November 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wadau wa misitu wataka mabadiliko ya sheria ya misitu

Spread the love

WADAU wa misitu wameomba mabadiliko ya Sheria na Sera za misitu ili ziwekwe vizuri, kusaidia kuondoa uharibifu wa misitu nchini. Anaripoti Christina Haule, Tanga … (endelea).

Mratibu wa Programu ya Kuendeleza Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC) Kitaifa, Emmanuel Msofe alisema hayo katika mafunzo ya waandishi wa Habari kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania yaliyofanyika jijini Tanga.

Msofe ambaye pia ni Afisa Misitu Mwandamizi kutoka Wizara ya maliasili na utalii alisema, kwa sasa sheria na sera za misitu zilizopo ni za muda mrefu na kwamba zinaendelea kufanyiwa marekebisho ili ziendane na hali halisi iliyopo.

Alitolea mfano sera ya misitu ya mwaka 1953 ambayo ni ya kwanza na ilifanyiwa marekebisho mwaka 1998 lakini bado haijakidhi mahitaji ya misitu kwa jamii na hivyo inaendelea kurekebishwa na kuletwa tena kwa ajili ya maendeleo kwa wananchi.

Alisema, kuboreshwa kwa sheria na sera za misitu zilizopo kutasaidia jamii inayoishi pembezoni mwa misitu kuona faida ya msitu kiuchumi, na kimaendeleo na hivyo kuendeleza utunzaji wa misitu.

Aidha alisema, karibu hekari milioni 2.4 sawa na asilimia 5 za ardhi ya jumla zilizopo nchini zipo hatarini kutoweka ikiwa hakutakuwa na nguvu kubwa ya uhifadhi wa misitu.

Msofe alisema, ardhi hiyo ya jumla ipo hatarini kutoweka kufuatia kuwa na misitu aina ya miombo (mataji wazi) huku ikiwa katika eneo kubwa la nchi ambayo hutumiwa zaidi na jamii katika matumizi mbalimbali ikiwemo ya nishati majumbani kama vile mkaa na kuni.

Alisema, Programu ya FORVAC inatekelezwa katika Halmashaui 10 nchini ambazo zimetengwa katika Kongani tatu zilizopo katika mikoa ya Tanga ni Halmashauri za Kilindi, Handeni na Mpwapwa ambayo imeongezewa ikitokea mkoani Dodoma, Kongano ya Lindi- ni Halmashauri za Liwale, Nachingwea na Ruangwa na Ruvuma- Songea, Namtumbo, Mbinga na Nyasa Programu ambayo ilianza mwaka 2018 na inatarajiwa kuisha mwaka 2022.

Naye Mratibu wa FORVAC Kongani ya jijini ya Tanga, Petro Masorwa alisema, lengo kuu la Program ya FORVAC ni kuongeza faida za msitu kiuchumi, kijamii na kimazingira kufuatia Sekta ya misitu kuwa ndio Sekta inayobeba vitu vingi inayopaswa kufuatiliwa na kulindwa kwa ukaribu.

error: Content is protected !!