Friday , 26 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Vilio vyakwamisha wasemaji msiba wa Prof. Ngowi
Habari Mchanganyiko

Vilio vyakwamisha wasemaji msiba wa Prof. Ngowi

Spread the love

VILIO vya uchungu vimesababisha baadhi ya wasemaji katika ibada ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Profesa Mshiriki wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Prosper Honest Ngowi na wa dereva wake, Innocent Mringo, kukwama kuzungumza kwa muda.Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Tukio hilo limetokea leo Ijumaa, tarehe 31 Machi 2022, katika ibada iliyofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam, iliyoendeshwa na na Baba Paroko wa Kanisa la Romani Katholiki la St. Peter’s, Stephen Kaombe na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Tabata Kuu, Kaanasia Msangi.

Miongoni mwa wasemaji waliokwama kuzungumza kwa sababu ya kulia, ni mtoto wa marehemu Prof. Ngowi, Nana Ngowi, ambaye kina mama wawili walipanda jukwaani kumshikilia na kumbembeleza, baada ya kukosa nguvu wakati akitoa shukrani za familia yake.

Kina mama hao walipanda jukwaani kumshikilia Nana, baada ya kusimama kuzungumza kwa sekunde kadhaa, wakati akitoa shukrani za familia yake, ikiwa ni dakika moja baada ya kuanza zoezi hilo.

“Tunapenda kutoa shukrani zetu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Chuo Kikuu cha Mzumbe na Watanzania wote kwa kutufariji katika kipindi kichungu kwetu. Marehemu baba yangu alikuwa mchapa kazi hodari katika kuleta maendeleo nchini,” amesema Nana.

Mtoto huyo wa pili wa Prof. Ngowi, amesema baba yake ameacha watoto watatu, ambapo wa kwanza ni Alpha na wa mwisho ni Omega, pamoja na mama yao, Bahati.

“Baba yetu alipenda tutimize ndoto zetu na tutazitimiza na kuitumikia Tanzania, kama baba yetu alivyofanya,” amesema Nana.

Msemaji mwingine aliyesimama kuzungumza kwa muda kutokana na kulia, ni Dk. Seif Muba, ambaye alikuwa mwanafunzi wa Prof. Ngowi.

Dk. Muba alishindwa kujizuia kwa kuangua kilio, wakati anasoma wasifu wa Prof. Ngowi, katika kipengele cha tarehe ya kufariki kwake.

Alipokuwa anataja tarehe ya kifo cha Prof. Ngowi, alipofikia kwenye kipengele cha “kifo chake kimeacha pengo na huzuni kubwa kwa familia, jamii na taifa kwa ujumla” alianza kulia kwa dakika kadhaa, kisha akaendelea kusoma wasifu huo.

“Hapa anayesoma risala hii ni mwanafunzi wa Prof. Ngowi aliyenifundisha 2002, ameacha wanafunzi wengi aliowafundisha,” amesema Dk. Muba.

Akielezea maisha ya utumishi wa Prof. Ngowi, Dk. Muba amesema alikuwa mcheshi, mnyenyekevu na mwenye kujituma.

Mwingine aliyelia wakati anazungumza kwenye ibara hiyo, ni Mwakilishi wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Jonas Baraka, akielezea mara ya mwisho alivyoonana naye ofisini kwake, Alhamisi iliyopita, ambapo alimuahidi wataonana Jumatatu, siku ambayo alipoteza maisha.

“Alitamani sana siku moja wanafunzi kujitegemea wenyewe katika maoni yao, pamoja na tulichojadili tulikubaliana kwamba siku jumatatu ambako umauti ulimkuta tutaona,” amesema Baraka.

Prof. Ngowi na dereva wake, Mringo, walifariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea maeneo ya Mlandizi mkoani Pwani, ambapo gari yao iliangukiwa na kontena.

Prof. Ngowi alipata ajali hiyo akiwa safarini kuelekea mkoani Morogoro kikazi, akitokea Dar es Salaam.

Baada ya miili yao kuagwa, inatarajiwa kusafirishwa katika nyakati tofauti, kwenda Moshi mkoani Kilimanjaro, kwa ajili ya mazishi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Wakili: Ukimpa zawadi mwenza marufuku kumpora hata mkiachana

Spread the love  WANANDOA na watu waliko kwenye mahusiano ya kimapenzi, wamekumbushwa...

Habari Mchanganyiko

Majaliwa: Mvua zimesababisha vifo vya watu 155, kuendelea hadi Mei

Spread the love  WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mvua kubwa za El-Nino...

Habari Mchanganyiko

Exim Bank yatoa  vitanda kwa shule ya Jeshi la Polisi Moshi

Spread the love  BENKI ya Exim imekabidhii  seti ya vitanda kwa Shule...

Habari Mchanganyiko

NBC yakabidhi vitanda Shule ya Polisi Moshi

Spread the loveBenki ya NBC imekabidhi msaada wa vitanda 28 kwa Shule...

error: Content is protected !!