Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Utoaji hati wasitishwa Arusha
Habari za Siasa

Utoaji hati wasitishwa Arusha

Jerry Silaa
Spread the love

KAMISHNA wa Ardhi mkoani Arusha, Geofrey Msomsojo amezuia zoezi la utoaji hati za umiliki wa ardhi, katika eneo la ekari sita, lililopo kata ya Olmoti katika jiji hilo kutokana na eneo hilo kuwa na mgogoro kwa miaka 17 sasa, ikiwa ni utekelezaji agizo la siku 30 la Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Slaa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).

Waziri Slaa wiki iliyopita, alitembelea eneo hilo na kuzungumza na William Mollel ambaye analalamika eneo lake kuvamiwa pamoja na majirani wa eneo.

Katika mgogoro huo, familia ya Mollel inamtuhumu aliyekuwa Ofisa Ardhi jiji la Arusha, Chritopher Kitundu ambaye hivi sasa amehamishiwa wilaya ya Tandahimba kuuziwa eneo na Leah Neeva hilo kinyume cha sheria.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, Kitundu alikana kuvamia eneo hilo na kueleza wanaomlalamikia waende mahakamani badala ya kumtuhumu kuvamia eneo lao.

“Mimi sijavamia eneo la mtu, kama kuna wanaonilalamikia basi waende mahakamani, ndipo haki inaweza kupatikana,” amesema.

Akizungumza katika kikao cha kutafuta suhulu ya mgogoro huo, Kamishna Msomsojo akiwa na Ofisa Ardhi wa mkoa huo, Neema Uloma amesema ameamua kusitisha utoaji hati wa viwanja katika eneo hilo, hadi suluhu itakapopatikana.

Amesema katika kutekeleza maagizo ya Waziri, Slaa juzi (Jumatatu) akiwa na maafisa wake, watafika tena katika shamba lenye mgogoro na kuzungumza na pande zote wakiwemo majirani ambao nao wanalalamika  kumegwa ardhi yao.

“Tumepata taarifa kupimwa kwa eneo hilo na maafisa wetu wa ardhi licha ya kuwepo mgogoro  na kuanza kuuzwa viwanja taratibu za kinidhamu zinaendelea na sasa tumesitisha utoaji wa hati,” amesema.

Awali Mollel amesema kwa miaka 17 wamekuwa katika mgogoro huo, baada ya Neeva Savoroi kuvamia shamba hilo ambaye tayari alifariki na baadaye mkewe Leah Neeva kuendelea kulimiliki kinyume cha sheria na kumuuzia Kitundu.

Amesema suala hilo limefikishwa Baraza la Ardhi la Kata  kwa shauri namba S/2006 ambalo alishinda na baadaye shauri kuhamishiwa baraza la ardhi wilaya na baada ya kukata rufaa mahakama ya rufaa, shauri hilo lilirejeshwa baraza la ardhi.

“Hata hivyo wakati shauri lipo bado katika baraza la ardhi, Kitundu alitumia maafisa wenzake wa ardhi, kwenda kupima eneo hilo na kukata viwanja ploti namba 60-70 Block A, Plan No E/248/205 mnano Agosti mwaka jana,” amesema.

Amesema baada ya tukio hilo, walipeleka malalamiko baraza la ardhi na ofisi za Serikali kata ya Olmoti, ambao walifika shambani na kuagiza kusitishwa upimaji lakini maafisa hao walikaidi.

Mwenyekiti wa baraza la ardhi kata ya Olmoti, Yusuph Abdalah alikiri kuwepo na shauri la mgogoro huo, hata hivyo, amesema mlalamikiwa aliyeuza eneo hilo, Leah Neeva ameandika barua kutokuwa na imani na baraza na hivyo hatashiriki katika shauri hilo.

“Hili shauri bado lipo hapa, kwetu lakini Mlalamikiwa amekuwa hafiki kwenye vikao vya baraza na tayari ameandika barua rasmi kutokuwa na imani na baraza la ardhi,” amesema.

Hata hivyo, Neeva akizungumzia eneo hilo, ameeleza ni eneo la familia yake na waliuziwa na Mollel (ambaye analalamika kuvamiwa) miaka ya nyuma.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za SiasaTangulizi

Samia awataka watanzania kudumisha muungano

Spread the loveRais wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuendeleza Muungano kwa...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

error: Content is protected !!