KATIKA kukabiliana na majanga ya moto, Halmashauri ya mji Tunduma mkoani Songwe umetenga Sh 377 milioni za mapato ya ndani kununua gari la zima moto. Anaripoti Ibrahim Yassin, Songwe…(endelea).
Akizungumza leo tarehe 10 Julai 2023 ofisini kwake mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Phillimon Magesa amesema kutokana na mji wa Tunduma kukua kwa kasi huku ujenzi wa masoko ukiongezeka, wameamua kununua gari la zima moto kujikinga na majanga ya moto pindi yatakapotokea.
Amesema gari hilo lenye thamani ya Sh 377 milioni, wamepanga kulipa kwa awamu tatu kupitia fedha za mapato ya ndani.
Amesema kwa kuanzia wamelipa Sh 130 milioni lengo ikiwa ni kuhakikisha wafanyabiashara wanaokolewa bidhaa zao pindi zitokeapo ajili za majanga ya moto.
Amesema mbali na gari hilo la zima moto pia wametenga Sh. 6 milioni kununua gari litakalokuwa likifanya kazi ya kutembelea miradi ya halmashauri hiyo.
Pia amesema wanaendelea na mipango ya kufungua kampuni itakayofanya kazi hiyo ya usimamizi wa vitega uchumi vya halmashauri.
Amesema kutokana na uwepo wa mipango hiyo, wanataka kuunda kampuni au chombo (Special purpose vehicle (SPV) kitakachosimamia shughuli mbalimbali zikiwemo za kibiashara na uzalishaji.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ayoub Mlimba amesema nia ya baraza la madiwani kupitisha manunuzi hayo ni kutaka mali za wafanyabiashara na wawekezaji wa miradi mbalimbali kuwa salama na kuwavuta wawekezaji wengi kuja kuwekeza Tunduma.
Leave a comment