October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yaombwa kuingiza tafiti za Prof. Ngowi kwenye mitaala

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania, imeshauriwa kuingiza katika mitaala ya elimu ya juu, ripoti za tafiti zilizofanywa na aliyekuwa Profesa Mshiriki wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Honest Ngowi, ili kumuenzi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Wito huo umetolewa na Mratibu wa Udhibiti Ubora kutoka Shirika la HakiElimu, Dk. Ellen Otaru wakati akizungumza katika ibada ya kuuaga mwili wa Prof. Ngowi na wa dereva wake, Innocent Mringo iliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.

Prof. Ngowi na Mringo, walifariki dunia katika ajali ya gari, iliyotokea maeneo ya Mlandizi mkoani Pwani, tarehe 28 Machi 2022, baada ya gari lake kuangukiwa na kontena. Alikuwa anaelekea Morogoro kikazi, akitokea Dar es Salaam.

“Ninaomba kusihi sana yale ambayo tuliyaona yameandikwa na Prof. Ngowi, tusiishie kwenye maandikio, chuo tuna wanataaluma tuhakikishe tunaingiza aliyotafsiri yawafikie walengwa wote Tanzania. Iwe kwenye mitaala yetu, tuingize kwenye mifumo ya elimu katika vyuo nchini,” amesema Dk. Otaru.

Dk. Otaru amesema Prof. Ngowi aliandika uchambuzi wake kuhusu masuala mbalimbali, ikiwemo ya kiuchumi katika magazeti, ambayo alikuwa anayatafsiri kutoka lugha mbalimbali za kimataifa.

Awali akisoma wasifu wa Prof. Ngowi, Dk. Seif Muba amesema mwanataaluma huyo alifanya tafiti mbalimbali, pamoja na kutoa ushauri ndani ya Chuo Kikuu cha Mzumbe na nje ya chuo hicho.

“Prof. Ngowi ni mtafiti na mshauri katika masuala ya uchumi na biashara. Amefanya tafiti na ushauri kwa ujumla katika maeneo ya uchumi na biashara, ikiwa na pamoja na uchumi mkubwa na mdogo, biashara ya kimataifa, uwekezaji, ujasirialiamali, Sekta zisizo rasmi, ubinafsishaji,” amesema Dk. Muba.

Dk. Muba amesema “ushirikiano wa kibinafsi wa umma, usimamizi wa miradi, uchumi katika ushirikiano wa kikanda, usimamizi wa fedha za umma; umasikini, mdororo wa kifedha/uchumi wa dunia, mapinduzi ya nne ya viwanda, mtizamo wa uchumi kwenye UVIKO 19 na masuala mengine mengi.”

Amesema, Prof. Ngowi ameandika machapisho zaidi ya 50 katika majarida ya kitaifa na kimataifa, pamoja na machapisho 1,000, kwenye magazeti yanayohusu masuala ya uchumi na biashara.

Dk. Muba ametaja kazi zilizofanywa na Prof. Ngowi, ikiwemo ile ya upangaji, utekelezaji na usimamizi wa miradi katika sekta mbalimbali kama kilimo, afya, uwekezaji na biashara.

“Kazi nyingine ni kuelekeza na kufundisha jinsi ya kutumia na kuchochea fursa za kimaendeleo, na kupambana na changamoto za biashara na uchumi katika jamii na taifa kwa ujumla,” amesema Dk. Muba.

Kazi nyingine alizofanya Prof. Ngowi ni, kuzijengea uwezo asasi za kijamii na zisizo za kiserikali, katika masuala ya kupambana na umasiki, kutoa ushauri kwenye masuala ya tozo na kodi, biashara ndogondogo na za kati, vyanzo vya mapato.

Nyingine ni Kufanya tathmini katika maendeleo miradi mbalimbali ya kimataifa ikiwemo Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Shirika la Chakula Duniani (FAO).

error: Content is protected !!