Friday , 26 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Vijiji 2,349 kufaidika na miradi ya TASAF
Habari Mchanganyiko

Vijiji 2,349 kufaidika na miradi ya TASAF

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga akifungua kikao cha Mapitio ya Kati ya Utekelezaji wa Kipindi cha Pili cha Mpango wa TASAF
Spread the love

 

IMEELEZWA kuwa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF, inatarajiwa kutoa ajira kwa walengwa 195,000 ambao watalipwa jumla ya shilingi bilioni 36 kama ujira wa kushiriki katika kazi hizo kwa mwaka 2021 – 2022 katika Vijiji/Mitaa/Shehia 2,349 za Tanzania Bara na Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamebainishwa katika mkutano wa TASAF pamoja na wadau wa maendeleo waliokutana hivi karibuni kufanya mapitio ya kipindi cha pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF.

Kikao hicho cha wiki mbili kilifunguliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamaga katika ukumbi wa Mikutano wa TASAF Jijini Dar es Salaam.

Pia kilihudhuriwa na wadau ambao wanachangia utekelezaji wa mpango wa TASAF ambao ni Benki ya Dunia, Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya ILO, WFP na UNICEF.

Wengine waliohudhuria ni wawakilishi kutoka SIDA, Umoja wa Nchi za Ulaya (EU), Ubalozi wa Uswisi, Ubalozi wa Norway, Bill and Melinda Gates Foundation na FSDT.

Aidha, wawakilishi kutoka Halmashauri za Kagera, Magu, Chunya na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar wamehudhuria.

Kiongozi wa shughuli za TASAF katika Benki ya Dunia Tanzania, Michele Zini, akizungumza katika kikao cha Mapitio ya Kati ya Kipindi cha Pili cha Mpango wa TASAF

Mwenyekiti Mwenza wa Kikao hicho ambaye pia ni Kiongozi wa Shughuli za TASAF katika Benki ya Dunia nchini Tanzania, Michele Zini aliipongeza TASAF kwa kazi nzuri ambayo imefanyika kupitia miradi ya Ajira za Muda, Kujenga Uchumi wa Kaya na Uhawilishaji Fedha.

Amesema Benki ya Dunia pamoja na wadau wengine ambao wanachangia utekelezaji wa TASAF wameridhishwa na utekelezaji wa kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu na wanajivunia mafanikio ya walengwa ambao wamepiga hatua katika kujikwamua kiuchumi na kuwapatia watoto wao mahitaji yao ya msingi.

Katika vikao vya mapitio, washiriki hupata nafasi ya kwenda kwenye maeneo ya utekelezaji na kufanya mazungumzo na walengwa, watendaji na viongozi kuhusu utekelezaji.

Hata hivyo, katika kipindi hiki, ziara za kwenye maeneo ya utekelezaji hazitafanyika na badala yake wawakilishi waliohudhuria kutoka maeneo ya utekelezaji watatoa taarifa za utekelezaji wa maeneo yao.

Mapitio ya utekelezaji wa mpango wa TASAF utahusisha kujadili taarifa za utekelezaji, kubainisha changamoto za utekelezaji na hatimaye kuja na mapendekezo ya kuboresha kipindi kilichobaki na kitakachofuata.

Baadhi ya washiriki wakifuatilia ufunguzi wa kikao cha Mapitio ya Kati ya Kipindi cha Pili cha Mpango wa TASAF

Akizungumzia utekelezaji wa kipindi hiki, Michele amesema pamoja na kwamba toka kipindi cha pili cha Mfuko wa TASAF kilipozinduliwa, kulitokea matukio mengi yaliyosababisha kuchelewa kuanza utekelezaji hata hivyo, kazi zote zilizopangwa zilifanyika kwa ufanisi ikiwemo walengwa wa zamani kuhakikiwa.

“Pia walengwa wapya kutambuliwa na kulipwa stahili zao ndani ya dirisha la malipo lililofunguliwa mwezi Januari 2022. Kaya za walengwa wa kipindi cha kwanza wamelipwa malipo yao kwa mikupuo miwili.

