May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Yanga taamu! Yairarua KMC mbele ya JK

Spread the love

VIGOGO – Yanga wameendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuizabua Klabu ya KMC mabao 2-0 usiku huu Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Katika mchezo huo uliohudhuriwa na Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ulikwenda sambamba na kusherehekea mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo tarehe 19 Machi, mwaka jana.

Bao la kwanza la Yanga lilitiwa kimyani na beki wa zamani wa timu hiyo, Andrew Vincent ‘Dante’ aliyejifunga dakika ya 39 katika harakati za kuokoa mpira uliounganishwa na mshambuliaji Mkongomani, Fiston Kalala Mayele.

Mayele alikuwa anaunganisha pasi ya kichwa iliyopigwa na Denis Nkane baada ya kupokea krosi maridhawa ya beki hatari Djuma Shaban

Bao la pili la Yanga lilifungwa na beki mkongomani, Djuma Shaban dakika ya 52, kwa kichwa maridadi ‘free header’ wakati akiunganisha kona iliyochongwa Chico Ushindi kuelekezwa katika lango la KMC.

Kwa ushindi huo, Yanga wanafikisha pointi 48 katika mchezo wa 18 na kuendelea kuongoza ligi kwa pointi 11 zaidi ya  mabingwa watetezi, Simba ambao wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi 37 kwenye mechi 17 lakini wakiwa na mechi moja mkononi.

Pia Yanga wanaendeleza  ubabe wa kutopoteza mchezo wowote katika Ligi kuu ya NBC.

Aidha, kwa kichapo hicho KMC wamebaki na pointi zake 22 za mechi 18, nafasi ya saba.

error: Content is protected !!