Sunday , 30 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Usiyoyajua ziara ya Rais Samia Korea Kusini
Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Usiyoyajua ziara ya Rais Samia Korea Kusini

Spread the love

MWEI 31 mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa na ujumbe mzito, alisafiri umbali wa kilomita 10,200 kutoka jijini Dar es Salaam hadi jiji la Seoul, Korea Kusini (Jamhuri ya Korea) katika juhudi mpya za kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na taifa hilo lililoendelea kiteknolojia la mashariki ya mbali.  Anaandika Gabriel Mushi … (endelea).

Kwa mara ya kwanza, katika ziara hiyo ya siku sita, Rais Samia ameambatana pia na wasanii mbalimbali wa filamu nchini ili kwenda kubadilishana uzoefu na kujifunza mambo yanayoweza kuboresha tasnia hiyo hasa ikizingatiwa Korea imepiga hatua kubwa katika sekta ya sanaa.

Tanzania na Korea zimekuwa na uhusiano mzuri kwa zaidi ya miaka 32 sasa, huku Tanzania ikifaidika katika nyanja mbalimbali kutokana na ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Katika ziara hiyo, Rais Samia ameshuhudia utiwaji saini wa mkataba mmoja wa mkopo wa masharti nafuu wa dola za Marekani 2.5 bilioni sawa na shilingi 6.5 trilioni, kwa ajili ya miradi ya miundombinu.

Mkataba huo unalenga ushirikiano kwenye utafiti, uwekezaji na kujenga uwezo wa kuongeza thamani ya madini ya kimkakati hasa ya nickel, lithium na kinywe.

Mbali na mkataba huo, Rais Samia alishuhudia utiwaji saini wa Hati ya Maelewano (Memorandum of Understanding-MOU) katika sekta za Uchumi wa Bluu na Madini ya Kimkakati.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Korea, Yoon Suk Yeol kabla ya kushuhudia utiaji saini Mikataba mbalimbali baina ya nchi mbili kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Seoul.

Aidha, alishuhudia kusainiwa kwa Tamko la Utayari wa Kuanza Majadiliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi (Joint Statement on the launch of Negotiation on Economic Partnership Agreement-EPA).

Fedha hizo kwa ajili ya miundombinu ya maendeleo zitatolewa chini ya Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Serikali ya Korea (EDCF) kwa masharti nafuu.

Hii ni mara ya tatu mfuko huo wa EDCF unatoa mkopo wenye masharti nafuu kwa Serikali ya Tanzania kwani mara ya kwanza ilikuwa katika kipindi cha mwaka 2014 hadi 2020 ambapo ilitoa kwanza dola za Marekani milioni 733 ambazo zilitumika kwenye mradi ya ujenzi wa Hospitali ya Taifa ya Mloganzila Muhimbili, Daraja la Maragarasi, Mradi wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA), mradi wa umwagiliaji Zanzibar.

Mara ya pili ni mwaka 2021 hadi 2025 ambapo Korea ilitoa dola bilioni moja kwa ajili ya mradi wa upimaji ardhi kidijitali ambao utawekeza data za viwanja kidijitali kupitia Chuo cha Tekonolojia Kijiditali (DTI) na Ujenzi wa Hospitali ya Miguni Zanzibar ya vitanda 600.

Pia kuna mradi wa dola milioni 230 wa kuijenga upya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambayo itakuwa ni maghorofa. Ujenzi huo unaendelea hadi 2030.

Katika mkopo huo wa tatu ambao ni wa dola za Marekani bilioni 2.5 utadumu kuanzia mwaka 2024 hadi 2028.

Kwa mujibu wa Balozi wa Tanzania nchini Korea, Togolani Mavura, nchi 59 zilizoko barani Afrika, Asia na Ulaya zinafaidika na mkopo wa aina hii kutoka EDCF.

Anasema mkopo huo wa dola bilioni 2.5 ni wa masharti nafuu una riba ya asilimia 0.01, unalipwa kwa miaka 40, na una fungate (grace period) ya miaka 25.

“Yaani unaanza kulipa baada ya mwaka wa 26. Hivyo, si kweli kwamba mkopo huo utalipwa kwa miaka mitano,” anasema.

Mikopo ya aina hii inaungwa mkono na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu ambaye anasema kwa upande wao wawakilishi wa vyama vya upinzani, hawapingi ukopaji, ila wanapinga mikopo yenye masharti ya kibiashara. Lakini kwa upande wa mikopo hiyo yenye masharti nafuu wanaiunga mkono.

Kwa maana hiyo, ushirikiano kati ya Tanzania na Korea Kusini umeendelea kuiletea maendeleo Tanzania katika nyanja mbalimbali. Kwa sababu Korea imeshiriki katika miradi mingine ya maendeleo nchini ikiwamo ujenzi wa mradi wa maji safi na maji taka Iringa na ujenzi wa daraja la Malagarasi na daraja la Tanzanite.

