October 21, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia aitembelea LSF

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametembelea banda la Shirika Lisilo la Kiserikali, linaloshughulika na masuala ya msaada wa kisheria, Legal Service Facility (LSF), kwa ajili ya kuangalia huduma zinazotolewa na shirika hilo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Rais Samia ameitembelea LSF, katika mkutano wa mwaka wa Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s), uliofanyika kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma, leo Alhamisi, tarehe 30 Septemba 2021.

Baada ya kutembelea banda hilo, Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala, alimuelezea Rais Samia namna programu ya upatikanaji haki iliyozinduliwa na shirika hilo hivi karibuni, linavyofanya kazi.

Programu hiyo ilizinduliwa tarehe 20 Agosti 2021, jijini Dar es Salaam na Msajili wa NGO’s nchini Tanzania, Vickness Mayao.

Akielezea utekelezwaji wa programu hiyo, Ng’wanakilala amesema utatekelezwa kwa vipaumbele vinne, cha kwanza ni upatikanaji wa huduma bora za msaada wa kisheria, wakati cha pili kikiwa ni kujenga uelewa kwa jamii juu ya sheria na haki zao.

Ng’wanakilala amesema kipaumbele cha tatu, ni uboreshwaji mazingira endelevu ya upatikanaji wa haki, huku cha mwisho kikiwa ni uimarishwaji wa taasisi na sekta ya msaada wa kisheria.

Afisa Mtendaji huyo wa LSF, amesema programu hiyo itaendeshwa nchi nzima, Tanzania Bara na Visiwani, hasa kwa wananchi waishio pembezoni mwa miji.

error: Content is protected !!