitto nautaka urais kama chama kitakubali.  Lakini kwa mazingira ya Tanzania, lazima tuwe na mgombea anayeungwa na vyama vya upinzani, ukivuka kwenye chama chako, uanenda kwenye kigingi kingine. Kama vyama vikiona naweza kupeperusha bendera kwa niaba yao, sitakataa,” amesema Zitto.

Pia amesema, kama vyama vya siasa vya upinzani havitampa ridhaa ya kugombea nafasi hiyo, atatoa ushirikiano kwa mtu atakayeteuliwa kugombea urais katika uchaguzi huo.

“Lakini pili, wenzangu wakiona kuna mwanachama mwingine wa upinzani tunaona anafaa kubeba bendera na kugombea, mimi namuunga mkono,” amesema.

Mbunge huyo wa Kigoma Mjini amesema, ndoto yake ni kuiongoza Tanzania katika misingi ya haki, usawa na demokrasia.

“Mimi nina ndoto, ningependa siku moja kuongoza nchi yangu.  Kutenda haki, kuirudisha heshima ya Tanzania kimataifa.

“Kuona haki za binadamu zinaheshimiwa na si Tanzania ukigombana na viongozi unafunguliwa mashtaka ya utakatishaji fedha. Tuwe na uhuru wa mawazo na si hofu kama ilivyo sasa hivi,” amesema.

error: Content is protected !!