May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tanzania yataja sekta sita kinara utoaji ajira

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania imetaja sekta sita zilizo kipaumbele katika kutoa nafasi za ajira nchini. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Sekta hizo zimetajwa leo Jumatano, tarehe 30 Juni 2021, jijini Dodoma na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiahirisha shughuli za Bunge la 12, zilizoanza tarehe 30 Machi mwaka huu.

Waziri Majaliwa amesema sekta hizo zimebainika baada ya Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), kufanya utafiti mdogo kuhusu hali ya ajira nchini.

“Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania, imefanya utafiti mdogo katika sekta sita za kipaumbele nchini. Utafiti huu umeainisha baadhi ya ujuzi ambao waajiri wanauhitaji,” amesema Waziri Majaliwa.

Waziri Majaliwa ametaja sekta hizo kuwa ni, kilimo na biashara, ambapo ujuzi unaohitajika ni wa ufugaji, mbinu za kilimo, uendeshaji na utengenezaji wa mashine za kilimo.

Sekta ya pili ni utalii na ukarimu, ambayo inahitaji watu wenye ujuzi katika masuala ya mawasiliano ikijumuisha matumizi ya lugha mbalimbali, kuongoza watalii, utunzaji wa nyumba za kulala wageni na maeneo ya wageni.

Bunge la Tanzania

“Sekta ya tatu ni Nishati, ujuzi unaohitajika ni wa kutumia kompyuta katika masuala ya nishati, ujuzi wa masuala ya umeme na ujuzi wa masuala ya nishati jadidifu,” amesema Waziri Majaliwa.

Sekta ya nne iliyotajwa na Waziri Majaliwa ni ya ujenzi, na kwamba ujuzi unaohitajika ni wa uhandisi ujenzi, usanifu majengo na uendeshaji mitambo.

Waziri Majaliwa ametaja sekta ya tano kuwa ni Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

“Ujuzi unaohitajika ni wa kutengeneza na kutunza kanzi data, ujuzi wa mifumo na programu za kompyuta na sekta ya sita ni usafiri na usafirishaji, ujuzi unaohitajika ni wa mawasiliano, matengenezo ya vyombo vya usafiri, Tehama katika mifumo ya usafiri na usafirishajina ujuzi katika kuendesha mitambo,” amesema Waziri Majaliwa.

Aidha, Waziri Majaliwa amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi nchini, ambao utatoa taswira ya hali halisi ya ujuzi.

Ikijumuisha viwango vya ujuzi wa chini, wa kati na wa juu.

“Matokeo rasmi ya utafiti huu yatatolewa mwezi Agosti 2021. Matokeo hayo, yatatuwezesha kufanya mlinganisho wa hali halisi ya ujuzi ilivyokuwa kwa 2014, wakati utafiti ulipofanyika na hivi sasa,” amesema Waziri Majaliwa na kuongeza:

“Kwa kuzingatia afua mbalimbali zilizofanywa na Serikali pamoja na wadau kuhusu kukuza ujuzi wa nguvu kazi ya nchi yetu. Kwa mfano, mwaka 2014 ujuzi wa juu ulikuwa ni asilimia 3.6 ya nguvu kazi, ujuzi wa kati 16.4% na ujuzi wa chini 80% ya nguvukazi yote.”

error: Content is protected !!