July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ni mwaka mmoja wa uchumi bila vyuma kukaza

Spread the love

MWAKA mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani, unawezakuwa ni mwaka wa uchumi ambao hauhitaji sana takwimu kuelezea ukuaji wake, bali ni kwa kuangalia  maisha mtaani yalivyo rahisi tofauti na ilivyokuwa kwa miaka mitano ya nyuma. Inachambua Mwanahalisi Online…(endelea)

Ni kwa mwaka mmoja tu, imetosha kusahaulisha watu misemo kama “vyuma vimekaza”  “tufunge mkanda” . Ni mwaka ambao ukimwambia mtu uchumi wa Tanzania umekuwa kwa asilimia 4.9 tu, anaweza kushindwa kutofautisha na ule ukuaji wa asilimia 7 ya miaka ya nyuma.

Uchumi wa Tanzania umeongezeka kwa asilimia 0.1 baada ya kukua kwa asilimia 4.9 katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2021 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2020. Ni ongezeko dogo lakini lenye athari chanya kwa maisha ya watu.

Hali hii ina akisi kile kilichoelezwa na Rais Samia katika hotuba yake bungeni kuwa, anakwenda kufungua uchumi utakaogusa maisha ya mtu mmoja mmoja na sekta binafsi.

Mbali na kuwa uchumi wa watu zaidi kuliko takwimu, hata hivyo bado kwenye takwimu za viashiria vya ukuaji uchumi, Tanzania bado ipo sehemu salama licha ya athari za janga la virusi vya Uviko-19.

Mathalani katika kipindi cha mwaka mmoja,  ujazi wa fedha ulikua kwa wastani wa asilimia 10.2 mwaka 2021 ikilinganishwa na asilimia 8.8 mwaka 2020 huku riba ya mikopo ikipungua na kufikia wastani wa asilimia 16.59 mwaka 2021 ikilinganishwa na asilimia 16.66 mwaka 2020.

Aidha mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa asilimia 10 Desemba 2021 ikilinganishwa na asilimia 3.1 Desemba 2020 huku akiba ya fedha za kigeni ikiwa ni dola za Marekani bilioni 6.4 kufikia Desemba 2021 kiasi kinachotosheleza kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 6.6 ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 6.0 zilizotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 5.6 Desemba 2020.

Licha ya kuongezeka kwa mfumuko wa bei katika kipindi cha mwaka mmoja kutoka wastani wa asilimja 3.3 mwaka 2022 hadi wastani wa asilimia 4 katika kipindi cha Julai 2021 hadi Januari  2022.

Hata hivyo Waziri wa Fedha na mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, akiwasilisha mapendekezo ya serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2022/23 na mfumo na ukomo wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2022/23  Bungeni, alisema “hali ya mfumuko wa bei inayoendelea imechangiwa na sababu zilizo nje ya uwezo wa Serikali.”

Alizitaja sababu hizo kuwa ni kuvurugika kwa mnyororo wa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma katika soko la dunia kutokana na athari za UVIKO-19.

Aliongeza sababu nyingine ni kuongezeka kwa gharama za uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma katika soko la ndani hali ambayo alisema  imetokana na kuongezeka kwa bei na gharama za usafirishaji wa bidhaa na huduma kutoka nje, ikiwemo petroli, mafuta ya kula, mbolea, chuma na malighafi za viwandani.

Vilevile alitaja sababu zingine ni kuongezeka kwa mahitaji baadhi ya bidhaa na huduma na mwisho ni kupungua kwa upatikanaji wa mazao ya chakula katika baadhi ya masoko ya ndani.

Hata hivyo, alisema kiasi hicho cha ukuaji kipo  ndani ya lengo la kuwa na mfumuko wa bei usiozidi asimilia 5.0.

Sehemu nyingine ambayo Serikali ya Rais Samia imefanya vizuri ni mapendekezo ya kuongeza ukomo wa bajeti kufikia Sh.  41 Trilioni  zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika mwaka wa fedha 2022/2023, sawa na ongezeko la  asilimia 8.1  ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2021/22 ya Sh. 37.9 Trilioni.

Hii inaweza kuwa bajeti ya matumaini kwa watanzania kwani ongezeko lake limetokana na fedha ambazo zinakwenda kuwafikia watu moja kwa moja.

Kwa mujibu wa Dk. Nchemba bajeti hiyo imezingatia mahitaji ya Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ikijumuisha ulipaji wa deni la Serikali; mapendekezo ya mahitaji ya nyongeza ya mshahara, upandishwaji wa madaraja kwa watumishi wa umma; ajira mpya; sensa ya watu na makazi; na kugharamia miradi mikubwa ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa.

Jumla ya mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa sh 28.6 Trilioni, sawa na asilimia 69.9 ya bajeti yote. Hii inaonyesha ni jinsi gani Serikali inatarajia kuwa uzalishaji utaongezeka ambao pia utaleta ustawi wa jamii yake.

Kati ya mapato hayo, mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania yanakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 11.1 hadi sh 24.1 Trilioni kutoka makadirio ya sh 21.7 Trilioni mwaka 2021/22.

Mapato Yasiyo ya Kodi (Wizara, Idara, Taasisi na Mamlaka za Serikali za Mitaa) yanakadiriwa kuongezeka hadi sh 4.5 trilioni mwaka 2022/23 kutoka sh 3.9 trilioni mwaka 2021/22.

Hata hivyo changamoto kwa Serikali inaweza kuwa ni kuongezeka kwa deni la Serikali ambapo kwa kipindi cha mwaka mmoja limefikia Sh 68.5 Trilioni Desemba 2021 kutoka Sh 58.6 Trilioni mwaka 2020.

Katika kipindi hicho kuna ongezeko la Sh. Trilioni 10 sawa na ongezeko la asilimia 16.8.

Deni hilo liliongezeka kwa kasi kutokana na kupokelewa kwa mikopo kutoka vyanzo vyenye masharti nafuu na ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo. Mwaka ujao Serikali inatarajia kupata mikopo ya Sh. 4.1 trilioni kutoka kwa wadau wa maendeleo.

Miradi inayigharamwa na fedha hizo  ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme, elimu na afya.

Sababu nyingine iliyotajwa ya ongezeko hilo la deni ni kutolewa kwa hatifungani maalumu yenye thamani ya sh. 2.1 trilioni  kwa ajili ya kulipa deni la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

error: Content is protected !!