WANAFUNZI wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini mkoani Dar es Salaam (TUDARCo) wameunga mkono juhudi za Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hasssan kwa kutembelea mapango ya Amboni yaliyopo mkoani Tanga kwa lengo la kujionea mambo mbalimbali na mengine yakiwa ya ajabu. Anaripoti Victoria Mwakisimba, TUDARCo … (endelea).
Rais Samia ambaye aliamua kutengenezwa na filamu ya utalii ya “The Tanzania Royal Tour” ikiwa na lengo la kuhamasika na utalii wa nje na ndani ya nchi ikiwemo kuzuru maeneo mbalimbali ya utalii na hata ya makumbusho ya kihistoria.
Wanafunzi hao wanaosomea shahada ya mawasiliano ya Umma katika chuo hicho wamechukua maamuzi hayo ya kutembelea mapango hayo ili kumuunga mkono Rais Samia na kuwa kama mfano kwa wanafunzi wengine kutembelea katika vivutio mbalimbali vya utalii nchini .
Mmoja kati ya waandishi waliotembelea mapango hayo, Isack Yohana alisema; “Wengi wetu ikiwa ni mara ya kwanza kutembelea mapango ya Amboni tumejionea mambo ya ajabu ambayo tungesimuliwa tungedhani hayana ukweli wowote.
“Tumeonyeshwa njia mbili moja ikiwa ni ya mizimu na nyingine ikiitwa njia ya uzima, lakini pia tumeona mapango yenye picha ya bikira Maria. Kwetu hiki ni kitu kikubwa sana kwani tumepata ushuhuda ambao umeongeza kitu katika elimu yetu.”
Alisema ndani ya mapango ya Amboni kuna vitu vingi vinavyoibua udadisi na vinavutia, ikiwemo njia ya uzima ambayo ni nyembamba lakini mtu hata akiwa mnene sana anapita bila shida.
Kwa upande wake, Abraham Manfred alisema kutokana na umbo lake la unene aliamini hawezi kupita katika njia ya uzima lakini alistahajabu alivyoweza kupita katika njia hiyo.
“Mwongozaji alipotoa maelekezo nilihisi haikuwa kweli lakini niliweza kupita kwenye njia hiyo nyembamba bila shida yoyote wala kukwama mpaka mwisho,” alisema Abraham.
Maajabu mengine ambayo yapo katika mapango ya Amboni ni uwepo wa giza nene kiasi hata watu wakiwa wawili wameshikana mikono bila taa hawawezi kuonana na hata wakivaa nguo nyeupe bado hawawezi kuonekana bila mwanga wa taa.
Aidha kuna jumla ya mapango saba lakini waongozaji wamepewa ruhusa ya kuwaonyesha watalii mapango manne tu.
Ni wakati wa watanzania kuamka sasa na kulitangaza taifa kimataifa na kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kukuza sekta ya utalii.
Leave a comment