RAIS wa Benki ya Dunia (W.B), Jim Yong Kim aliyehudumu katika wadhifa huo tangu mwaka 2012 hadi mwanzoni mwa mwaka huu, amejiuzulu ghafla. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Kim ambaye alitakiwa kumaliza muda wake mwishoni mwa mwaka 2021, ametangaza uamuzi wake wa kujiuzulu jana Jumatatu tarehe 7 Januari 2019.
Katika tamko lake hakueleza sababu za kujiuzulu, zaidi ya kusema kwamba kazi ya W.B ni ya muhimu katika kipindi hiki kuliko kipindi kingine kutokana na ongezeko la masikini, matatizo ya mabadiliko ya hali ya hewa, njaa na wakimbizi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na W.B kwa vyombo vya habari inaeleza kuwa, Kim atajiunga na shughuli za uimarishaji uwekezaji wa miundombinu katika nchi zinazoendelea pamoja na kurejea katika Bodi ya Shirika la Afya, aliyoianzisha miongo mitatu iliyopita.
Tangu benki hiyo ilipoanzishwa mwishoni mwa vita kuu ya pili ya dunia, W.B imekuwa ikiongozwa na Wamarekani, ambapo viongozi wake walikuwa wanachaguliwa na rais wa Marekani.
Hivyo, Rais wa sasa wa taifa hilo, Donald Trump anatarajiwa kuteua mrithi wa Kim.
Leave a comment