October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Majaliwa asimulia Ole Nasha alivyofikwa na mauti

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amesema kifo cha aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, William Tate Ole Nasha, kilichotokea tarehe usiku wa tarehe 27 Septemba 2021, kilikuwa cha dharura. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endele).

Majaliwa amesema hayo leo Alhamisi, tarehe 30 Septemba 2021, katika shughuli ya kuuaga mwili wa Ole Nasha, iliyofanyika katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma na kuongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, pamoja na viongozi wengine wa Serikali na Bunge.

“Kifo hiki ni cha dharura na mapokeo yake ni ya uchungu mkubwa, kwetu tuliyekuwa tunafanya kazi naye,” amesema Majaliwa.

Majaliwa amesema kifo hicho kilikuwa cha dharura kwa kuwa mchana kutwa alishinda salama, ambapo alisafiri kutoka Arusha kwenda Dodoma kikazi.

“Tulipokea taarifa ya kifo hiki kwa huzuni kubwa, sababu mchana kutwa alikuwa safarini kutoka Arusha kuja Dodoma kikazi na hata alipofika Dodoma saa 11 jioni, bado alikuwa anashirikiana na wenzake kwenye maeneo mbalimbali,” amesema Majaliwa.

Amesema, baada ya marehemu Ole Nasha kuwasili Dodoma, alipata chakula maeneo mbalimbali, kisha alirudi nyumbani kwake majira ya saa 2.00 usiku salama, lakini alishindwa kupanda ghorofa ya tatu ili kwenda ndani kwake.

“Taarifa ambazo tumezipata, dereva aliyekuwa anamuendesha alieleza alimuacha nyumbani salama na dereva kwenda kupumzika, lakini baadae jirani wa marehemu alionesha marehemu alikuwa anapata chakula maeneo mbalimbali,” amesema Majaliwa.

Waziri Majaliwa amesema “na aliporudi nyumbani saa 2 usiku alishuka salama, alikuwa anapanda kwenye ghorofa yake ya tatu akaishia ghorofa ya pili akashindwa kuendelea, jirani mmoja alipokuwa anashuka akamuomba msadaa.”

Waziri Majaliwa amesema, Ole Nasha alikwama katika ghorofa ya pili, ndipo jirani yake aliyekua anashuka chini alimkuta na kumsaidia kumfikisha ndani kwake kwa ajili ya taratibu za kumpeleka hospitali, lakini isivyo bahati alipoteza maisha.

“Alimpeleka chumbani, basi akiwa anatafakari namna ya kufanya Mungu akamchukua, waziri wa afya alileta gari lakini alimbeba akiwa ametangulia mbele ya haki,” amesema Waziri Majaliwa.

Mwili wa Ole Nasha ambaye pia alikuwa Mbunge wa Ngorongoro (CCM), unatarajiwa kuzikwa kijijini kwao Ngorongoro mkoani Arusha, Jumamosi ya tarehe 2 Oktoba 2021.

error: Content is protected !!