Sunday , 2 April 2023
Home Kitengo Michezo Yanga waanza kazi Ligi Kuu, yaichapa Mtibwa 2-1
Michezo

Yanga waanza kazi Ligi Kuu, yaichapa Mtibwa 2-1

Spread the love

YANGA SC imeanza vyema Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Ushindi huo wa pili mfululizo baada ya Jumapili kuichapa USM Alger 2-1 pia katika mchezo wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika unamaanisha Yanga si timu ya kubeza katika msimu mpya.

Mabao ya Yanga SC leo yalipatikana kipindi cha kwanza yote, yakifungwa na mshambuliaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Eritier Makambo na Nahodha Kelvin Yondan kwa penalti, wakati la Mtibwa lilifungwa na Haroun Chanongo.

Mtibwa Sugar waliuanza mchezo vizuri na kuutawala kwa takriban robo saa, kabla ya Yanga SC kuzinduka na kuanza kucheza vyema.

Makambo alifunga bao zuri dakika ya 23 kwa kichwa, lakini refa Meshack Suda wa Singida, aliyekuwa anasaidiwa na Sylvester Mwanga wa Kigoma na Geoffrey Msakila wa Geita akakataa bao hilo.

Wana Jangwani hao hawakukata tamaa na juhudi zao zikawalipa dakika ya 32, Makambo tena akifunga kwa kichwa tena akimalizia krosi ya beki wa kushoto Gardiel Michael.

Beki Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ akamuangusha mkongwe Mrisho Khalfan Ngassa kwenye boksi na Yondan akaenda kufunga kwa penalti dakika ya 40.

Kipindi cha pili Yanga SC walikianza vizuri tena na Makambo akapoteza nafasi mbili nzuri za kufunga akiwa amebaki na kipa Benedictor Tinocco, mara zote akikosa hesabu nzuri za kumchenga mlinda mlango huyo.

Na kiungo mshambuliaji wa zamani wa Simba, Chanongo akauwahi mpira uliopanguliwa na kipa Benno Kakolanya kuifungia bao pekee Mtibwa Sugar leo.

Bao hilo likawazindua Yanga na kuanza tena kupeleka mashambulizi langoni mwa Mtibwa Sugar, lakini wakaishia kukosa mabao ya wazi.

Mechi nyingine za Ligi Kuu leo; Stand United imeichapa 1-0 African Lyon Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga wakati, KMV imelazimisha sare ya 0-0 na JKT Tanzania Uwanja wa Meja Isamuhuyo, Mbweni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Mchezo kati ya Azam FC na Mbeya City unaendelea Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam kukamilisha mechi za ufunguzi za Ligi Kuu zilizoanza jana. 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Michezo

TANROADS wawataka watumishi wazingatie michezo kazini

Spread the love  WAKALA wa barabara Tanzania (TANROADS) imesema michezo inapaswa kuzingatiwa...

Michezo

Yanga: Fedha za Rais Samia zinaleta ari kubwa

Spread the loveUONGOZI wa klabu ya Yanga, umesema fedha zinazotolewa na Rais...

Michezo

Simba Sc. yamvulia kofia Rais Samia, yamuahidi makubwa dhidi ya Horoya

Spread the loveWAKATI timu ya Simba ikiibuka na ushindi wa bao 3-0...

Michezo

Taasisi ya TKO na TFF yawapiga msasa makocha wa kike 54

Spread the love WAKATI Soka la wasichana likichipua kwa kasi Taasisi ya...

error: Content is protected !!