May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia ateta na bosi AfCFTA

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) Wamkele Mene, Ikulu Chamwino, Mkoani Dodoma. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Mazungumzo hayo yamefanyika leo Jumatano, tarehe 30 Juni 2021 ambapo Rais Samia amempongeza Wamkele kwa kushinda nafasi ya Ukatibu Mtendaji wa (AfCFTA).

Amemhakikishia Tanzania itashirikiana nae katika kufanikisha utendaji kazi wake katika kulikwamua Bara la Afrika Kiuchumi.

Aidha, Rais amemhakikishia kuwa Serikali iko katika hatua za mwisho za kuridhia Mkataba wa AfCFTA.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa AfCFTA, Wamkele Mene amempongeza, Samia kuwa Rais wa kwanza Mwanamke nchini Tanzania na Rais pekee mwanamke ambaye ni Mkuu wa nchi na Serikali Barani Afrika.

Wamkele ameshukuru kuwa Tanzania imerejea kwenye majadiliano na masuala mengi waliojadili wamekubaliana.

Aidha, Wamkele amemualika Rais Samia kuhudhuria mkutano wa Sekretarieti na kuwa Mzungumzaji Mkuu kwenye mkutano huo wenye lengo la kuandaa Itifaki ya Wanawake katika Biashara (Women in Trade Protocol ) utakaofanyika Jijini Accra nchini Ghana kwa ajili ya Wafanyabiashara ndogondogo.

Kupitia mkutano huo Sekretarieti inatarajia kufanya harambee ya kukusanya fedha kwa ajili ya kuwezesha biashara kutoka taasisi mbalimbali za fedha zikiwemo benki.

Wamkele amemhakikishia, Rais kuwa Sekretarieti ya AfCFTA inakusudia kuhakikisha wanachama wake wote wananufaika kwa usawa kupitia uwekezaji katika viwanda ambavyo vitaongeza minyororo ya thamani ya bidhaa zinazozalishwa katika nchi wanachama.

Katibu Mtendaji wa AfCFTA amempongeza Rais Samia kwa kuirudisha Tanzania katika dhima yake ya uongozi kama alivyowahi kufanya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alikuwa muasisi wa Umajumui wa Afrika (Pan Africanism).

error: Content is protected !!