November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

THRDC kuimarisha utetezi haki za binadamu mikoa ya Kusini

Spread the love

 

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umeahidi kuzifanyia kazi changamoto zinazokwamisha shughuli za utetezi wa haki za binadamu, zinazotekelezwa na Asasi za Kiraia, zilizoko katika Kanda ya Pwani Kusini. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ahadi hiyo imetolewa leo Jumatatu, tarehe 25 Oktoba 2021 na Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, akizungumzia ziara yake ya kikazi katika kanda hiyo, inayojumuisha mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara.

“Sisi kama mtandao tunajitahidi kuendelea kuwa na kanda hii kwa karibu, sababu tumejua ina changamoto nyingi za ustawi wa asasi za kiraia. Tutakuwa karibu na kanda hii kuhakikisha zinasadiwa, zinajengewa uwezo ziweze kujiendesha vizuri zaidi,” amesema Olengurumwa.

Mratibu huyo wa THRDC ametoa ahadi hiyo baada ya kubaini changamoto zinazozikabili asasi hizo, ikiwemo ukata wa rasilimali fedha.

“Tunashukuru wanachama wetu wanafanya kazi zao kama walivyopanga kufanya, ingawa kuna changamoto za hapa na pale. Kikubwa ni kwamba, operesheni za asasi za kirai katika kanda hii zinakabiliwa sana na changamoto za rasilimali fedha,” amesema Olengurumwa na kuongeza:

“Nyingi zinafanya operesheni zao bila kuwa na rasilimali fedha, baadhi zinakabiliwa na changamoto za kiofisi ambazo pengine tunahitaji kuona namna gani kuzitatua. Tatizo zinarudisha nyuma harakati na shughili za utetezi wa haki za binadamu katika Kanda ya Kusini.”

Naye Mratibu wa THRDC Kanda ya Pwani Kusini, Clemence Mwombeki, amesema ujio wa Olengurumwa katika kanda hiyo, utazisaidia asasi za kiraia zilizoko kwenye maeneo hayo kupata suluhu ya changamoto zinazozikabili.

“Kwa kiwango kikubwa ujio wa mratibu kwenye Kanda ya Pwani Kusini, inayojumuisha mikoa mitatu umekuwa wa hamasa kubwa ikizingatia THRDC ina kanda 11 na hii moja wapo,” amesema Mwombeki na kuongeza:

“Tuna wanachama wengi hii imetupa nguvu, ameelewa changamoto za wanachama wake, fursa zilizopo na mambo mengine ya kushirikiana pamoja, kuhakikisha tunaboresha mazingira ya utetezi wa haki za binadamu .”

error: Content is protected !!