Klabu ya soka ya Yanga itazindua rasmi wiki ya Mwananchi visiwani Zanzibar Agost 22, mwaka huu, kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, kuelekea kilele cha Tamasha la siku ya mwananchi. Anaripoti Wiston Josia TUDARCo…(endelea)
Tamasha hilo litafanyika Agosti 29, 2021 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na MwanaHALISI Online, Afisa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Yanga, Hassan Bumbuli amesema kuwa uzinduzi wa wiki hiyo utafanyika Zanzibar na kuwataka mashabiki wa klabu hiyo kujiandaa kurudisha kwa jamii.
“Uzinduzi utafanyika Zanzibar Agosti 22, na mtaona nini kitakwenda kutokea, wanayanga wajiandae kwa kurudisha kwa jamii kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.” Alisema Afisa Habari huyo
Yanga watakwenda kufanya tamasha hili kwa mara ya tatu mfululizo, huku likitumika kama jukwaa la kuwatambulisha wachezaji wapya waliosajiliwa na klabu hiyo kwa msimu huu.
Aidha Bumbuli aliendelea kusema kuwa wao kama Yanga na kwa kushirikiana na wadhamini wao kampuni ya GSM, wamechangia kiasi cha shilingi 50 milioni kusaidia uwendeshaji wa Ligi visiwani Zanzibar katika hafla maalumu iliyoudhuliwa na makamu wa pili wa Rais visiwani humo Hemed Suleiman Abdulla.
“Yanga na GSM tumechangia Shilingi 50 milioni kusaidia uwendeshaji wa Ligi ya Zanzibar mbele ya makamu wa pili wa Rais.” Alinena Bumbuli
Katika hatua nyingine Afisa Habari huyo alizungumzia kuhusu maendeleo ya kambi ya timu hiyo nchini Morocco ambapo alisema kuwa, wachezaji wameshaanza mazoezi na suala la usajili limeshakamilika pamoja na kupata vibari vya uhamisho wao (ITC)
“Wachezaji wameshaanza mazoezi, na kuhusu usajili tumekamilisha usajili wa kimataifa na ITC zote zimekamilika isipokuwa ya Kharid Haucho ambaye klabu yake ilkuwa bado haijatoa ila ndani ya siku mbili yatakamilika.” Alifunguka kiongozi huyo
Leave a comment