November 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tanzania wasaka soko la korosho Algeria

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Dk. Damas Ndumbaro amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Algeria, Saad Belabed

Spread the love

SERIKALI imefanya mazungumzo na Algeria kuhusu masuala ya diplomasia ya kiuchumi, ambapo nchi hiyo imeonyesha nia ya kutaka kununua korosho za Tanzania. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Akizungumza na vyombo vya habari leo tarehe 8 Januari 2019, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Damas Ndumbaro amesema Tanzania na Algeria ziko kwenye mazungumzo ya mwisho ambayo yatapelekea kukamilisha zoezi hilo la biashara ya korosho.

Dkt. Ndumbaro ameeleza kuwa, soko hilo limepatikana baada ya kuzungumza na Balozi wa Algeria nchini Tanzania, na kwamba kutokana na mazungumzo hayo, ni wazi kuwa korosho zinazolimwa hapa nchini zitapata soko Algeria.

“Nimekutana na mabalozi wa wawili , balozi wa kwanza ni wa Algeria nchini Tanzania ambaye tumefanya kikao kizuri sana kujadili masuala yanayohusu diplomasia ya kiuchumi, katika mkutano wetu tumeweza kujadili kuhusu suala la soko la korosho, wameonyesha nia ya kutaka kununua korosho. Hivyo tumefanya mazungumzo ya awali, kutokana na mazungumzo ya awali ni wazi sasa korosho ya Tanzania itapata soko Algeria,” amesema na kuongeza Dk. Ndumbaro.

“Na tayari tumewasiliana na wenzetu wa wizara ya viwanda na biashara, wamelipokea suala hili kwa mikono miwili na sasa tunaenda kwenye mazungumzo ya mwisho ambayo yatapelekea kukamilisha zoezi hilo la biashara ya korosho kati ya Tanzania na Algeria.”

Katika hatua nyingine, Dk. Ndumbaro amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli inafanya kila juhudi kuhakikisha inawakomboa kiuchumi wakulima wa Tanzania na hasa katika kutafuta masoko ya mazao nje ya nchi.

error: Content is protected !!