Tuesday , 23 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Jaji mwingine apangiwa kesi ya Mbowe, kuanza kusikiliza
Habari za SiasaTangulizi

Jaji mwingine apangiwa kesi ya Mbowe, kuanza kusikiliza

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi nchini Tanzania, kesho Jumanne tarehe 26 Oktoba 2021, itaendelea kusikiliza kesi inayomkabili kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini humo cha Chadema, Freeman Mbowe na wenzake. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Kesi hiyo ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya kupanga njama za vitendo vya ugaidi, itaendelea kusikilizwa chini ya jaji mpya. Ni baada ya aliyekuwa akiisikilisa Jaji Kiongozi Mustapha Siyani kujitoa.

Siyani aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, alianza kusikiliza kesi hiyo tarehe 10 Septemba 2021, baada ya aliyekuwa akiisikiliza Jaji Elinaza Luvanda kujitoa.

Jaji Luvanda alitangaza kujitoa tarehe 6 Septemba 2021, baada ya Mbowe akiwawakilisha washtakiwa wenzake, kuomba ajitoe kwani hawana imani kama atawatendea haki, ombi ambalo alilikubali naye akajitoa.

Siyani, alijitoa ikiwa ni takribani wiki mbili zimepita tangu Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alipomteua kuwa Jaji Kiongozi, tarehe 8 Oktoba 2021.

Siyani aliteuliwa kuchukua nafasi ya Eliezer Feleshi ambaye yeye aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, Halfan Hassan Bwire, Adam Kasekwa na Mohamed Abdillah Ling’wenya.

Taarifa kwa umma, iliyotolewa leo Jumatatu, tarehe 25 Oktoba 2021 na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, imesema tayari mahakama hiyo imewapatia taarifa rasmi ya wito mawakili, watuhumiwa na Jeshi la Magereza.

“Kesi ya Mwenyekiti na wenzake namba 16/2021, ya uhujumu uchumi yenye mashitaka ya ugaidi ndani yake, itaendelea kesho Jumanne.”

“Tayari Mahakama wameshawapatia taarifa rasmi ya wito (summons) mawakili, watuhumiwa pamoja na Jeshi la Magereza, kuhusu kuwafikisha watuhumiwa mahakamani,” imesema taarifa ya Mrema.

Taarifa ya Mrema imesema, mahakama hiyo haijamtaja jaji aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo.

“Tunachukua nafasi hii kuwajulisha wananchi, kesi hiyo imepangwa kuanza chini ya Jaji ambaye atakuwa amepangiwa kuendelea na shauri hilo, baada ya Jaji Kiongozi Mustapha Siyani, aliyekuwa anasikiliza shauri hilo kujitoa kuendelea na kesi hiyo,” imesema taarifa ya Mrema.

Kesi hiyo ya msingi itaendelea kusikilizwa, baada ya Jaji Kiongozi Siyani kabla ya kujitoa kutoa uamuzi katika kesi yake ndogo, iliyotokana na mapingamizi ya utetezi dhidi ya maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Adam Kasekwa.

Wakitaka yasitumike mahakamani hapo kama sehemu ya ushahidi wa jamhuri, ukidai yalichukuliwa nje ya muda kinyume cha sheria, pamoja na mtuhumiwa huyo kupewa mateso kabla ya kuhojiwa.

Kwa sababu ambazo alizitoa mara baada ya uamuzi wake dhidi ya kesi ndogo na kuamua kutupilia mbali mapingamizi ya upande wa utetezi.

Lakini katika uamuzi wa mahakama hiyo mbele ya Jaji Kiongozi Siyani, iliyatupilia mbali mapingamizi hayo, hatua inayopelekea kesi ya msingi kuendelea kusikilizwa pale ilipoishia.

Kesi ya msingi ilisimama kusikilizwa tarehe 15 Septemba 2021, baada ya Kamanda wa Polisi Kinondoni, ACP Ramadhan Kingai, kuwasilisha maelezo hayo wakati akitoa ushahidi wake.

Ambapo mawakili wa Mbowe na wenzake, waliweka mapingamizi wakiiomba mahakama hiyo isikubali kuyapokea.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

Habari za Siasa

Serikali kuanzisha mradi wa Gridi ya maji ya Taifa

Spread the loveWaziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika mwaka wa fedha...

Habari za Siasa

Rais Samia aridhishwa utendaji mabalozi, awapa neno

Spread the loveRais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amewapongeza mabalozi  wanaowakilisha ...

error: Content is protected !!