September 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Urais Chadema: Mbowe ‘kuwavaa’ Lissu, Nyalandu na Dk.Maryrose

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

FREEMAN Mbowe, amejitosa katika kinyang’anyiro cha kutia nia kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Demokarsia na Maendeleo (Chadema). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea)

Mbowe ametia nia hiyo leo Jumatatu tarehe 15 Juni 2020 baada ya kupelekewa barua iliyoandikwa na baadhi ya wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam wa chama hicho ili aisaini na kupelekwa Ofisi ya Katibu Mkuu.

Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema, amepelekewa barua hiyo nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, anakoendelea kupata matibabu baada ya kudaiwa kushambuliwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia tarehe 9 Juni 2020.

Tukio hilo lilitokea akiwa anapanda ngazi nyumbani kwake Area D jijini Dodoma.

Hatua ya Mbowe kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho, kinazidisha joto la urais ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania.

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema

Joto hilo, linatokana na waliokwisha kujitokeza kuwania nafasi hiyo kuwa na ushawishi ndani ya chama hicho hivyo kukipa wakati mgumu kumpata mmoja.

Wengine waliokwisha jitosa ni; Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Tundu Lissu, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Lazaro Nyalandu na mwanachama wa chama hicho, Dk. Maryrose Majige.

Dk. Maryrose Majinge, kada wa Chadema aliyetangaza nia ya kuwania Urais kupitia chama hicho

Akizungumza na wazee hao nyumbani kwake, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni amesema, hakukusudia kujitokeza kutiua nia kwani, “waliojitokeza kwa hatua ya sasa ni wazuri, bora na bado kuna imani kuna wagombea wengine bora.”

“Sikukusudia kutia nia katika nafasi ya kugombea nafasi ya urais, siyo kwa sababu siwezi ila naamini katika kutumia muda mwingi kujenga taasisi, kujenga chama na kuinuanua vijana viongozi, wazee, wana mama,” amesema Mbowe.

Mch. Peter Msigwa

Amesema, “nimekitumikia chama hiki tangu nimezaliwa, kwa unyenyekevu kwa miaka 30” na kwa umri wake wa ujana “nimeutumika katika harakati. Sasa hili ombi wazee wangu, sisi kama chama tuliweka utaratibu wa leo ndio siku ya mwisho kutangazania.”

Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai ambako ametia nia ya kugombea tena amesema, “wapo waliotangaza nia hadharani na wapo ambao wamewasilisha barua kwa katibu mkuu, wote ni wa kwetu na chama kwa kutumika mifumo yao itawapima na mwisho wa siku atapatikana mmoja na wote watamuunga mkono.”

Lazaro Nyalandu, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati

Amesema, yeye kama mwenmyekiti hatokubali mchuano huo wa kumpata mmoja atakayepeperusha bendera akigawa chama kwa kuwa na kundi lake, bali atahakikisha baada ya mchakato chama kinakuwa kimoja.

Mbowe amesema licha ya wazee hao kumpendekeza na kuisaini barua hiyo na kupelekwa ofisi ya katibu mkuu, imani yake ni kuona chama hicho kinampata mgombea sahihi miongoni mwa waliojitokeza na kila mmoja aliyejitokeza amuunge mkono.

Kama atapitishwa na chama hicho kuwania Urais, itakuwa ni mara ya pili kwani mwaka 2005 aliwania akichuana na mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Mrisho Kikwete na Kikwete kuibuka mshindi.

error: Content is protected !!