October 21, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wadau wanolewa matumizi sahihi ya mitandao

Spread the love

 

SHIRIKA lisilo la kiserikali, linaloshughulika na masuala ya utetezi wa haki za kidigitali, Zaina Foundation, likishirikiana na Shirika la Haki Maendeleo, limewanoa wadau kuhusu matumizi sahihi ya mitandao, kwenye ukuzaji uchumi wa Watanzania. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mashirika hayo yameendesha mafunzo ya siku tatu, kuanzia tarehe 28 hadi 30 Septemba 2021, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Jukwaa la Uhuru wa Mtandao Afrika (FIFA21).

Lililoandaliwa na Taasisi inayoshughulika na Sera za Teknonolojia, Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Afrika Mashariki na Kusini (CIPESA).

Katika mafunzo hayo ya siku tatu, wadau hao walifundishwa kuhusu sheria, kanuni na miongozo inayosimamia matumizi ya mtandao na haki za kidigitali, kimataifa, kikanda na kitaifa.

Mafunzo hayo yalifunguliwa rasmi na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania (THBUB), Nyanda Shuli.

Akizungumza wakati anafungua mafunzo hayo, Shuli amesema yamekuja katika wakati sahihi ambapo Tanzania inashuhudia ongezeko la matumizi ya mtandao, ikiwemo katika masuala ya kiuchumi, biashara na kijamii.

“ Mafunzo haya yamekuja katika wakati sahihi, ambapo Serikali ya Tanzania inaingia kwenye mageuzi ya matumizi ya mtandao, kwa kuwa watu wengi wanatumia mtandao,” amesema Shuli.

Kamishna huyo wa haki za binadamu, amesema Serikali ya Tanzania inaendelea kurekebisha mazingira ya upatikanaji wa haki za kidigitali, ikiwemo kwa kuanzisha kituo cha Teknonolojia, Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Shuli amewataka wadau waliohudhuria mafunzo hayo, kutoa maazimio na mapendekezo yatakayoisaidia Serikali kuboresha zaidi huduma za mtandaoni.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Haki Maendeleo, Wilfredy Warioba, amesema wameandaa mafunzo hayo ili kutoa elimu kwa wadau hao, ambao watakuwa mabalozi wazuri wa kuielemisha jamii juu ya matumizi sahihi ya mtandaoni.

“Shughuli nyingi zimehamia kwenye mtandao, maisha mengi ya watoto wetu yanafanyika mtandaoni, badala ya wananchi kuwa nyuma katika mageuzi haya, tumeona bora kuweka chachu kuhakikisha wanakuwa na uelewa kuhusu masuala ya mtandao na wajibu wao,” amesema Warioba.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika Lisilo la Kiserikali la Human Dignity and Enviromental Care Foundation (HUDEFO), Sara Pima, amesema mafunzo hayo yamewasaidia kujua mipaka ya matumizi ya mitandao.

“Tuko kwenye maunzo haya kuhusu haki za kidigitali ili tuweze kuelewa na kuyatumia kuifundisha jamii kujua haki zetu ni zipi, vitu gani tufanye na vipi tusifanye ili tupate uhuru wa habari,” amesema Pima.

Jukwaa hilo la FIFA21, linafanyika mtandaoni ambapo wadau mbalimbali kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s), barani Afrika, wanapewa mafunzo pamoja na kujadili juu ya namna bora ya matumizi ya mtandao.

Miongoni mwa mambo yanayojadiliwa katika jukwaa hilo, ni kanuni za TEHAMA na haki za kupata taarifa, sheria na miongozo inayosimamia teknolojia hizo.

error: Content is protected !!