Kwa upande wa biashara kati ya nchi hizi mbili, pia imeendelea kukua. Kwa mujibu wa Mtandao wa Takwimu za Kiuchumi Duniani (OEC), katika kipindi cha miaka 27 iliyopita, biashara kati ya Tanzania na Korea imekua kutoka dola milioni 17.4 mwaka 1995 hadi dola milioni 344 mwaka 2022.

Rais Samia ambaye pia ametunukiwa shahada ya Udaktari wa Falsafa wa Heshima (Honoris Causa) kwenye Sekta ya Anga na Rais wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga (Korean Aerospace University), Hee Young Hurr ametumia ziara hiyo kuweka nia ya kujenga chuo cha masuala ya anga nchini kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga cha Korea.

Rais Samia anasema sekta ya anga ya Tanzania kati ya mwaka 2021 – 2023 imekua, kwani abiria wameongezeka kila mwaka kwa takriban asilimia 28 na pia idadi ya ndege zinazofanya safari za kimataifa zimeongezeka kutoka 26 hadi 33.

Anasema idadi ya wasafiri wa ndani imeongezeka kwa asilimia 26.5 baada ya Covid-19 kutoka abiria milioni tatu hadi kufikia milioni 3.8 kwa mwaka 2023.

“Kabla mwaka 2016, ATCL ilikuwa na ndege moja inayofanya kazi ambapo hadi kufikia Machi 2024 zimeongezeka ndege 14 za abiria na moja ya mizigo. Ndege 6 kati ya hizo zimenunuliwa katika kipindi cha miaka mitatu ikiwemo ndege ya mizigo.

“Vilevile mtandao wake umepanuliwa kutoka maeneo manne tu nchini hadi 24, ikiwemo safari katika miji minane barani Afrika na mitatu ya kimataifa (Guangzhou, Dubai na Mumbai),” anasema.

Rais Samia amesema kufufua shirika hilo kumesaidia kuongeza mapato kutoka shilingi 23 bilioni mwaka 2016/17 hadi Sh 380.4 bilioni mwaka 2022/23.

Pia, soko la shirika la ATCL la safari za ndani limefika asilimia 53 kutoka asilimia 2.4 tu mwaka 2022/23, huku idadi ya abiria imeongezeka kwa asilimia 42 kutoka milioni 4.8 mwaka 2015 hadi milioni 6.8 mwaka 2024.

Mbali na hapo, idadi ya marubani waliosajiliwa na wahandisi wa ndege imeongezeka kufikia 604 ikiwa ni ongezeko la asilimia 21 na wahandisi kufikia 76 ambalo ni ongezeko la asilimia 181 mpaka mwisho wa mwaka 2023.

“Mchango katika sekta ya anga kwenye Pato la Taifa la Tanzania umeongezeka kutoka asilimia 0.9 mwaka 2018 hadi asilimia 2.5 mwaka 2023,” anasema.

Rais Samia ambaye pia ni mwanamke pekee aliyeshiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kati ya Korea na Afrika, mapema wiki hii, ameendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano na uwekezaji kwenye ajenda ya nishati safi ya kupikia huku akimtaka Rais wa Jamhuri ya Korea, Yoon Suk Yeol kuungana na mataifa ya Afrika katika ajenda hiyo.

“Kwa kuwa mimi ni Rais mwanamke pekee katika chumba hiki, lazima nizungumzie ajenda ambayo ni muhimu kwa Afrika hasa kwa wanawake, na hii ni kuwekeza kwenye ajenda ya nishati safi ya kupikia,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Yeol wa Korea amesema nchi yake inakusudia kuongeza uwekezaji pamoja na biashara na mataifa ya Afrika.

“Korea Kusini itakuza zaidi uhusiano wake na mataifa ya Afrika katika kuimarisha mifumo ya kidigitali pamoja na kushirikiana katika masuala mtambuka yanayoikumba dunia kwa sasa,” anasema Rais Yeol.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Mpina amng’ang’ania Bashe, kumburuza mahakamani pamoja na bodi ya sukari

Spread the loveMbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM) amesema amenuia kumpeleka mahakamani...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Majahazi yadakwa na madumu 1,731 ya mafuta ya kupikia

Spread the loveKikosi kazi cha Polisi Wanamaji Dar es Salaam kimekamata majahazi...

Habari za SiasaKimataifa

30 wafariki dunia maandamano Kenya

Spread the loveShirika la Human Rights Watch limesema takriban watu 30 walifariki...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Tanzania yakubali kukutana na mabalozi 9 kutatua changamoto za kikodi

Spread the loveSerikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na...

error: Content is protected !!