WAZIRI Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson anakabiliwa na kitisho katika utawala wake baada ya wabunge kadhaa wa chama chake kupanga kuwasilisha barua za kutaka kuitishwa kwa mchakato wa kura ya kutokuwa na imani naye. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Gazeti maarufu nchini Uingereza, Daily Telegraph limeripoti habari hizo likinukuu duru kutoka ndani ya chama cha Conservatives, ambacho ndicho anachotoka Waziri Mkuu Johnson.
Taarifa zinasema, mpaka sasa, tayari wabunge 20 kutoka chama hicho, wameahidi kuwasilisha barua zao katika wakati hasira ya umma inaongezeka kufuatia ufichuzi kwamba waziri mkuu Johnson alikiuka sheria za kukabiliana na janga la corona.
Kwa mujibu wa taratibu za chama hicho, barua 54 ndiyo zinahitajia kuanzisha mchakato wa kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu na duru zinasema idadi hiyo huenda itafikiwa hivi karibuni.
Johnson, Meya wa zamani wa mji wa Londona, analaumiwa kwa kuhudhuria dhifa iliyoandaliwa kwenye ofisi yake ya mtaa wa Downing mwaka 2020, wakati Uingereza ilipokuwa imezuia mikusanyiko yote ya umma ili kuweza kukabiliana na janga la Covid-19.
Johnson alichaguliwa kuwa kiongozi mpya wa chama cha Conservative na aliingia madarakani kumrithi aliyekuwa waziri mkuu wa taifa hilo, Theresa May, Julai mwaka 2019.
Alipata kura 92, 153 dhidi ya aliyekuwa mpinzani wake mkubwa Jeremy Hunt, ambaye alipata kura 46,656, wakati wa mzozo wa kuiondoa Uingereza kwenye Jumuiya ya Ulaya (EU).
Leave a comment