“Walengwa wapya na kipindi cha pili wamelipwa kwa mkupuo mmoja wa kwanza na kiasi cha fedha kilicholipwa ni jumla ya shilingi bilioni 51.1,” amesema.

Mbali na malipo kwa walengwa, utekelezaji wa miradi inayotoa ajira za muda kwa walengwa na kuboresha miundombinu imetekelezwa katika halmashauri 51 na jumla ya miradi 3,185 imeibuliwa.

Amesema miradi hiyo inatarajiwa kutoa ajira kwa walengwa 195,000 ambao watalipwa jumla ya shilingi bilioni 36 kama ujira wa kushiriki katika kazi hizo kwa mwaka 2021 – 2022 katika Vijiji/Mitaa/Shehia 2,349 za Tanzania Bara na Zanzibar.

“Mpango mwingine ambao unatekelezwa ndani ya Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF ni Mpango wa Kukuza Uchumi wa Kaya. Utekelezaji wa mpango unaendelea ingawa bado kuna kazi kubwa ya kufanya ikiwemo kuangalia namna bora zaidi ya kuwawezesha Walengwa kuweza kukuza uchumi wa kaya zao,” amesema.

Watumishi wa TASAF katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa maendeleo wanaochangia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF baada ya kufunguzi wa kikao cha Mapitio ya Kati ya Kipindi cha Pili cha TASAF

Amesema lengo la mapitio ya Kipindi cha Pili cha Mpango wa TASAF ni kuangalia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha utekelezaji na kujadili namna bora ya kukamilisha kipindi hiki ambacho kinatarajiwa kukamilika 2023.

Aidha, Michele amewataka washiriki kujadili namna bora ya kukamilisha kipindi cha pili kwani anaamini kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha walengwa ambao ni kaya zinazoishi katika mazingira duni wanawezeshwa ili kukidhi mahitaji ya msingi.

Pamoja na mambo mengine Michele amegusia uwezekano wa kuongeza muda wa utekelezaji wa kipindi hiki cha Pili ili kukamilisha mipango iliyowekwa.

Amewataka washiriki kutumia muda wa majadiliano kuja na mapendekezo ya muda utakaohitajika kukamilisha mipango ya Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu.

Michele amesema kwa niaba ya wadau wote wa Maendeleo ambao wamekuwa wakichangia shughuli za TASAF kwamba wameridhishwa na utekelezaji na wako tayari kuendelea kuchangia utekelezaji wa Mpango huu wa TASAF ili kuhakikisha kwamba Walengwa wanapata ruzuku zao ipasavyo.

“Nawashukuru wote wanaohusika katika utekelezaji kuanzia ngazi ya Jamii, Halmashauri, Mikoa, Taifa na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar kwa kusimamia vyema utekelezaji wa Kipindi cha Pili na pia kuja na mpango nzuri wa utekelezaji wa kukamilisha Kipindi kilichobakia na kuandaa Awamu inayofuata,” amesema.

Kwa nyakati tofauti mkutano huu ulihusisha pia mazungumzo na Katibu Mkuu Ikulu Dk. Moses Kusiluka, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Ndugu Idarous Fairia na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mpango Bwana Emmanuel Tububa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Wakili: Ukimpa zawadi mwenza marufuku kumpora hata mkiachana

Spread the love  WANANDOA na watu waliko kwenye mahusiano ya kimapenzi, wamekumbushwa...

Habari Mchanganyiko

Majaliwa: Mvua zimesababisha vifo vya watu 155, kuendelea hadi Mei

Spread the love  WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mvua kubwa za El-Nino...

Habari Mchanganyiko

Exim Bank yatoa  vitanda kwa shule ya Jeshi la Polisi Moshi

Spread the love  BENKI ya Exim imekabidhii  seti ya vitanda kwa Shule...

Habari Mchanganyiko

NBC yakabidhi vitanda Shule ya Polisi Moshi

Spread the loveBenki ya NBC imekabidhi msaada wa vitanda 28 kwa Shule...

error: Content is protected !!